Habari za Punde

Ripoti ya Tume ya Mv Spice Yatolewa Hadharani

Mustafa Aboud Jumbe pamoja na Wengine Kuchukuliwa Hatuwa za Kinidhamu.

Na Faki Mjaka Maelezo Zanzibar 19/01/2012

Ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv. Spice Islanders 1 imependekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Mustafa Aboud Jumbe pamoja na wahusika wengine wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu kutokana na uzembe waliofanya na kusababisha kuzama kwa Meli hiyo

Akitoa mapendekezo ya Ripoti hiyo leo katika Ukumbi wa Wizara ya Habari Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeyakubali mapendekezo ya ripoti hiyo na kusema itaiachia Mahakama na Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao


Dk.Abdulhamid amesema miongoni mwa watu ambao walibainika na makosa katika ajali hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Haji Vuai Ussi, Mkuu wa kituo cha usimamizi wa usalama wa vyombo vya baharini wa Shirika la Bandari,Usawa Khamis Said na Kaimu Mdhibiti wa Bandari ya Malindi Sarboko Makarani Sarboko.

Wengine ni pamoja na Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku Hashim Ayub ambaye ni Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo la Muyuni, Salim Said Mohammed, Makame Hasnuu Makame na Yussuf Suleiman Issa.

Dk.Abdulhamid amesema wahusika wote waliotajwa katika ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na Captain wa Meli hiyo Said Abdallah Kinyanyite na wasaidizi wake, Afisa usafirishaji wa Shirika la Bandari Hassan Mussa Mwinyi na Mkaguzi wa Meli wa Mamlaka ya Usafisiri wa Baharini Juma Seif Juma watachukuliwa hatua za kisheria kulingana na makosa yao

Mrajis wa meli Abdallah Mohammed Abdallah, Afisa Usalama wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Simai Nyange Simai, na wasimamizi wa watatu wa uingiaji wa abiria katika meli hiyo Yussuf Suleiman Issa,Shaib Said Mohammed na Juma Abdallah Hussein nao wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu.

Wengine ni Afisa Mkuu wa Mv.Spice Abdalla Mohammed Ali, Mhandisi Mkuu wa Meli hiyo Khamis Ahmada Hilika, Mabaharia wote wa Meli hiyo pamoja na Askari wa Bandarini waliokuwepo zamu katika kupanga abiria siku ya tukio ambao ni Sajent Jumbe Muhaji na Koplo Juma Abdulla.

Akizungumzia juu ya fidia kwa wahanga wa ajali hiyo Dk.Abdulhamid amesema jukumu la kuwalipa wahanga hao liko mikononi mwa wamiliki wa meli hiyo kwa mujibu wa sheria na kwamba vigezo vya kulipwa wahanga vitafuata utaratibu maalum uliowekwa ambapo kwa waliofariki watalipwa si chini ya Sh Milioni Kumi

Kwa waliopata ulemavu watalipwa asilimia 75% ya Fedha watakazolipwa waliofariki dunia ambapo waliokuwemo katika meli hiyo bila kupata ulemavu watapata asilimia 50% ya kiwango hicho.

Kuhusu fedha za michango ya maafa ambazo zimetolewa na taasisi mbalimbali Dk. Abdulhamid amesema fedha hizo zitagawiwa kwa wahusika chini ya utaratibu maalum utakaowekwa na Mfuko wa Kamati ya maafa uliopo chini ya Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais

Aidha Dk.Abdulhamid alisema ripoti hiyo itawekwa wazi na kupatikana katika mitandao na Maktaba kuu ili wananchi waweze kuisoma.

Ripoti ya Tume hiyo iliundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kufuatia kuzama kwa Meli ya Mv. Spice Islanders 1 tarehe 9/09/2011 katika Mkondo wa Nungwi kuelekea Pemba ambapo inasadikiwa ilikuwa na abiria 2470 na tani kadhaa za mizigo

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.