Na Safiya Shamis
KATIKA kuwakuza vijana watakao kuwa na uelewa wa sheria za barabarani, skuli ya chekechea ya Kidutani iliyopo mjini hapa inawafunza wanafunzi wake namna ya kuzitambua na kuzitumia alama za barabarani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwalimu wa skuli hiyo Sabah Muhidin alisema skuli hiyo imeamua kuwafunza alama za barabarani kwani kwa kiasi kibwa wataweza kuepukana na ajali za barabarani.
Alisema unapomfundisha mtoto wa chekechea namna ya kufuata sheria na kuzitumia alama za barabarani, unajenga taifa ambalo litakuwa na watu wenye upeo wa kuziheshimu na kuzisimamia sheria hizo.
Aidha alisema mara nyingi watu hupatwa na ajali ambazo husababisha ulemavu na vifo kutokana na kutozijua sheria za barabarani.
“Ni muafaka kuwafunza watoto wakiwa wadogo kuzijua sheria za barabarani kwani watazitumia na kuzizingatia hali itakayopunguza maafa ya ajali zinazotokea kila siku”, alisema mwalimu huyo.
Alisema mbali ya kuwapa nadharia darasani watoto hao wenye umri wa miaka mitano hadi saba, pia wamekuwa wakifundishwa kivitendo namna ya kuzitambua na kuzitumia alama hizo.
Mwandishi wa habari aliwakuta wanafunzi hao wakiwa na walimu wao wakisaidiwa na askari usalama barabarani Sajenti Ali Kassim na PC Abdulhakim wakiwafundisha namna ya kutumia alama hizo ikiwemo zebra.Zoezi hilo lifanyika jana katika eneo la skuli ya sekondari ya Haileselasi.
No comments:
Post a Comment