Habari za Punde

Wanamichezo Mkanyangeni Wahimiza ligi yao

Na Omar Hassan, Pemba

WACHEZAJI na wapenzi wa soka katika Jimbo la Mkanyageni wamemuomba Waziri wa Mawasiliano, sayansi na Teknolojia kuharakisha kuanzisha ligi ya Jimbo, ili kukuza kiwango cha soka cha wachezaji wa Jimbo hilo na kuweza kupambana katika ligi mbali mbali.

Ombi hilo walilitoa huko Michenzani katika Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, katika hafla ya kukabidhi jezi kwa timu ya Mageuzi ya Michenzani inayoshiriki ligi daraja la pili Wilaya ya Mkoani.


Wachezaji hao wa Mageuzi walimueleza Mnyaa kuwa ni muda mrefu sasa toka alipowaahidi kuwa ataanzisha ligi ya Jimbo, bila ya kuona utekelezaji wake.

Kwa upande wake Profesa Mnyaa alieleza kuwa ligi hiyo itaanza hivi karibuni na kwamba tayari ameshajipanga na kilichomkwamisha ni muda tu kwa vile yeye anataka ligi hiyo ikiwa inaendelea awepo Kisiwani Pemba ili aweze kuishuhudia.

“Nimeshajipanga, karibuni ligi itaanza, nyinyi fanyeni mazoezi ili muweze kukabiliana vyema kwenye ligi hiyo”, alisisitiza mpenda soka huyo.

Akipokea jezi hizo Katibu msaidizi wa timu ya Mageuzi Ali Makame Mohamed alisema jezi hizo zitawasaidia kwa kiasi kikubwa kwa vile wana uhaba wa jezi.

“Tunazo jezi zisizozidi pea mbili, pia zitatutia hamasa ya kuisaka pointi moja ili tuingie nne bora” alieleza kwa furaha katibu msaidizi wa Mageuzi.

Timu ya Mageuzi ya Michenzani imebakisha pointi moja ili iweze kuingia katika hatua ya nne bora huku ikikabiliwa na michezo miwili, mmoja ukiwa dhidi ya timu ya Kombora ya Mkanyageni na Danger boys ya Kangani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.