Habari za Punde

CHANGAMOTO NYINGI ZAIKABILI BTMZ PEMBA

Na Mwandishi Wetu

AFISI za mabaraza ya michezo katika mikoa miwili ya Pemba, zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi, kutokuwepo ofisi za uhakika na uhaba wa mawasiliano.

Hayo yalibainika wakati wa ziara ya viongozi wa Baraza la Taifa la Michezo iliyofanyika wiki iliyopita, ambapo viongozi wa juu wa baraza hilo kutoka Unguja walitembelea mikoa hiyo kuangalia utendaji..

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa BTMZ, Hassan Khairallah Tawakal, ukosefu wa mawasiliano kati ya watendaji wa ofisi za Pemba na BTMZ Unguja, wanashindwa kuyasimamia na kuyaendesha vyema mabaraza ya michezo ya wilaya ambazo ndio msimamizi mkuu wa michezo wilayani.

Khairallah amesema maafisa hao wameiomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kupitia Kamisheni ya Michezo na BTMZ, kuwasaidia na kuzidisha ushirikiano kwa manufaa ya michezo nchini.

Aidha miongoni mwa shughuli zilizofanywa katika ziara hiyo, ni pamoja na kukutana na viongozi wa vyama vya michezo wakiwemo wenyeviti, makamu wao na wasaidizi makatibu, ambapo matatizo mbalimbali yalitajwa na kuelezewa kuwa ndiyo yanayokwamisha shughuli za michezo.

Katika mkutano huo, ilielezwa kuwa mabaraza ya wilaya yapo kinadharia na utendaji wake hauonekani kwa kukosa nyenzo na mawasiliano na ofisi kuu zilizoko Unguja.

Kutokana na sababu hizo, makatibu na watendaji wengine walishauri yafufuliwe ili yafanye kazi vizuri kwa faida ya michezo nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.