MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi amewataka wananchi kisiwani humo kujadili kwa kina nafasi ya Zanzibar kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati utakapofika wa kutoa maoni juu ya kuandikwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakapofika.
Alisema ili kulifanikisha hilo wakati huo tume itakapopita kukusanya maoni, waache woga, jazba, na wasiwasi na badala yake wajitarishe vyema kwa kuzungumzia kwa kina nafasi ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mkuu huyo wa mkoa, alitoa kauli hiyo ukumbi wa mikutano wa ZSSF, Chake Chake alipofungua mdahalo wa kuwajengea uwezo wananchi juu ya kutoa maoni ya kuandikwa kwa katiba mpya ya Tanzania wakati tume itakayoteuliwa itakapopita.
Dadi alieleza kuwa jazba, woga na fujo hazitosaidia kutoa maoni yao kwenye mchakato huo na badala yake wawe makini kuyaelezea kwa kina mambo wayatakayo kwenye katiba hiyo, ili kuona Zanzibar inafaidika mara dufu kwenye Muungano huo.
Aliendela kueleza kuwa, Katiba katika taifa lolote lile ulimwenguni ndio nguzo kuu na dira kwa maendeleo ya wananchi husika, hivyo katika uandikaji wa Katiba hiyo ni vyema kwa wananchi hao kujipanga ili kupata katiba waitakayo.
“Wananchi hamnabudi kuhakikisha wakati ukifika wa kutoa maoni yenu muwe makini na msisahau kuwa katiba ndio dira na msingi mkuu wa kufikia maendeleo katika taifa hili’’,alifafanua Dadi.
Katika hataua nyengine Mkuu huyo wa Mkoa wa Kaskazini Pemba amewataka wananchi kuifahamu vyema katiba ya sasa na mambo yaliyomo, hilo litasababisha kuwa na mchango mzuri kwenye mchakato wa kukusanya maoni kuelekea kuandika Katiba mpya.
Mapema akitoa maoni yake juu ya mambo yanayopaswa kuingizwa kwenye katiba mpya mwanasiasa, Said Soud alisema kuwa ni vyema katiba hiyo mpya kubanisha juu ya kuwepo kwa serikali tatu ili katika mgawanyo wa rasilimali za muungano kuwepo kwa uswa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano.
Soud alieleza kuwa Tanzania ilipaswa iwe na katiba tatu moja ikiwa ya Zanzibar, Tanganyika, na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo itakuwa ikijumuisha pande mbili za Muungano huo.
Naye Nassor Harith alisema katiba ijayo ni vyema ikaweka mgawanyo sawa wa misaada na rasilimali za Muungano ili nayo Zanzibar ineemeke na matunnda ya Muungano huo na sio kama ilivyo sasa.
Aidha wananchi wengine waliochangia kwenye mdahalo walisema, ni vyema kabla ya kupita kwa tume maalum wananchi wakaendelea kuelimishwa juu ya njia bora na sahihi ya kutoa michango yao wakati tume hiyo itakayoteuliwa itkapoanza kazi rasmi.
Nae Mwenyekiti wa mwemvuli wa Jumuia zisizo za Serikali Kisiwani Pemba, Abubakary Mohamed, ambao ndio walioandaa mdahalo huo alisema kuwa, wanajipanga ili kuhakikisha wanagawa kopi za katiba kwa wananchi wa Pemba ili kuzisoma na kuzifahamu.
Aliongeza kuwa pamoja na ahadi hiyo ni vyema kwa wale walio na uwezo kuzitafuta katiba zote mbili kuzisoma na kuzifahamu ili wakati utakapofika waweze kuchangia mambo wanayoyafahamu.
Mdahalo huo ambao uliwashirikisha wananchi wa makundi mbali mbali ikiwa ni pamoja na wasomi, wananchi wa kawaida, wenye ulemavu na viongozi wa jumuia za kiraia ulikuwa na lengo la kuwajengea uwezo wananchi ili kuwaweka tayari wakati utakapofika wa kutoa maoni wawe na uhakika.
No comments:
Post a Comment