Na Mwajuma Saidi
RAIA wa Italia aliyeingia nchini kama mtalii, Peradiso Roberto (42), amefariki dunia usiku wa kuamkia jana huko katika hoteli ya The Residence iliyoko Mchangamle wilaya ya Kusini Unguja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaizidizi wa Polisi Agostino Allomi alisema mtalii huyo alifariki majira ya saa 2 usiku akiwa amepumzika katika kiti.
“Akiwa amejipumzisha kwenye kiti alianguka ghafla na kufariki papo hapo”, alisema Kamanda Ollomi.
Alifahamisha kuwa kabla ya Roberto kufikwa na mauti hayo, mkewe Maritos Sandra (36) raia wa Ufransa alifikishwa katika hospitali ya Mnazimmoja kwa matibabu baada ya kuanguka hafla wakati akiwa choni katika hoteli hiyo.
Kamanda Ollomi alisema uchunguzi unafanyika kufahamu sababu za kifo cha mtalii huyo, na ni tukio la kwanza katika mwaka huu kufariki katika mkoa wake.
Kwa upande wake Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Peradiso, Dk. Marijani Msafiri alisema tayari wamechukua sampuli ya damu na mabaki ya chakula kwa kufanya uchunguzi zaidi.
Dk. Msafiri alisema kuhusu mke wa marehemu huyo, amesafirishwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment