Habari za Punde

Dk Shein Aitaka Bodi ya Mapato Zanzibar Kutumia Teknolojia Kuimarisha Utendaji

Fakih Haji Mbarouk Maelezo Zanzibar 07/01/2012

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Moh’d Shein ametoa wito kwa Bodi ya Mapato Zanzibar ( ZRB )kutumia teknolojia ya kisasa katika kurahisisha mawasiliano na kuimarisha utendaji katika Taasisi hiyo ya fedha..

Amesema kuwa teknolojia ya kisasa ya habari kutarahisisha kufanikisha azma ya kuwa na mtandao madhubuti wa E-Government ambao utaimarisha utendaji kazi katika taasisi za Serikali.


Dk Shein ametoa wito huo huko Mazizuni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati wa ufunguzi wa Jengo la Makao Makuu ya Bodi ya Mapato Zanzibar ililogharimu kiasi cha shilingi Bilioni nane ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ameongeza kwamba kuwa na vifaa vya kisasa vya teknolojia ya habari kutarahisisha kutoa huduma kwa uhakika na salama hasa katika taasisi nyeti ikiwemo bodi ya mapato.

Amesema Serikali itatoa mahitaji yote muhumu ili kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi katika taasisi hiyo

Aidha Dk Shein amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi na Mipango ya Maendeleo itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa uongozi wa ZRB ilikuhakikisha kwamba mapato ya serikali yanakusanywa kwa ufanisi wa hali ya juu na hayavuji,

Hivyo alitoa wito kwa Makatibu Wakuu na Watendaji wWakuu wa Taasisi zote za kiserikali kuchukua hatua za makusudi kwa mwaka ujao wa fedha kuhakikisha kwamba mapato yanayotokana na vianzio mbali mbali iwe ndani ya Wizara,Idara au Taasisi nyengine za Serikali zinakusanywa na kuwasilishwa hazina na kutoa mashirikiano ya hali ya juu na Bodi ya Mapato.

Amesema ni kinyume na utaratibu kutumia fedha za Serikali kabla ya kufikishwa Hazina hivyo ni vyema kwa taasisi kutoa ushirikiana na wafanyakazi wa ZRB wakati wa kufuatilia vianzio vyao vya mapato.

Amesema kumekuwa na ongezeko la mapato kutoka shilingi billion 1.5 kwa mwezi katika kipndi cha miaka minane iliyop[ita hadi kufikia shilingi Bilioni kumi kwa mwezi hivi sasa.

Amesema ongezeko hilo ni la kutia moyo hivyo hakuna budi kuongeza juhudi kwani matumizi ya serikali yanakuwa siku hadi siku.

Aidha aliwataka wafanya kazi wa Bodi hiyo ya mapato kuwa wabunifu wakupanga njia bora za kufanya kazi kulingana na wakati uliopo bila ya kuathiri ukuaji wa biashara na Ajira za Wananchi wa Zanzibar.
Vile vile Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wananchi wa Zanzibar kuwa na utamaduni wa kudai risiti kila wanapo nunua bidhaa kwani bila ya kudai risiti kunaweza kumnyima mtu haki ya kitu chake na pia ni moja ya njia za wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi na kuikosesha serikali mapato.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 07/01/2012


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.