Habari za Punde

NCCR - MAGEUZI UNGUJA WAAFIKI MBATIA 'ACHINJWE'

Na Salum Vuai, Maelezo

WENYEVITI wa majimbo ya mikoa mitatu ya Unguja wa Chama cha NCCR-Mageuzi, wametoa kauli ya kuunga mkono hoja ya wajumbe 28 wa halmashauri kuu ya taifa ya chama hicho kutaka kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wake taifa, James Mbatia.

Taarifa ya wenyeviti hao iliyosambazwa kwa vyombo mbalimbali vya habari jana, imesema wameamua kutoa tamko hilo na kuafiki uamuzi wa chama taifa, kutokana na uzito wa hoja hiyo kuwagusa na kukitia doa chama hicho.


Imeelezwa katika taarifa hiyo iliyosaiiniwa na Faki Salum Abdalla kwa niaba ya wenyeviti wa mikoa hiyo, kwamba kitendo kilichofanywa na Mbatia ni kosa na kupoteza sifa za uongozi kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, ibara ya 13 (3 na 8).

Katika kikao cha Novemba 5, mwaka huu kilichofanyika kwenye ukumbi wa iliyokuwa ofisi ya TCD Mikocheni Dar es Salaam, halmashauri ya NCCR Mageuzi ilieleza azma ya kutaka kumsimamisha uongozi Mwenyekiti huyo, kwa kuonekana na mwenendo mbaya, akishutumiwa kutumiwa na walioitwa mamluki wa chama tawala.

Halmashauri hiyo ilimpa Mbatia siku 21 kuwasilisha utetezi wake kabla ya kujadiliwa na kumsimamisha na kufuatia hatua ya kuitishwa mkutano mkuu wa taifa ambayo itakuwa ya mwisho itakayoamua kumsimamisha au kumundoa.

"Sisi wenyeviti wa majimbo ya mikoa mitatu ya Unguja, tupo bega kwa bega na wajumbe hao 28, na tupo tayari kuja kufanya kazi moja ya kuondoa madarakani wakati huo wa mkutano mkuu pindi akishindwa kujiuzulu kwa hiyari yake", ilisema taarifa hiyo ikionesha msimamo wa Wenyeviti hao.

Aidha wenyeviti hao walisema katika siasa za sasa, hakuhitajiki watu wababaishaji kama Mwenyekiti wao wa taifa James Mbatia.

Walivitaja vitendo vibaya vilivyofanywa na Mwenyekiti huyo ambavyo walidai vimeanza siku nyingi, kuwa ni pamoja na kushindwa kupeperusha nembo ya bendera ya chama kwenye slogani zake za kampeni pamoja na vipeperushi mbalimbali alivyotumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, na badala yake alitumia nembo ya bendera ya taifa.

"Je, mbona Mwenyekiti wa CCM alitumia nembo ya chama chake, kwa nini asitumie nembo ya taifa wakati alipogombea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania?", ilihoji taarifa hiyo ya kuunga mkono kusimamishwa kwa Mbatia.

Wenyeviti hao wamesema, hayo na mengine yanaonesha dhahiri kuwa Mbatia ameshapoteza sifa za kuwa kiongozi wa chama hicho, hivyo wanaungana na wajumbe wa halmashauri kuu ya taifa, kumuondoa na kutafuta kiongozi aliye makini katika siasa kuliko kuwa na kiongozi anayeudhalilisha upinzani.

Aidha wamemtaka Mwenyekiti huyo akae kando na kuwapa nafasi wanaotaka kufanya siasa, na pia akiache chama hicho ili kiweze kujipanga vizuri kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.