
TAARIFA YA MHE. MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, BALOZI
SEIF A. IDDI KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
(PRESS CONFERENCE), TAREHE 28 FEBRUARI, 2012
Ndugu Wanahabari, Assaalam Aleykum,
Baada ya maelezo hayo mafupi kutoka kwa Bw. Yussuf Omar Chunda, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa katika hali ya uzima na afya njema. Pia kukushukuruni sana waandishi nyote kwa kuitikia wito na kuwa pamoja nasi hapa leo katika mkutano huu. Azma yangu leo ni kutoa taarifa fupi inayohusu majukumu mbali mbali pamoja na mafanikio na changamoto tulizonazo katika ofisi yangu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Kwa ujumla taarifa hii itagusia masuala ya hali ya uchumi nchini kwa jumla na changamoto zake. Pia nitazungumzia juu ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri; shughuli za kuendeleza zao la karafuu; migogoro ya ardhi; shughuli za kilimo; sekta ya elimu, sekta ya maji; shughuli za utafiti, maendeleo ya mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na taarifa ya sekta zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kupitia Wasaidizi wangu, nimeamua kuitisha mkutano huu kwa kuelewa kuwa vyombo vya habari ndio wadau muhimu katika azma ya Serikali ya kuwapatia taarifa wananchi ili waweze kuelewa shughuli zinazotekelezwa na Serikali yao. Hivyo, naomba mnivumilie ili kufanikisha azma iliyokusudiwa.
1.0. HALI YA UCHUMI:
Hali ya Uchumi wa Dunia:
1.1. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) ya mwezi wa Septemba, 2011, uchumi wa dunia utakuwa kwa kusuasua kwa wastani wa asimilia 40 kwa mwaka 2011.
1.2. Kwa nchi zilizoendelea uchumi wao utakuwa kwa wastani wa asilimia 1.5 kwa mwaka 2011 wakati kwa nchi zinazoendelea na zile nchi zilizo chini kiuchumi zinatarajiwa uchumi wao utakuwa kwa asilimia 6.4 kwa mwaka 2011.
1.3. Uchumi wa dunia ukuaji wake unasuasua kutokana na kudorora kwa uchumi wa Ulaya na Marekani na hii imetokana hasa na ongezeko la bei ya mafuta na kushuka kwa biashara katika soko la dunia.
Hali ya Uchumi wa Zanzibar:
1.4. Uchumi wa Zanzibar ulikua kwa asimilia 6.5 mwaka 2010 kutoka asilimia 6.7 mwaka 2009. Sababu za kushuka kwa uchumi wa Zanzibar mwaka 2010 ni pamoja na:-
● Kudorora kwa Uchumi Ulaya na Marekani.
● Machafuko ya kisiasa katika nchi za Mashariki ya Kati.
● Tatizo la umeme nchini; na
● Uzalishaji mdogo wa ndani.
1.5. Uchumi wa Zanzibar ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 mwaka 2011. Matarajio hayo yalitokana na mambo yafuatayo:-
a) Serikali kuchukua juhudi za makusudi za kuongeza uzalishaji wa chakula na hasa zao la mpunga wa kumwagilia maji, ili kupunguza kiwango cha uagiziaji wa bidhaa hiyo kutoka nje.
b) Kuimarishwa kwa miundombinu ya kiuchumi kama vile Uwanja wa Ndege, Barabara na Umeme kwa Pemba.
c) Uhamasishaji wa uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
d) Kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo kutaongeza kigavi cha mapato ya ndani kwa Pato la Taifa na kufikia asilimia 20.2.
e) Kuimarishwa kwa rasilimali watu, kuweka mazingira mazuri na utendaji kazi na kuinua kiwango cha sayansi, teknolojia na mafunzo kwa vitendo.
f) Kutekeleza mkakati wa usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi kama vile karafuu na mwani.
g) Kuimarishwa kwa sekta ya fedha kwa lengo la kuchangia na kujenga ukuaji uchumi ambao utategemea utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mageuzi ya Sekta ya Fedha.
Hata hivyo, takwimu zinaonesha katika robo ya kwanza ya mwaka 2011 uchumi ulikuwa kwa asilimia 6, na katika robo ya pili ulikuwa kwa asilimia 1.2 kupungua kwa kasi ukuaji wa uchumi katika robo ya pili kulisababishwa na kupungua kwa shuguli za uchumi kama uvuvi, utalii, mawasiliano, uchukuzi na ujenzi. Aidha, sababu nyingine ni msukosuko wa kifedha wa nchi za Mashariki ya Kati na kuendelea kwa tatizo la uharamia katika bahari ya Hindi.
