KIKOSI cha Zimamoto Zanzibar (KZU) leo kilifanikiwa kuzuia kutokea kwa hasara ya mamilioni baada ya kuuzima moto uliokua ukiwaka katika jengo la afisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) liliopo Kilimani mjini Unguja.
Moto huo uliozua hofu kwa wakaazi wa Mji wa Zanzibar na vitongoji vyake baada ya kuwepo kwa taarifa za kuwaka kwake zilizokua zikitolewa na baadhi ya vyombo vya habari wakati wa tukio.
Kikosi hicho kilifanikiwa kuuzima moto huo uliokua ukiwaka katika chumba kimoja kilichopo ghorofa ya tatu ya jengo hilo, ulioanza kuwaka majira ya saa 4:30 asubuhi baada ya kikosi hicho kupewa taarifa za tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo Msaidizi Ispekta wa Zimamoto, Mwanajuma Mussa alisema kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa chanzo cha moto huo kilisababishwa na hitilafu ya umeme uliokuwepo katika kipozea hewa (AC)cha chumba kilichotokezea moto huo.
Inspekta huyo alisema licha ya kuwepo vifaa maalum vya kuzimia moto wafanyakazi waliokuwepo wakati wa tukio walishindwa kuvitumia jambo linaloashiria kuwa wafanyakazi hao hawapewi mafunzo ya matumizi ya vifaa hivyo.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar , Balozi Seif Ali Iddi alifika eneo hilo muda mfupi baada ya kutokea tukio hilo na kujionea madhara halisi yaliotokezea sambamba na kuwataka Viongozi wa taasisi kutoa mafunzo ya kutumia vifaa maalum vya kuzimia moto ili kuepuka athari mbali mbali zinazoweza kutokea maeneo yao ya kazi.
“Ni vyema kwa viongozi wa taasisi mbali mbali mkawa na utaratibu wa kuwapa mafunzo ya ujasiri wafanyakazi wenu ili waweze kukabiliana na matukio mbali mbali katika sehemu zao za kazi,haiwezekani vifaa vipo moto ndio kwanza unaanza kuwaka mfanyakazi akimbie na kuacha atahri iendeleo wakati alikua anauwezo wa kuizuia” alisema Balozi Seif .
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar,Khamis Fil fil alisema kwa upande wao wanawapa mafunzo wafanyakazi wao ila wafanyakazi waliokuwepo wakati wa tukio walikua ni wa kampuni ya usafishaji hivyo atawashauri kampuni husika kuwapa mafunzo hayo wafanyakazi wao ili waweze kuzuia athari mbali mbali.
No comments:
Post a Comment