ABU ‘AMMAAR
Baada ya kumshukuru Allah Subhaanahu Wata’ala na kisha kumtakia rehma Mtume wake Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam, tunaukaribisha tena mwezi mtukufu wa Ramadhaan, mwezi ambao Allah Subhaanahu Wata’ala ameteremsha Quraan ndani yake.
Suala hili ambalo wengi wetu tunaweza kujua sababu inayotufanya tufunge ni kwamba Allah Subhaanahu Wata’ala ametuamrisha tufunge. Ni moja katika nguzo tano za kiislamu. Mtume wake Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam pia alifunga na akatufahamisha ni wajibu kwetu kufunga.
Kimsingi Allah Subhaanahu Wata’ala huwa hafaradhishi jambo au kakataza isipokuwa kuna sababu na hekima ndani yake. Hekima tunaweza tukaijua kwa ujumla au tukaweza kufahamishwa kiasi tu na pia tunaweza pia tusijue hekima yake. Hivyo kwa Muislamu kwanza ni wajibu kwake kufuata jambo lililoamrishwa bila ya kutaka kujua sababu, hekima au kwa nini jambo limeamrishwa au kukatazwa.
Kila amali aifanyao binadamu lazima iwe na chanzo na pia iwe na lengo ili iweze kuhesabika kama ni ibada ambayo Allah Subhaanahu Wata’ala atailipa. Chanzo cha ibada hii ya funga ni imani iliyo safi iliyoamini kilillahi na kwa ajili ya Allah Subhaanahu Wata’ala. Si mazoea, wala matamanio au kupata umaarufu na kujulikana na mfano wake.Na lengo ni kupata radhi za Allah Subhaanahu Wata’ala na si vyenginevyo. Ndiyo maana kwa anaefunga hupaswa kila siku yake ya Saumu ajiulize jee amelifikia lengo lililokusudiwa?
Ama kwa kufunga, Allah Subhaanahu Wata’ala ametuelezea sababu na hekima ya kutufaridhishia katika Suuratul Baqarah /183
Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa funga juu yenu kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allah.
Funga ndio njia mojawapo ya kujifunza Taqwa – uchamungu. Na Uchamungu kwa maana nyepesi ni kufanya kila aliloliamrisha Allah Subhaanahu Wata’ala na kuacha kila alilolikataza Allah Subhaanahu Wata’ala.
Hii ndiyo hekima aliyotuelezea Subhaana kwanini ameifaradhisha funga juu yetu na pia kwa kaumu zilizopita.
Maulamaa, Allah Subhaanahu Wata’ala awarehemu, nao wametuongezea faida kwa kutuonesha njia ya kuweza kutufikisha kwenye makusudio yetu ya kuifikia taqwa kama ifuatavyo:
· Funga hutuwezesha Waislamu kufahamu na kuenzi vile ambayo Allah Subhaanahu Wata’ala ameturuzuku katika neema zake. Kwa kuacha kula, kunywa na kustarehe kwa wanandoa ndipo tunapoweza kubaini umuhimu wa neema hizi hasa kwa tuliojaaliwa kuwa nazo na pia kuwakumbuka wasiojaaliwa na hivyo wakati tunapokuwa nazo truzitumie kwa vizuri.
· Funga hutufundisha kuachana na kuepukana na mambo ya haramu. Ikiwa Muislamu ameweza kujiepusha na halali anapofunga kwa kumridhisha Allah Subhaanahu Wata’ala na pia kwa kuchelea adhabu na ghadhabu zake, atakuwa katika nafasi nzuri ya kujiepusha na haramu. Na kujiepusha na haramu ndio uchamungu - taqwa.
· Funga hutupelekea kuweza kuzidhibiti shahawa na matamanio. Kwa aliefunga mwili wake huwa na udhaifu unaompelekea kudhibiti matamanio kwani nafsi ni kawaida kumpeleka mja kwenye uovu. Ama tukiwa na shibe ndipo tunapowaza na kuwazua na nafsi kutuendesha hadi kututumbukiza kwenye maovu.
· Funga hutufundisha kujijenga na tabia ya kuwafikiria na wengine hasa masikini na wasio na uwezo. Kwa aliefunga na kukaa na njaa kwa muda mchache kwa ajili ya ibada humsaidia kumpa fikra ya wasiojiweza ambao hiyo ndio hali yao katika maisha yao. Kwao kupata rizki huwa mtihani na kazi pevu na hivyo kwa waliojaaliwa kuwa na moyo wa kutoa na kuwasaidia kwa kuweza kuiona hali halisi inayowakabili.
· Funga humuumiza shetani na kumdhoofisha. Kwa sababu shetani huingia kwa binadamu kama damu inavyomtembea na funga huizuia njia hii na hivyo kutopata nafasi ya kumtia wasiwasi na athari zake kudhoofika.
· Anayefunga anajipa mazoezi muhimu katika kumkumbuka Allah Subhaanahu Wata’ala kwamba kila wakati anamuona na hivyo kuacha vitu anavyovipendelea licha ya kuwa na uwezo wa kuvitumia. Na hii ndiyo daraja ya Ihsaan – daraja ya juu ya Ibada ambayo ni kumuabudu Allah Subhaanhu Wata’ala kama tunamuona na ikiwa hatumuoni, yeye anatuona.
· Funga hutupa fursa ya kuzidisha na kukithirisha ibada kwani mwezi wa Ramadhaan kwa Muislamu ni mwezi wa ibada na somo hili huondoka nalo hata baada ya Ramadhaan ambazo ibada huwa tayari zimezoeleka na kutekelezwa .
Kwa uchache hizi ni miongoni mwa sababu ambazo Allah Subhaanahu Wata’ala ametuwajibisha tufunge ikiwa ni fardhi kwetu.
No comments:
Post a Comment