2.0. MFUMKO WA BEI:
Bei ya bidhaa mbali mbali hasa za chakula na mafuta zinaongezeka kwa kasi. Bei ya bidhaa za chakula hapa Zanzibar zimeongezeka kutoka asilimia 3.9 mwezi Oktoba mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 22.5 mwezi Oktoba, 2011. Hali hii imesababisha mfumko wa bei kuongezeka kutoka asilimia 6.6 mwezi wa Januari, 2011 hadi kufikia asilimia 17.4 mwezi Oktoba, mwaka 2011. Mfumko wa bei unaathiri shughuli mbali mbali za kiuchumi kama vile biashara na uwekezaji.
Ongezeko la kasi ya mfumko wa bei Zanzibar katika siku za karibuni linatokana zaidi na mambo yafuatayo:-
a) Uagiziaji mkubwa wa bidhaa za chakula hasa mchele, sukari na unga wa ngano ambazo bei zake zimekuwa zikipanda mara kwa mara katika soko la dunia.
b) Kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa kunakotokana na kuimarishwa kwa ulinzi katika Baharí ya Hindi kutokana na hofu ya maharamia.
c) Kuendelea kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
d) Tatizo la kukatika kwa umeme kusikotarajiwa ambalo linapelekea kupunguka kwa uzalishaji wa ndani wa bidhaa na huduma.
e) Kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine ambapo huzifanya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kuwa ghali zaidi.
Katika kukabiliana na hali hii, Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
a) Imekuwa ikiendelea kupunguza ushuru katika bidhaa za vyakula kama vile mchele, unga wa ngano, sukari na bidhaa nyenginezo ikiwa na lengo la kusaidia wananchi kuweza kujikimu kimaisha.
b) Imewapatia wakulima pembejeo na ushauri kwa lengo la kuwawezesha wananchi walio wengi kuweza kujitegemea kwa chakula na kuongeza uzalishaji wa ndani.
c) Inaendelea kukamilisha mradi mkubwa wa umeme kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba. Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kukabiliana na tatizo la umeme, mazungumzo na wadau mbali mbali yanaendelea Zanzibar ili kuangalia uwezekano wa kupatikana nishati mbadala itakayopelekea kuwa na umeme wa uhakika zaidi. Halikadhalika, Benki Kuu kwa kuzingatia madhara ya mfumko wa bei kwa Watanzania imechukua hatua mbali mbali kuhakikisha kuwa utulivu wa bei unapatikana. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na hizi zifuatazo:-
i) Kupandisha kiwango cha riba ya Benki Kuu (Bank rate) inayotozwa kwa mikopo iendayo katika Taasisi za fedha nchini kutoka asimila 7.58 hadi asilimia 12. Hatua hii imeanza kutekelezwa mara moja tangu tarehe 17 Oktoba, 2011, na inatarajiwa kusaidia kupunguza kasi ya ongezeko la ukwasi (liquidity) baina ya Benki Kuu na Taasisi nyingine za fedha, na hivyo kuleta uwiano kati ya ujazi (volumes/Money supply) wa fedha na mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi.
ii) Kupandisha kiwango cha kisheria kinachotozwa kwenye amana za Serikali katika benki (Statutory Minimum Reserve Requirement on Government Deposits) kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30. Hatua hii imeanza kutekelezwa rasmi tarehe 21 Novemba 2011, na itasaidia kupunguza ukwasi kwenye benki ambazo zimekuwa na akiba kubwa sana ya amana za Serikali ambazo hutumiwa kuikopesha Serikali pesa yake yenyewe kupitia dhamana za Serikali na hati fungani (Treasury bonds). Hatua hii pia itasaidia katika kuhakikisha kwamba ukwasi unaokuwepo kwenye benki unaendana na mahitaji halisi ya kiuchumi na hivyo kupunguza kasi ya mfumko wa bei na hatimaye kupunguza kasi ya kuporomoka kwa thamani ya sarafu.
iii) Kudhibiti ulanguzi au kuotea katika soko la fedha za kigeni. Hatua hizo ni pamoja na kupunguza wigo wa benki kuwa na fedha za kigeni kuliko mahitaji yake ya kibiashara (Net Open Position (NOP). Kwa kawaida benki zinapokuwa na viwango vikubwa mno vya fedha za kigeni huzitumia katika kujipatia faida ambayo haitokani na shughuli za kiuchumi na hivyo kuiangusha thamani ya Sarafu. Benki Kuu imepunguza “Net Open Position“ ya benki kutoka asilimia 20 hadi asilimia 10 ya mtaji wa benki (core capital) ili kupunguza uwezo wa Benki kuotea (speculate) katika sarafu ya Tanzania.
