Habari za Punde

ZANZIBAR HEROES YAREJEA KUTOKA MISRI

Jihad kuikabidhi bendera, kwenda Dar es Salaam leo

Na Salum Vuai, Maelezo

TIMU ya taifa ya soka 'The Zanzibar Heroes', ilirejea nchini jana ikitokea Misri ambako ilikuwa imepiga kambi ya wiki mbili kujiandaa kwa ajili ya michuano ya Chalenji inayotarajiwa kuanza keshokutwa jijini Dar es Salaam.

Msafara wa timu hiyo uliwasili katika uwanja wa ndege wa Zanzibar mnamo saa tano asubuhi, ambapo kocha msaidizi Hemed Suleiman 'Moroko', alieleza matumaini yake kuwa kambi hiyo imesaidia kukiimarisha kikosi chake kitakachoanza kutupa karata yake ya kwanza keshokutwa dhidi ya Uganda Cranes.


Akizungumza mara baada ya kutua Zanzibar, Moroko alisema ingawa siku chache za mwanzo wakati walipowasili Cairo, hali ya hewa ya baridi iliwasumbua mno na hivyo kuchangia kushindwa katika mechi mbili za awali za kujipima nguvu, ambapo ilifungwa 2-0 na Suez, kabla kutandikwa 3-0 na NB.

Aidha alisema, kupoteza michezo yake hiyo kulisababishwa zaidi na kukosekana kwa wachezaji wake mahiri ambao ni mabeki wa kati, akina Nadir Haroub 'Cannavaro', Aggrey Morris, pamoja na mlinda mlango nambari moja Mwadini Ali.

Naye kocha mkuu wa timu za vijana Abdelfatah Abbas aliyekuweko Cairo kusaidiana na Moroko, alisema kimsingi, timu hiyo imeimarika vyema pamoja na kutiwa moyo na ziara na nasaha za Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, aliyetua Cairo kwa muda akitokea nchini Uingereza katika safari ya kikazi.

Akizungumzia kundi la 'B' ambalo timu hiyo imepangwa pamoja na Uganda, Burundi na Somalia, Abbas alisema, anaamini timu hizo zinalingana kiuwezo na Zanzibar Heroes, lakini bado zipo nafasi kadhaa zinazohitaji kuongezewa nguvu katika kikosi hicho.

"Nimewaambia viongozi wa timu wahakikishe wanapata angalau wachezaji wawili miongoni wa wengi wa safu ya ushambuliaji waliopo nchini, pia nafasi ya ulinzi inahitaji kuongezewa zege", alishauri Mmisri huyo.

Wakati huohuo, Zanzibar Heroes inatarajiwa kukabidhiwa bendera na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, katika hafla itakayofanyika kwenye ukumbi wa wizara hiyo Mnazimmoja, kabla kutia mguu kwenye mashindano ya Chalenji yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia, Serengeti (SBL).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.