Habari za Punde

TUMSIKILIZE MDAU AKIWASHAURI WANAFUNZI


Kwa mara ya kwanza napenda kujitokeza kuwaasa wanafunzi kutambua haki zao na wajibu wao. Inasikitisha kuona asilimia kubwa ya wanafunzi wa hapa Zanzibar kutotambua haki na wajibu wao kama wanafunzi. Wanafunzi wengi hasa wale wanaotegemea Serikali elimu bila ya malipo, hawaithamini elimu wanayoipata na kwao imekuwa kama ni mapitio tu ya maisha yao kwenda skuli na kitu ambacho kitapita na kuondoka. Ni kweli kitu cha kupita na kuondoka lakini hapo kitapoondoka ndipo utajua umuhimu wake kwani Elimu ni Ufunguo wa maisha ni wajibu wako kuutunza na ingawa elimu haina mwisho lakini jali wakati.

Ninachotaka kusema zaidi ni kuwaasa wanafunzi kutumia muda wao vizuri katika masomo yao kwani wakati ni ukuta haumngoji mtu. Ewe mwanafunzi tambua haki zako kama mwanafunzi, nini unapaswa kukifanya na kukipata ili kutimiza malengo yako ya baadae katika maisha yako. Kitu muhimu ni kujitambua wewe ni nani, ukisha jitambua kuwa wewe ni nani hapo utajua nini hasa malengo yako katika maisha. Ishi kwa malengo.

Kuna mfano hai naweza kukupeni. Nilikutana na wanafunzi kwenye daladala. Wanafunzi hao walikuwa wasichana na wavulana. Walikuwa wamegubikwa na mazungumzo yao ambayo yalinigusa hata nikaamua kuandika haya.

Wanafunzi hao walikuwa katika kipindi cha majaribio na hapo walikuwa wahoi na mazungumzo yao yalikuwa ni ya kukata tama. Msichana mmoja alisema kuwa jaribio lilikuwa gumu isitoshe topic iliyotolewa hawakusomeshwa anaamini kapata F akimaanisha jaribio hilo kafeli basi mwenziwe aliruka na kumwambia ikiwa yeye F basi kajipa moyo yeye atapata Z herufi ya mwisho. Kweli inasikitisha kuona bado wanafunzi hawajui haki na wajibu wao.

Kwanza hawajiamini na hawajui thamani ya elimu, na kutojiamini ni kutofikia mafanikio yako. Pili inaonekana hawajui haki zao kwa sababu kama topic hawakusomesha ni nini wajibu wao kati ya haki zao? Isitoshe wanafunzi wengi wamekuwa wakitegemea walimu kuwafundisha kila kitu, hawafahamu kuwa ni wajibu wao kuwa watundu katika kufanya upekuzi wa masomo yao. Ikiwa mwalimu hakufika katika kipindi chake ni wajibu wenu wanafunzi kumfuata na vile vile kwenu nyinyi ni vizuri zaidi kufanya utafiti kwa vitendo msitosheke na chaki za ubaoni pamoja na madaftari yenu.

Napenda zaidi kutoa mfano ili munifahamu nini dhamira yangu kwenu. Ikiwa mmesomeshwa civics na mkajua kuwa sheria hutungwa na Baraza la Wawakilishi au Bunge, basi ni wajibu wenu baada ya masomo kufanya tafiti kuhudhuria hilo baraza kwenda kuuliza maswali mbali mbali yanayohusu Baraza au mmesoma somo la Biology na somo lilikuwa huhusu uzazi au maradhi, mfano Ukimwi au Cholera basi hamna budi pia kwenda hospitali kufanya tafiti za ugonjwa huo kwa kweli akili itafunguka na mtafahamu mengi zaidi ya mliyosomeshwa. Pia kwenye Search Engine kama google pia mtapata mengi zaidi. Mngeweza kutoa changamoto kwa Walime na maskuli ziara hizi za kujifunza zifanyike.

Kwa upande wa Serikali ningependa kutoa maoni yangu machache ambayo yatahitaji kuchambuliwa kwa kina na wizara husika, Labda kungeundwa Jumuiya ya maendeleo kwa wanafunzi wa Zanzibar mfano ZASTUDA (Zanzibar Student Development Association) ambayo itashughulika zaidi na maswala ya wanafunzi wenyewe ikiwa kuwa na mafunzo ya kujiendeleza , kujitambua na kujiamini. Suala zima la kujitolea katika ujenzi wa taifa na mafunzo kwa vitendo, pia kuwa na kongamano kwa ajili ya wanafunzi. Hapo nadhani tutaweza kunyanyua kiwango cha elimu hapa Zanzibar.

Kwangu mimi binafsi nasikitika kwa kupoteza muda wangu nilipokuwa skuli, ni kweli sikuwa na bidii na masomo lakini sasa najua nimeutupa muda wangu na majuto ni mjukuu. Kwa hiyo wanafunzi elimu ni nafasi adhimu katika maisha yenu, mtapokwenda vizuri na maisha yatakuwa mazuri lakini mtapofanya masihara maisha hayataki hivyo, Elimu ndio Msingi wa Maisha.

Ashura M Hamad

1 comment:

  1. Aisee waraka mzuri sana ningeomba mwenye uwezo na aichapishe na wasambaziwe watoto maskuli kiasi ya mtu uwezo wake, nasema hivi sababu naamini wengi wa wanafunzi hawana mitandao majumbani na wala hawana pesa au tabia ya kuenda kwenye cafe, kama watapatiwa waraka huu kwenye karatasi naamini watausoma zaidi ya mara moja na yatakaa akilini.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.