Vile vile, Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kusimamia kwa karibu zaidi shughuli za kibenki nchini na kudhibiti mfumko wa bei kwa kuhakikisha kwamba ukuaji wa ujazi wa fedha unakuwa kwa kasi itakayokidhi mahitaji halisi ya uchumi. Aidha, Benki Kuu itachukua hatua za ziada ikijitokeza haja ili kuhakikisha hali ya utulivu wa uchumi inadhibitiwa ipasavyo.
3.0. MIGOGORO YA ARDHI:
Ndugu Wanahabari,
Hapa Zanzibar wananchi waliowengi wanategemea ardhi kwa kuendesha maisha yao ya kila siku kwa kuitumia kwa shughuli za kilimo, ufugaji, biashara na makaazi. Ni ukweli usiopingika kuwa Zanzibar inakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi katika maeneo karibu yote ya mijini na vijijini Unguja na Pemba. Katika kuipatia ufumbuzi migogoro hiyo Serikali inakusudia:-
§ Kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya ardhi kwa shughuli mbali mbali.
§ Kuhakikisha Viongozi na Watendaji katika ngazi zote wanawajibika katika kusimamia masuala ya ardhi, na wao wenyewe kutokuwa sababu ya migogoro hiyo.
4.0 SEKTA YA MIUNDOMBINU:
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu wa Saba inaendelea na kuweka mkazo wa ujenzi wa muindombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, nishati na kadhalika.
4.1. BARABARA:
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, miradi kadhaa ya ujenzi wa barabara imeendelezwa katika Visiwa vyetu vya Unguja na Pemba, mijini na vijijini. Mradi wa barabara za vijijini Pemba zenye urefu wa kilomita 44.5 ambao ulizihusisha barabara za Mtambile-Mwambe, Mtambile-Kangagani, Mizingani-Wambaa, Chanjamjawiri-Tundaua, Kenya-Chambani na Chanjaani-Pujini ambao ulifadhiliwa kwa msaada wa Norway umekamilika.
Aidha, barabara za Mzambarautakao-Pandani-Finya na Bahanasa-Daya-Mtambwe unaofadhiliwa na Marekani kupitia “Millenium Challenge Corporation” (MCC), na miradi ya barabara za Wete – Gando na Wete – Konde unaogharamiwa na mkopo kutoka BADEA, Saudi Fund na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea.
Kwa upande wa Unguja, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za Mfenesini-Bumbwini, Amani-Dunga na madaraja ya Mwera, Kipange, Majimekundu, Mto wa Pwani na Mwanakombo. Miradi hii inagharamiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, Serikali imo katika hatua za mwisho za kutafuta Wakandarasi wa barabara za Jendele-Cheju-Kaebona, Kizimkazi-Kiboje na Koani-Jumbi.
Matengezo ya barabara za Mwanakwerekwe-Nyumbambili, Kwamchina-Nyumbambili na Mombasa-Mbuyumnene, zimefanyiwa matengenezo makubwa kwa kiwango cha lami kwa kutumia fedha za mfuko wa barabara.
4.2 Usafiri wa Anga:
Katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar unaofanywa na Kampuni ya Kichina Beijing Engineering Construction kwa mkopo kutoka Exim Bank ya China. Aidha, Serikali imekamilisha taratibu za kupata mkandarasi wa ujenzi wa njia za kupitia ndege (Taxiway) na maegesho ya ndege (Apron) mradi ambao unatarajiwa kutekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia. Nia ya kupanua kiwanja cha ndege ni kuendana na wakati tulionao wakati tukitegemea kupokea ndege nyingi kubwa. Uwnja lazima ukidhi kiwango cha Kimataifa.
