TAARIFA ILIYOTOLEWA NA KATIBU WA KAMATI MAALUM YA NEC ZANZIBAR MHE. ISSA HAJI USSI GAVU KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA VYOMBO MBALI MBALI VYA HABARI
LEO TAREHE 25/07/2011.
Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, jana ilifanya kikao chake cha siku moja cha kawaida, chini ya Mwenyekiti wake ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume, kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui.
Pamoja na mambo mengine, kikao kilipokea na kujadili majina ya wanachama wa UVCCM waliojitokeza kuomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo wa ngazi ya Taifa na hatimaye kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kwa hatua zinazofuata.
Jumla ya wanachama 21 wa UVCCM wamejitokeza kuomba kugombea nafasi hiyo, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Ndg. Hamad Masauni Yussuf, mnamo Mei 18, 2010.
Kikao hicho pia, kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kazi nzuri ya kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 – 2015 pamoja na ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kamati Maalum imempongeza Dk Shein, kwa hatua alizozichukua kwa lengo la kuinua hali za wananchi wake wa Unguja na Pemba za kwapunguzia mzigo wa maisha ili kufanikisha lengo la kupunguza umasikini. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuongeza mishahara ya Watumishi wa Serikali kwa asilimia 25, kupandisha bei ya karafuu kutoka Tsh. 5,000/- hadi Tsh.10,000/-, kwa kilo moja ya daraja la kwanza na Tsh. 9,500/- kwa daraja la pili. Pamoja na kuendeleza Mapinduzi ya Kilimo kwa kupunguza sana bei ya pembejeo za kilimo na gharama za matrekta, ambapo polo moja la mbolea ya TSP itauzwa Tsh. 16,000/-, badala ya Tsh. 32,000/- na UREA Tsh. 10,000/-, badala ya 20,000/-. Hili ni punguzo la asilimia 50%. Aidha, mbegu ya mpunga itauzwa Tsh. 10,000/-, kwa kilo badala ya Tsh. 25,000/-.
Kama hiyo haitoshi, Serikali imepunguza kwa asilimia 75 bei ya kuchimbua na kuburuga mashamba kwa kutumia trekta, kutoka Tsh. 32,000/- kwa heka hapo mwanzo na sasa ni Tsh. 16,000 kwa eka. Aidha, Serikali ya Mapinduzi imepunguza bei ya dawa ya kuua magugu kutoka Tsh. 12,500/- kwa lita hadi Tsh. 6,000/-, ikiwa ni punguzo la asilimia 52%.
Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Zanzibar, imeridhishwa na hatua hizo zilizofikiwa na Serikali na kwamba ni miongoni mwa Utekelezaji kwa vitendo wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Dira ya Maendeleo ya 2020 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar wa mwaka 2010 – 2015 (MKUZA II).
Vile vile, Kikao hicho kimewateua Wajumbe wapya wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar, watakaoongoza Idara mbali mbali za Chama. Wajumbe hao ni pamoja na Mhe. Machano Othman Said, aliyekuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Siasa naUhusiano wa Kimataifa (SUKI) na sasa anakuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC - Organaizesheni.
Wengine ni Mhe. Haroun Ali Suleiman, anakuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Mhe, Issa Haji Ussi (Gavu) - anakuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC - Itikadi na Uenezi, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Mhe. Vuai Ali Vuai, ambaye sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na Mhe. Mansoor Yussuf Himid, ataendelea Kuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC- Uchumi na Fedha.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Issa Haji Ussi Gavu
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar
Itikadi na Uenezi
25 Julai, 2011.
No comments:
Post a Comment