Habari za Punde

Wizara ya Mifugo na Uvuvi yakabidhiwa Vifaa vya Maabara Na Mwandishi wetu.

MFULULIZO wa utekelezaji wa ahadi za Rais, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhiwa vifaa mbali mbali vya maabara kwa ajili ya vituo vya tiba na uzalishaji wa mifugo vyenye thamani ya shilingi milioni 150.95.

Sherehe hiyo imefanyika jana katika ukumbi wa uendeshaji wa programu za ASSP/ASPD-L huko Maruhubi Mjini Zanzibar.

Waziri Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Alhabib Fereji, alikabidhiwa vifaa hivyo na Kaimu Waziri wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, ambae ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Ashaaban.

Waziri shaabani katika sherehe hiyo alikabidhi dawa na kemikali mbali mbali za maabara, vifaa vya maabara kwa ajili ya vituo vya tiba na uzalishaji wa mifugo, ambapo alisema ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kupambana na umasikini MKUZA na malengo ya Milenia.

Alisema Wizara hiyo inatekeleza hilo kwa lengo la kumuonfdola umasikini kwa kuwaondoa wafugaji katika uzalishaji duni na kwenda kwenye tija zaidi ili kukuza biashara kwa kuzifanya ziwe zenye tija.

Alisema katika Wizara hiyo hivi sasa inatekeleza miradi kadhaa ambapo kati ya hiyo ni ya ukuzaji wa huduma za kilimo na programu ya kuendeleza sekta ya kilimo eneo la mifugo ikiwa ni hatua ya kuinua hali za maisha ya wakulima na wafugaji.

Alisema mpango huo dhamira yake ni kuona unaongeza kiwango cha uhakika wa chakula ili kuweza kupunguza umasikini ambapo itaweza kuwajengea uwezo kutambua matatizo yao ili yaweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Alisema mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo ni sehemu itayweza kufanikisha ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Ali Mohammed Shein, ya Zanzibar kuwa na mapinduzi ya kilimo.

Alisema tangu kuanza utekelezaji wa programu hizo mwaka 2007 tayari kuna mafanikio kadhaa yameweza kupatikana ingawa hapo awali uliambana na matatizo ya ukosefu wa vifaa.

Alisema kuja kwa vifaa hivyo ni moja ya vitu muhimu vitaweza kuondoa matatizo hayo na kuifanya programu hiyo kufanya kazi zake vizuri huku serikali ikiahidi kuvitunza.

Hata hivyo, Waziri huyo aliishukuru Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD, kwa kujitolea kuwapatia mkopo utaoiwezesha programu hiyo kufanya shughuli mbali mbali kwa lengo la kuwakwamua wakilima na wafugaji.

Nae Waziri Waziri Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Alhabib Fereji, akitoa shukrani zake alisema serikali inathamini kupata msaada huo kwani utaiwezesha sekta ya mifugo kufanya vizuri.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein wakati wa kampeni zake aliahidi kuimarisha sekta ya mifugo kwa kuwa na vifaa vya kisasa katika maabara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.