4.3 Bandari:
Kwa upande wa usafiri wa baharini Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ujenzi wa gati mpya ya Mpigaduri. Tayari utafiti wa awali umeshafaywa. Aidha, Serikali inaendelea na juhudi zake za kutafuta meli za abiria na mizigo kwa usafiri wa uhakika baina ya Visiwa vya Unguja na Pemba. Kwa upande wa sekta binafsi tayari wawekezaji wawili wa vyombo vya baharini wameanza kuleta meli za kuchukulia abiria katika bandari za Unguja na Pemba. Aidha, Serikali kwa kupitia kwa wawekezaji inakusudia kujenga Terminal ya kisasa kwa ajili ya wasafiri wetu.
4.4 Mawasiliano:
Katika kuimarisha huduma za mawasiliano kwa Zanzibar, Serikali inasimamia mradi mkubwa wa uwekaji wa Mkonga wa Mawasiliano ambao utarahisisha mawasiliano ya mtandao wa Internet kwa Visiwa vya Zanzibar.
Vile vile, Serikali inaendelea na hatua za kusimamia mabadiliko ya kiteknolojia ya mawasiliano (TV na Radio) kutoka Analogia kwenda Digitali kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Technolojia ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
5.0 ZAO LA KARAFUU:
Karafuu ni zao pekee linalosafirishwa kwa wingi nchi za nje na bado linaendelea kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu. Kutokana na umuhimu wa zao hilo kwa uchumi wananchi Serikali imefanya yafuatayo:-
i) Kumpa mkulima asilimia 80 ya bei ya soko la dunia.
ii) Imeotesha miche 239.600 na kuwapa wakulima bure. Nia ni kuongeza zao la karafuu kwa kupanda mikarafuu mipya kufidia ile iliyozeeka na iliyokufa.
iii) Kutoa mafunzo ya kuendeleza zao la Karafuu kuanzia vitaluni kwa kulima 250 katika Wilaya 9 za Unguja na Pemba.
iv) Kuanzisha mfuko wa karafuu wenye lengo la kusaidia uzalishaji wa miche na usambazji wake, utafiti na kutoa elimu kwa wakulima. Kwa sasa Serikali inatafutia karafuu ya Zanzibar Hatimiliki (Branding) kwa lengo la kupata bei nzuri na kuepusha isifujiwe na nchi nyingine.
Kuongezeka kwa bei ya karafuu kwa mkulima kumeliwezesha Shirika la ZSTC kuongeza ununuaji wa Karafuu kutoka lengo la tani 3000 hadi kufikia tani zaidi ya 4000 katika msimu uliomalizika hivi karibuni.
6.0 SEKTA YA KILIMO:
Katika sekta ya kilimo Serikali inaendelea na juhudi za kuendeleza kilimo chenye tija na kuliwezesha taifa kuwa na uhakika wa chakula. Katika sekta hii Serikali imefanya yafuatayo:-
§ Jumla ya miche 830,300 ya matunda, viungo na misitu imeoteshwa katika vitalu vya Serikali na miche 450,000 katika vitalu vya watu binafsi.
§ Serikali tayari imetayarisha sera ya uhakika wa chakula na lishe na Sheria Nam. 5 ya uhakika wa chakula na lishe ya mwaka 2011.
§ Jumla ya tani 24 za mbegu ya mpunga ilisambazwa kwa wakulima walioathirika na ukame.
§ Serikali imo katika hatua mbali za utafiti wa mbegu ya NERICA ili kuona inafanikiwa na kutoa mavuno bora itakapogawiwa kwa wananchi na kuanza kuitumia.
§ Lita 10,000 za dawa za kuulia magugu ya mpunga na lita 170 za dawa ya kuulia viwavi jeshi imenunuliwa na kusambazwa kwa wakulima.
§ Utafiti wa mbegu ya mahindi kutoka China unaendelea.
§ Wakulima 296 wamepatiwa mafunzo ya mpunga wa umwagiliaji katika mabonde ya Mtwango, Weni na Mangwena. Wakulima wa mabonde hayo kwa sasa wanaweza kuongeza uzalishaji wa mpunga kati ya tani 4 hadi 6 kwa hekta.
7.0 SEKTA YA ELIMU:
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutoa kipaumbele kwa kuwapatia wananchi wake elimu bora katika ngazi zote. Katika sekta hii miongoni mwa yaliyofanyika ni:-
§ Kukamilisha jumla ya madarasa mapya 132 na kuanza kutumika kwa Unguja na Pemba.
