Na Suleiman Masoud, MUM
KATIBU Mkuu Jumuia ya Wakalimani wa lugha ya alama Zanzibar (JUWALAZA), Kheir Muhammed Simai ameishauri jamii kujifunza lugha hiyo, ili kupanua usawa baina ya walemavu wa usikivu (viziwi) na jamii katika kufaidika na matumizi ya lugha kama chombo cha mawasiliano.
Kheir aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika kituo cha kufundishia lugha hiyo kilichopo Magomeni, Mjini Zanzibar.
Alisema, jamii haina budi kufahamu umuhimu wa lugha na kulipa nguvu suala la kujifunza kwani iwapo kutakuwa na ueledi mkubwa wa lugha hiyo, walemavu wa usikivu watashiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Aidha, Khier alisema jamii inapaswa ikumbuke kuwa viziwi nao ni sehemu ya jamii na inapaswa kushiriki katika mambo mbali mbali ikiwemo elimu, mazingira, huduma za afya, warsha, makongamano na semina tofauti.
Alisema, ukalimani wa lugha ya alama ni kazi sawa na kazi nyengine, mkalimani anahitaji kuthaminiwa kama mfanyakazi mwengine.
Alieleza kuwa jumuiya hiyo iko tayari kushirikiana na taasisi nyengine kwa kupokea mialiko mbali mbali itakayohudhuriwa na walemavu wa usikivu na kutafsiri baina ya lugha ya kuzungumza na na lugha ya ishara na hatimae ujumbe wowote unaohitajika kutumwa kwa jamii kuweza kufika kwa watu wote pasi na ubaguzi.
Akizungumzia changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa alisema, ukosefu wa kituo maalum cha kufundishia lugha hiyo kwani hadi sasa wanatumia sehemu ya kujishikiza kwa muda tu.
Hivyo aliwasihi wanajamii kujitokeza kwa wingi kuidhamini kwa kuichangia katika kufanikisha malengo waliyoyakusudia.
No comments:
Post a Comment