Habari za Punde

KILI STARS KAMA ZANZIBAR HEROES

Yapita kwa miujiza ya Mungu, yajipeleka kwa Malawi
Zanzibar Heroes mikononi mwa Amavubi

Na Salum Vuai, Dar es Salaam

KILIMANJARO Stars imesonga mbele hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji Afrika Mashariki na Kati, licha kukubali kipigo cha magoli 2-0 mbele ya Zimbabwe, katika mechi ya mwisho hatua ya makundi iliyochezwa uwanja wa Taifa jijini hapa.

Hicho kilikuwa kipigo cha pili kwa mabingwa hao watetezi baada ya awali kuchapwa 1-0 na Rwanda 'Amavubi' kabla ya kuzinduka katika mechi iliyofuata na kuitandika Djibout magoli 3-0.


Kwa ushindi huo, Zimbabwe inaungana na Rwanda kucheza hatua ya robo fainali kutoka katika kundi hilo la 'A' huku Kili Stars ikiingia mshindi wa pili wa waliopoteza ikitanguliwa na Zanzibar Heroes.

Kili Stars sasa itacheza na Malawi katika hatua ya robo fainali siku ya Jumanne jioni ambapo itatanguliwa na mchezo kati ya Uganda na Zimbabwe saa 8: 00 mchana.

Kama ilivyokuwa katika michezo iliyopita, Kilimanjaro Stars, ilionekana kukosa mbinu za kupata magoli hali ambayo iliwafanya mashabiki waendelee kuizomea timu hiyo inayonolewa na Charles Mkwasa na Jamhuri Kihwelu.

Pamoja na kumtumia Mrisho Ngassa ambaye hakuwemo kwenye mechi dhidi ya Djibout, Kili Stars haikuwa na jipya licha ya kupata nafasi kadhaa za kufunga.

Zimbabwe iliandika goli la mapema kunako dakika ya kwanza ya mchezo huo kupitia, Donald Ngoma baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Kili Stars.

Donald Ngoma kwa mara nyengine alizifumania nyavu za Kili Stars katika dakika ya 11.

Lakini Kili Stars ilijipatia goli la kufutia machozi lililofungwa na Mwinyi Kazimoto kwa njia ya penalti mwishoni mwa mchezo baada ya Ngassa kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Erik Muzengwa.

Zanzibar Heroes ambayo ilivuka hatua hiyo kwa mkono wa mungu baada ya kuilaza Somalia magoli 3-0 itacheza na Malawi siku ya Jumatatu wakati saa 10: 00 jioni huku Burundi na Sudan zikiumana saa 8:00 mchana.

Kocha wa Zimbabwe, Norman Mapenza, alisema, vijana wake walicheza vizuri na kustahili ushindi huo muhimu uliowahakikishia hatua ya pili ya michuano hiyo.

"Nimeridhika na kiwango cha vijana wangu, wamefanya vile nilivyokuwa nikitarajia", alisema Mpenza.
Kabla ya mchezo huo, Zimbabwe na Tanzania Bara zilishakutana mara tano huku Zimbabwe ikishinda mara tatu na kutoka sare mara moja nayo Tanzania ikishinda mara moja pekee mwaka 1990.

Kilimanjaro Stars ilishafanikiwa kutwaa ubingwa wa Chalenji mara tatu mwaka 1974, 1994 na 20101.
Zimbabwe kwa sasa si mwanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), lakini iliwahi kunyakuwa ubingwa mwaka 1985 kabla ya kujiondoa na kuhamia kwenye uanachama wa Baraza la Vyama vya Soka la Nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA).

Katika mchezo wa mapema, Sudan ilifanikiwa kuilaza Kenya goli 1-0 na kukata tiketi ya kucheza robo fainali.
Goli pekee la Sudan liliwekwa wavuni na Muawia Bashir kwenye dakika ya 25.

Sudan inaungana na Malawi kucheza hatua ya robo fainali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.