§ Jumla ya madarasa 485 yako katika hatua mbali mbali za ujenzi.
§ Jumla ya vitabu vya kiada 558,104 na vya maktaba 30,260 vya masomo mbali mbali kwa skuli za Sekondari vimenunuliwa na kusambazwa.
§ Kazi za ujenzi wa Skuli 16 kati ya skuli 21 za Sekondari za Wilaya za Unguja na Pemba zinaendelea. Vile vile, matayarisho ya ujenzi wa skuli za Sekondari za Ghorofa za Kiembesamaki, Mpendae, Kwamtipura, Kibuteni na Mkanyageni nayo yanaendelea vizuri.
8.0 SEKTA YA MAJI:
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mazungumzo ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ili kutusaidia mradi wa maji safi na salama wa kuchimba visima 9, kujenga matangi pamoja na kulaza mabomba yenye urefu wa kilometa 10. Mradi huu unategemea kufaidisha jumla ya vijiji 22 kwa Unguja na vijiji 11 kwa Pemba. Aidha, Serikali imekamilisha kazi za ujenzi wa matangi matano, uchimbaji wa visima vinne na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 20 kwa maeneo ya Unguja na Pemba.
9.0 MCHAKATO WA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA:
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imo katika mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshiriki kikamilifu katika matayarisho ya Mswada wa Sheria ya kuweka utaratibu wa kupata Katiba hiyo mpya ya nchi yetu. Ushiriki huo ulifanyika kwa kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na ulizingatia maoni ya wadau mbali mbali wa Zanzibar. Watendaji wetu walishiriki vikao mbali mbali vya kiutendaji vilivyohakikisha kuwa maslahi ya Zanzibar yanazingatiwa katika utaratibu mzima wa kuleta Katiba mpya.
Napenda kutoa wito kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba kujitokeza kwa wingi katika vikao vya kukusanya maoni ya wananchi ili kuhakikisha kuwa tunapata katiba ambayo inazingatia maslahi ya wananchi wa Visiwa hivi. Katika kutoa michango yetu inabidi tuondoe jazba na tutumie busara ili tuweze kutoa michango yenye faida kwetu na muelekeo wa kujenga nchi zetu na uchumi wao.
10.0 TAARIFA YA SEKTA ZILIZO CHINI YA OFISI YA
MAKAMU WA PILI WA RAIS:
Waheshimiwa Wanahabari,
10.1 Miradi ya TASAF:
Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, mradi wenu wa TASAF umeendelea kutoa mchango wake mkubwa wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya zote za Unguja na Pemba katika vita vya kupambana na umasikini. Mradi huu umetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwenye nyanja za kilimo, maji, elimu, afya na uwezeshaji wa wananchi. Jumla ya miradi 78 (Unguja 49 na Pemba 29) yenye thamani ya Shilingi 1,248,066,298 (Unguja 664,886,288 na Pemba 583,180,010) imetekelezwa.
10.2 Uratibu wa Shughuli za Muungano:
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imeendelea kufanya vikao na mazungumzo kadhaa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kuleta maelewano mema ya kudumisha na kuimarisha Muungano wetu. Vikao hivi viliwahusisha maafisa wa ngazi zote kutoka Wizara zote hapa nchini. Katika mwaka huu, vikao vitatu vya ngazi za Mawaziri vilifanyika, vikao 6 vya ngazi ya Makatibu Wakuu na vikao 15 vya ngazi ya Wakurugenzi wa pande zote mbili vilikaa kwa madhumuni ya kukuza maelewano baina ya Taasisi za pande mbili za Muungano.
10.3 Masuala ya Utafiti:
Serikali ya Awamu ya Saba imetoa umuhimu mkubwa kwa masuala ya utafiti ikijua kuwa utafiti ni kicheocheo cha maendeleo katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Katika kutekeleza ahadi aliyoitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2009 ya kuendeleza shughuli za utafiti nchini, Serikali imeanza kutekeleza ahadi zake kwa kiwango kikubwa kwa lengo la kuimarisha miundombinu na kukuza kazi za utafiti nchini. Serikali imetenga TZS. 30 Bilioni (Thelathini Bilioni) kwa kugharamia kazi na shughuli za utafiti nchini. Hivyo, mnamo mwezi wa Septemba, 2010 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa awamu ya kwanza imeshatoa jumla ya TZS 4 Bilioni ( Bilioni Nne) kugharamia shughuli za utafiti nchini. Kwa Awamu ya Pili Serikali imepanga kutoa jumla ya TZS. 15 Bilioni (Kumi na Tano Bilioni) mapema mwaka huu kwa shughuli hizo.
