Habari za Punde

Wahariri Waibue Ajenda za Kusukuma Maendeleo - Kibanda

Na Ramadhan Makame

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri wa Habari Tanzania, Absalom Kibanda, amesema umefika wakati kwa wahaririwa vyombo vya habari hapa nchini kuibua ajenda watakazozifanyiakazi kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya wananchi.

Kibanda alieleza hayo jana mjini hapa kwenye mkutano uliowashirikisha wa Wahariri wa Vyombo vya Habari Zanzibar, ulioendeshwa chini ya Baraza la Habari Tanzania, tawi la Zanzibar (MCT).

Alisema katika baadhi ya mataifa Wahariri wa Vyombo vya Habari huandaa ajenda na kuifanyiakazi kwa lengo la kushindika kuharakisha maendeleo ya wananchi.

“Nadhani imefika wakati sisi kama Wahariri wa Vyombo vya Habari tuwe na ajenda ambayo tutaifanyiakazi kwa pamoja kwa lengo la kuhamaisha maendeleo”, alisema Kibanda.
Akizungumzia juu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema uwepo wa serikali hiyo ni tunu na lulu kubwa kwa Wazanzibari, hivyo ni vyema kuwabainisha viongozi vigeugeu wenye kuipinga kichichini, huku wakiendelea kuwemo kwenye serikali hiyo.

“Kama nyufa zipo tuzieleze kwa ajili ya kujenga jamani sio kubomoa, kama wapo viongozi wakiwa pembeni huiponda tuwabainishe kwa maslahi ya maisha ya wananchi wa Zanzibar”, alisema Kibanda.

Akizungumza katika mkutano huo, Muandishi wa Habari Mkongwe visiwani hapa Salim Said Salim, alisema suali la maadili bado lingali tatizo hasa kwa waandishi wa habari na kutaka kuepukwe utamaduni wa kuongeza chumvi katika habari.

Aidha alisema haifai na si kazi ya vyombo vya habari kushuku shuku mambo na kujifanya kuwa ndio chombo cha kuhukumu watu, huku pia akiwataka wahariri kuacha kujifanya kuwa wanajua kila kitu.

Naye Mkurugenzi wa Shirika Habari Zanzibar (ZBC), Hassan Abdulla Mitawi akielezea uhuru wa habari hivi sasa alisema kwa kiasi hatua zimepigwa ikilinganishwa na zamani ilivyokuwa.

Alisema mbali ya waandishi kutimia uhuru wa katiba, lakini pia wameweza kutumia vyema uhuru uliopo kuelezea jamii mambo mbali mbali yakiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Wakichangia katika mkutano huo, wahariri hao walisema ni vyema Vyuo vya Habari hapa nchini vikatilia mkazo zaidi kwenye ufundishaji wa maadili ambalo limeonekana kuwa tatizo kwa waandishi wengi.
Aidha walisema wakati umefika viongozi wa waandamizi wa serikali kuwekwa kitako na kufahamishwa kuwa vyombo vya habari hivi sasa vimebadilika kuliko wanavyotaka viende.

Mkutano huo wa siku moja ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania tawi la Zanzibar, uliibuka na maazimio kadhaa ikiwemo kutaka mikutano ya wahariri kufanyika mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.