Habari za Punde

RAIS KARUME AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA UINGEREZA STEPHEN OBRIEN IKULU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume, akisalimiana na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Stephen Obrien(Mb) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume, akifuatana na mgeni wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Stephen Obrien(Mb)alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana, mara baada ya mazungumzo yao.

Picha na Ramadhan Othman, Ikulu


Habari na Rajab Mkasaba


UINGEREZA imepongeza hatua zilizofikiwa Zanzibar katika kuimarisha demokrasia hali ambayo imepelekea kufikiwa makubaliano ya kisiasa kwa lengo la kuendeleza amani na utulivu nchini.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza Mhe. Stephen Obrien aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Obrien alimueleza Rais Karume kuwa hatua hiyo iliyofikiwa Zanzibar tayari serikali ya nchi yake inaendelea nayo vizuri na ina matumaini ya kupata mafanikio zaidi.

Obrien alitoa pongezi zake kwa mafanikio hayo na kueleza kuwa kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja nchini ndio muhimili mkuu wa maendeleo endelevu pia, ni ishara kubwa ya kuimarika kwa demokrasia Zanzibar..

Aidha, Naibu Waziri huyo alitoa pongezi kwa Rais Karume kwa kuiongoza vyema Zanzibar katika kipindi chake cha miaka kumi na kusisitiza kuwa mafanikio yaliyofikiwa kiuchumi, kisiasa na kijamii ni ya kupongezwa na kuuungwa mkono.

Akieleza zaidi mafanikio yaliyofikiwa Zanzibar, Waziri Obrien alisema kuwa Zanzibar tayari imejijengea sifa kubwa ulimwenguni kwa kuweza kupata mafanikio katika kupiga vita Malaria.

Kutokana na hatua hiyo, Waziri Obrien alimueleza Rais Karume kuwa ipo haja kwa nchi nyengine duniani kuja kujifunza Zanzibar kutokana na mafanikio yaliopatikana katika kupiga vita maradhi hayo.

Naibu Waziri huyo pia, alieleza haja ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kupiga vita Malaria.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri huyo, alieleza kuwa nchi yake imeridhishwa na hatua za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar na kueleza kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Nae Rais Karume kwa upande wake alitoa pongezi na shukurani zake kwa Uingereza kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo.

Rais Karume alimueleza kiongozi huyo kuwa Uingereza imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kuendeleza Bajeti yake ambapo Zanzibar pia, hunufaika.

Pamoja na hayo, Rais Karume alisema kuwa Zanzibar itafanya kila iwezekanavyo katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kutokomeza Malaria.

Akieleza juu ya mafanikio ya kisiasa yaliyofikiwa hapa Zanzibar, Rais Karume alisema kuwa makubalioano ya kisiasa yameiwezesha Zanzibar kuendeleza amani na utulivu uliopo.

Rais Karume alimueleza kiongozi huyo kuwa hali ya siasa ya Zanzibar ni nzuri na inatoa matumaini makubwa ya kuimarisha mashirikiano, umoja, amani na utulivu.

Sambamba na hayo, Rais Karume alieleza kuwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuimarisha maendeleo yake katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alieleza kuwa miradi ya maendeleo imeweza kuimarika kwa kiasi kikubwa na kuweza kupata mafanikio nchini kote.

Pia, Rais Karume katika mazungumzo hayo na Naibu Waziri huyo hakusita kutoa shukurani zake za dhati kwa Uingereza kupitia Idara inayoshughulikia Misaada ya Kimataifa ya Uingereza (DfID) kwa kuisaidia Zanzibar hasa katika kipindi kilichokosekana huduma ya umeme.

Mhe.Obrien ambaye yupo nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi alimueleza Rais Karume kuwa alipata nafasi ya kutembelea katika Mkoa wa Mtwara ambako ndiko alikozaliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.