Kwa upande wa Zanzibar, COSTECH inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika azma ya Serikali ya kuendeleza malengo ya rasilimali watu katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo. Aidha, fedha hizo kupitia COSTECH zitatumika katika kuendeleza, kujenga na kukarabati miundombinu ya utafiti hapa Visiwani Zanzibar. Zaidi fedha hizo zitatumika kusaidia na kugharamia kazi za uimarishaji wa teknolojia kwa shughuli za ugunduzi na ubunifu katika fani mbali mbali za maendeleo hapa nchini.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika kuimarisha masuala ya utafiti imeunda Kamati ya watu sita kutoka sekta mbali mbali ili kufanya mapitio ya shughuli za utafiti nchini na kupendekeza juu ya suala hilo, Kamati hiyo inategemea kuwasilisha ripoti yake ya awali mapema mwaka huu.
Kwa kuzingatia kuwa suala la utafiti ni suala la Muungano, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais inashirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa masuala ya utafiti hapa Zanzibar. Kwa kupitia mashirikiano hayo Zanzibar imefaidika na mambo yafuatayo:-
a. Imeutambua ugunduzi na ubinifu wa Bw. Said Omar wa Mpendae wa kuunda gari aina ya SUGU II na imemzawadia cheti na fedha taslim. Aidha, imeahidi kumuedeleza ujuzi wake.
b. Imewapatia msaada wajasiriamali wa kijiji cha Bwejuu wanaotengeneza sabuni kwa kutumia mchaichai wa kushiriki katiko maonyesho ya saba saba mwaka 2011 kwa lengo la kutafuta soko la bidhaa zao.
c. Imesaidia mafunzo ya muda mrefu katika fani ya utafiti kwa wafanyakazi 3 wa Wizara ya Afya Zanzibar.
d. Imekisaidia Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Kizimbani jumla ya Tsh. 641,000,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya utafiti na kukarabati miundo mbinu ya utafiti katika kituo hicho.
e. Imeshirikiana na watalaamu wa sekta mbali mbali katika kuibua vipaumbele vya utafiti na tayari wataalamu kutoka katika sekta ya kilimo, mipango, fedha, uwekezaji, ujasiriamali, wameshiriki katika mikutano hiyo na kazi hiyo bado inaendelea.
10.4 Tume ya Uchaguzi:
Baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010, Tume imeanza matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Matayarisho makubwa kwa sasa yameelekezwa katika mambo matatu yafuatayo:-
a) Kuwajengea uwezo Makamishna na Watendaji wa Tume kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi; kushiriki katika mikutano ya Kikanda na Kimataifa inayohusiana na masuala ya uchaguzi.
b) Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imekamilisha kazi ya kuzifanyia mapitio Sheria ya Tume ya Uchaguzi Nam. 7 ya 1992 na Sheria ya Uchaguzi Nam.11 ya 1984. Kwa muda huu, Tume inaandaa utaratibu wa kufanya mikutano na wadau kujadili mapendekezo ya miswada hiyo ili hatimaye iwasilishwe Baraza la Wawakilishi kwa mjadala wa Baraza. Ni matumaini ya Tume kuwa Sheria hizo zitaanza kutumika katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
c) Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, ilikusudia kuendesha zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kila mwaka kwa kuanzia mwezi wa Oktoba mwaka wa 2011, kwa lengo la kuondoa kasoro ndogo ndogo katika Daftari la wapiga kura. Hata hivyo, kazi hiyo haikufanyika kama ilivyokusudiwa kutokana ukosefu wa fedha. Serikali kwa sasa inaangalia uwezekano wa kuendeshwa kwa zoezi hilo kuanzia mwaka huu.
