Habari za Punde

'OBAMA' ATUMIA KIBAJAJI KUNADI MKUTANO MJI MKONGWE.


Na Salum Vuai, Maelezo, Gazeti la Zanzibar leo, 14-10-2010

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mgombea Uwakilishi Jimbo la Mji Mkongwe, Simai Mohammed Said 'Obama', ameamua kuunadi mkutano wake wa kampeni katika vichochoro vya mji huo kwa kutumia kibajaji.

Mbali ya hali hiyo kutozoeleka, lakini pia hakuna hata mgombea mmoja kutoka chama chochote, aliyejitosa mitaani kutangaza kufanyika kwa mkutano wake wa kampeni.

Wagombea wote wanaowania nafasi za Ubunge, Uwakilishi, Udiwani na hata Uraisi, wanatumia wapambe wa vyama vyao kuitangaza mikutano yao ya kampeni kwa wananchi.

Mkutano huo wa kuomba ridhaa za wapiga kura wa Mji Mkongwe kwa CCM, umepangwa kufanyika leo saa tisa mchana katika viwanja vya Mapembeani, vilivyoko Mwembetanga.

Akiwa ndani ya usafiri huo wa kibajaji kilichopambwa kwa picha zake na rangi za CCM kijani na njano huku akiendeshwa na dereva maalumu, Simai alisimama kila penye mikusanyiko ya watu wengi, na kutoa tangazo la kufanyika kwa mkutano huo kwa kutumia kipaza sauti.

“Haijapata kutokea mgombea kuunadi mwenyewe mkutano wake wa kampeni, mimi nimeamua kuja kwenu kukujulisheni kuwa kesho (leo), tutafanya mkutano na wagombea wenzangu wa nafasi nyengine, nakuombeni mjitokeze kwa wingi kusikiliza sera makini za CCM”, alifahamisha Simai.

Aidha alisema wakifika katika mkutano huo, watafahamu kwa undani juu ya taasisi ya ‘HATUA’ aliyoianzisha kwa ajili ya kushughulikia kazi za maendeleo katika Jimbo la Mji Mkongwe.

Miongoni mwa maeneo aliyosimama kuupigia debe mkutano huo, ni pamoja na maskani maarufu ya wafuasi wa Cham cha CUF ‘Jaws Corner’ iliyoko Sokomuhugo, duka la vitabu na magazeti 'Masomo' Mkunazini, soko kuu la Darajani na mengineyo.

Katika hali inayoonesha kukua kwa demokrasia na Wazanzibari kusahau tafauti zao, alipofika maskani ya ‘Jaws’, Simai aliteremka kutoka katika kibajaji hicho na kukaa kitako na wanachama wa maskani hiyo wakinywa kahawa kwa pamoja.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa walieleza kuvutiwa na staili hiyo ya kuitangaza mkutano wa kampeni, wakisema inasaidia kuwafikia wananchi walio wengi popote walipo.

Simai amekuwa akiitwa Obama kutokana na mvuto na staili anazozitumia kwenye kuomba ridhaa ya kupigiwa kura.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.