Habari za Punde

ZFA Yatupa rufaa ya Kikwajuni.

Na Ameir Khalid

KAMATI ya Rufaa na Usuluhishi ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imeitupilia mbali rufaa ya klabu ya Kikwajuni, na kuridhia maamuzi ya adhabu yaliyotolewa awali na ZFA Taifa dhidi ya wachezaji wa timu hiyo.
Kamati hiyo ilikutana Machi 21 chini ya Mwenyekiti wake Mkadam Khamis Mkadam kujadili mambo rufaa hiyo ambapo Kiwajuni ilipinga kufungiwa kwa kocha na wachezaji wa timu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga muamuzi Waziri Sheha ziku ilipocheza na Zimamoto kwenye mchezo wa Ligi Kuu Zanzibar.

Barua iliyotumwa kwa klabu hiyo ambayo ilisainiwa na Katibu wa kamati hiyo Afan Othman Juma, yenye namba ya kumbukumbu KRUT/ZFA/VL 11/18, imeelezea mambo kadhaa ambayo kamati hiyo ilipitia, na hatimae kuona kuwa Kikwajuni ilihusika kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu wakati mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Mao Dzedong.

Miongoni mwa makosa yaliyotajwa kufanywa na timu hiyo, ni pamoja na viongozi wake kushindwa kuzuia fujo hizo, sambamba na mwalimu wao kumuendea mwamuzi mara baada ya mpira kumalizika, na hilo kuwa ndio chanzo vurugu hizo.

Kufuatia matukio hayo na mengine ambayo imehusishwa nayo, kamati imeungana na maamuzi ya ZFA Taifa, kwa kutumia kifungu cha 15 na kutoa adhabu kwa timu hiyo, ya kumfungia kocha Juma Idd Juma kutofundisha na kujihusisha na masuala ya mpira kuanzia tarehe ya barua hiyo hadi kumalizika kwa msimu.

Aidha wachezaji wote waliotajwa katika barua ya ZFA wamefungiwa michezo mitatu inayoandaliwa na chama hicho, pamoja na timu ya Kikwajuni kupigwa faini ya shilingi laki tano ambazo imetakiwa kuzilipa si zaidi Machi 30, 2012, na ikishindwa, ZFA itachukua hatua zaidi kwa mujibu kanuni zake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.