10.5 Kiwanda cha Uchapishaji:
Serikali imeandaa mpango wa kuimarisha shughuli za upigaji chapa kwa kukihamisha kiwanda kutoka eneo la Saateni kwenda Maruhubi pamoja na kununua mitambo mipya na ya kisasa. Vile vile, kurejesha huduma ya Bohari Kuu ya Serikali ili iweze kutoa huduma ya kuzipatia vifaa mbali mbali Wizara badala ya kutegemea maduka ya binafsi ya stationaries.
10.6 MAAFA:
Ndugu Wanahabari,
Kama tunavyofahamu kwamba nchi yetu ilikumbwa na msiba mzito wa ajali ya kuzama kwa meli M.V. Spice Islander I usiku wa kuamkia tarehe 10 Septemba, 2011 katika mkondo wa bahari ya Nungwi. Katika ajali hiyo, jumla ya wananchi 1529 walipoteza maisha na wengine 941 waliokolewa wakiwa hai. Tunawashukuru wale wote waliotoa msaada wao wa hali na mali katika kukabiliana na maafa yaliyosababishwa na ajali hii.
Kufuatia ajali hii, Taasisi za Serikali na zisizokuwa za Kiserikali, Mashirika, Taasisi za Kidini, Vyama vya Siasa na wananchi kwa ujumla kutoka Tanzania Bara na Zanzibar waliweza kuchangia vifaa, chakula, madawa au fedha taslim kwa ajili ya wahanga hao. Kwa upande wa vifaa kama vile mablanketi na sabuni vimekabidhiwa Wizara ya Afya kwa ajili ya matumizi ya hospitali zetu Unguja na Pemba.
Aidha, madawa nayo yalikabidhiwa Wizara ya Afya kwa ajili ya hospitali zetu. Kwa vile chakula kilichochangwa kilikuwa kidogo kuwagawia wahanga wa ajali hiyo, Serikali iliamua chakula hicho kigaiwe kwa vituo vya kulelea watoto yatima na wazee wasiojiweza Unguja na Pemba.
Ndugu Wanahabari,
Kwa upande wa fedha za maafa ambazo zilikusanywa kupitia michango mbali mbali kama ilivyoelezwa hapo awali, tunaelewa kuwa muda mrefu umepita bila ya wahusika kupata fedha hizo, lakini ziko sababu zilizofanya ucheleweshaji huo utokee. Ilikuwa lazima upite utaratibu wa kuhakiki hali halisi ya suala hilo na hatimae Serikali iweze kutoa maamuzi ya uhakika. Kwa msingi huo, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ambayo tayari imeshakusanya jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Mbili na Thelathini, Laki Mbili na Elfu Tatu, Mia Nane na Sitini na Moja tu (TShs. 1,230,203,861/=) ambazo zote ziko katika akaunti maalum yenye jina la ”Zanzibar Disaster Fund” katika Benki ya Watu wa Zanzibar. Na napenda kuchukua nafasi hii kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuanza kuchukua hatua ya kuzigawa fedha zote hizo kwa wahanga wa ajali hiyo. Kilichobaki hivi sasa ni kusubiri majibu ya zoezi la uhakiki kutoka katika Shehia mbali mbali Unguja na Pemba.
Ndugu Wanahabari,
Napenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia wananchi kwamba wakati zoezi hili la mgao wa fedha za maafa limeanza chini ya usimamizi wa Ofisi yangu na kwa kushirikiana na wadau wengine, Serikali itachukua juhudi kubwa kuona kuwa kila anayestahiki kupata fedha hizo kwa utaratibu uliopangwa, anapatiwa fedha zake bila ya usumbufu. Lakini wakati huo huo napenda kutoa tahadhari kwamba fedha hizo ni kwa wale wahusika tu na ikibainika kwamba kuna mtu amefanya udanganyifu basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Tunawaomba wananchi waendelee kuwa wastahamilivu na kusikiliza vyombo vya habari vya Serikali ambapo hivi karibuni Serikali itatoa utaratibu mzima wa ugawaji wa fedha hizo.
Mwisho, napenda kuwashukuru kwanza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Mohammed Aboud, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Ofisi yangu kwa ushauri na ushirikiano mkubwa walionipa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuwezesha kufanikisha shughulu zetu. Nawaomba sana waendelee na mwenendo wao huo. Lakini pia niwashukuru nyinyi wana habari kwa uvumilivu mliouonyesha na kunisikiliza kwa makini wakati nikitoa taarifa hii. Nakushukuruni sana na ahsanteni sana.
Mwisho
No comments:
Post a Comment