Habari za Punde

Siku ya Watoto Yatima Yaadhimishwa Kiwengwa

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akijumuika pamoja na watoto yatima pamoja na viongozi wa dini na Jumuiya zinazosaidia watototo yatima katika chakula cha mchana huko Kiwengwa mkoa wa Kaskazini Unguja kulikofanyika maadhimisho ya siku ya watoto yatima.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akionyesha zawadi aliyopewa na Jumuiya ya IHH ya Uturuki katika maadhimisho ya siku ya watoto yatima huko Kiwengwa. Kushoto yake ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi akifuatiwa na mwakilishi wa IHH Bw. Yussuf Armagan. 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimkabidhi zawadi mmoja kati ya watoto yatima waliofanya vizuri katika masomo yao ya maandalizi Warda Ramadhan Mgeni, katika maadhimisho ya siku ya watoto yatima yaliyofanyika katika kijiji cha Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

(Picha, Salmin Said, OMKR).

Na Hassan Hamad, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema jamii inapaswa kushirikiana katika kuwasaidia watoto yatima ili waweze kuishi kwa furaha kama walivyo watoto wengine.

Amesema suala la kuwasaidia watoto hao sio la hiari, bali ni jambo lililoamrishwa na Mwenyezi Mungu lifanywe kwa kutegemea malipo mema kutoka kwake siku ya kiyama.

Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa kauli hiyo huko Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika maadhimisho ya siku ya watoto yatima yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Muzdalifah kwa kushirikiana na Jumuiya ya IHH ya Uturuki.


Amesema Serikali kwa wake, inatambua umuhimu wa kuwalea na kuwatunza watoto yatima tokea kuasisiwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar, na kwamba azma hiyo inaendelezwa hadi leo kwa mafanikio.

Amefahamisha kuwa serikali itaendelea kuitekeleza kuitekeleza azma hiyo kwa kuendelea kuwajengea makaazi ya kisasa watoto wetu yatima na kuwapatia malezi ambayo yatazingatia maadili mema.

Ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja kufikiria kuanzisha vituo vya kusaidia watoto yatima au kupeleka misaada katika nyumba za kulelea watoto hao, pamoja na kuwa na utaratibu wa kuwatambua watoto yatima ambao hawaishi kwenye vijiji maalum, ili waweze kusaidia katika mahitaji yao muhimu.

Ameyataja mahitaji hayo kuwa ni pamoja na elimu, kwani kuwapa watoto elimu ni sawa na kuisaidia nchi, kuinua vipaji vya watoto kielimu na kujenga mustakabali mwema wa hapo baadaye.

Maalim Seif ameipongeza jumuiya ya Muzdalif kwa kutoa malezi mema kwa watoto yatima, sambamba na washirika wa maendeleo wanaosaidia malezi hayo zikiwemo Jumuiya ya IHH ya Uturuki na Jumuiya ya WEFA ya Ujerumani.

Katika hafla hiyo Maalim Seif ameahidi kuchangia Komyuta mbili kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao kupata elimu.

Katika risala yao iliyosomwa na mwanafunzi Firdaus Kassim, watoto hao wameiomba serikali kuifanya siku hiyo kuwa ya kitaifa, sambamba na kuanzishwa kwa mfuko maalum wa mayatima ili uweze kusaidia maendeleo ya watoto hao.

Watoto hao wameelezea kufurahishwa kwao na jinsi jumuiya ya Muzdalifah ilivyowaunganisha kuwa kama watoto wa familia moja wakiwa na matarajio ya kuijenga nchi yao kwa pamoja.

Jumuiya ya Muzdalif kwa upande wake imesifu mashirikiano wanayoyapata kutoka serikalini, na kuomba yaendelezwe ili kuleta faraja kwa watoto hao, ambapo hadi sasa wanawasaidia watoto yatima wapatao mia tano kutoka Unguja na Pemba.

Mwakilishi wa Jumuiya ya IHH ya Uturuki Bwana Yussuf Armagan amesema nchi yake inapata faraja kuona watoto yatima wanasaidiwa, na kwamba iwapo watu wengi zaidi watajitokeza kuwasaidia watoto hao wataweza kupata mafanikio yaliyotarajiwa.

Amesema jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inawasaidia watoto yatima katika nchi 130 dunia, itaendelea kutoa misaada yake kwa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanaishi katika mazingira mazuri.

Kauli mbiyu ya maadhimisho hayo yaliyoanza kwa kuwatembelea watoto yatima katika nyumba mbali ikiwemo ya mazizini na kijiji cha SOS ni “watoto yatima tukiwezeshwa, tunaweza”.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.