Habari za Punde

Chuo cha Kiislamu Chatimiza Miaka 40


RISALA YA MKUU WA CHUO KWA KUTIMIZA MIAKA (40) TOKEA KUASISIWA CHUO CHA KIISLAMU
MAZIZINI – ZANZIBAR

Mhe mgeni rasmi,
Mhe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna.
Mhe Katibu Mkuu
Mhe, Kamishna wa Wema
Waheshimiwa Wakurugenzi
Viongozi wa Taasisi mbali mbali
Nd. Wageni Waalikwa
Nd. Wakufunzi, Wafanyakazi na Wanafunzi wote
Mabibi na Mabwana na itifaki inazingatiwa.

ASSALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH

Awali ya yote tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambae ameepukana na kila upungufu na Aliye Mkamilifu, Mfalme wa ulimwengu wote, kwa kutupa nguvu leo hii, tukaweza kukutana kwa lengo la kusherehekea kutimia miaka (40), tokea kuasisiwa Chuo cha Kiislamu Mazizini Zanzibar.
Kwa vile sherehe zetu tunazifanya katika eneo la Chuo, itakuwa vizuri sana tueleze kwa ufupi historia ya Chuo hiki cha Kiislamu.


HISTORIA FUPI YA CHUO
Chuo cha Kiislamu Mazizini Zanzibar, kimefunguliwa rasmi tarehe Mosi April 1972 na Baba wa taifa hili la Zanzibar, marehemu mzee Abeid Amani Karume ambapo leo hii chuo kimetimiza miaka 40 kwa ukamilifu.  Ufunguzi huu ulitokana na fikra zake mwenyewe ya kuona kuna haja ya wananchi wa Zanzibar kuwa na Chuo chao cha Kiislamu, na baadae kuwa chuo kikuu.
 Mwaka 1969 marehemu mzee Abeid Amani Karume, alichagua kamati ya wananchi kusimamia ujenzi huo.  Alitoa eneo la Mazizini lenye ukubwa wa ekari 80 kwa ajili ya ujenzi, ambapo hadi leo hii, eneo hilo limebakia ekari zisizo zidi arobaini, hii ni kutokana na kutumika baadhi ya maeneo kwa sababu za kimsingi kiserikali, na maeneo mengine kuchukuliwa kinyume cha malengo .

Wananchi 21 waliochaguliwa kusimamia ujenzi wa chuo kwa niaba ya wenzao bila ya malipo yoyote ni kama ifuatavyo:
1. Bw. Haji wa Haji                          -           Mjini.
2.   “  Muhammed Othman             -           K/Samaki.
3.   “  Shaaban Zahran                      -           Maungani.
4. Bw. Fadhil Mzee                          -           Bweleo
5.   “    Vuai Khamis                         -           Jendele.
6.   “    Fakihi Iddi                            -           Mkokotoni.
7.   “    Fasihi Ahmed                       -           Dimani.
8.   “    Mahmoud Juma                   -           Kiboje.
9.   “     Ali Rijali                               -           Bambi.
10. “     Uzia Mohammed                -           Uroa.
11.  “    Hassan Mwinyi                   -           Kibuteni.
12.  “    Abdalla Othman                 -           Kizimkazi.
13.   Syd,   Nur Abdulqadir                        -           Tunduni.
14.    Bw,  Foum Ame                      -           Kinyasini.
15.  Sh. Ameir Tajo (Mkubwa)      -            Mjini.
16.  Bw. Zamani Haji                       -           Donge.
17.   “    Umbaya Vuai                     -           Chwaka.
18.  Sh.  Mussa Makungu                -           Ndijani.
19.   Bw. Yussuf Bira                        -           Mjini.
20.   “    Hussein Ramadhan           -           Mjini.
21.   “    Suleiman Ali                       -           Bwejuu.

Mnamo Oktoba 1971 kamati ya wananchi waliiomba Wizara ya Elimu kupitia waziri wake Mhe. Hassan Nassoro Moyo, kusimamia mafunzo ya chuo baada ya  kukamilika ujenzi wake.

Dhamira kuu ya Marehemu, Mzee Karume ilikuwa kukigeuza chuo hiki hapo baadae, kiwe Chuo Kikuu cha Kiislamu, kitakachojenga maadili mema ya vijana na kupata taaluma ya dini na maendeleo ya kidunia.  Ndio maana mbali ya kuwa Chuo cha Kiislamu kikisomesha mafunzo ya dini , lakini pia maabara za kisayansi zimejengwa kwa lengo la kusomesha masomo ya maendeleo ya kiteknolojia.   Kwa masikitiko makubwa hadi leo tunatimiza miaka (40) lengo hilo adhimu halikufikiwa.  Mzee Karume alifariki dunia baada ya siku sita tu ya ufunguzi wa chuo, hapo terehe 7/04/1972, Bila shaka serikali inayaendeleza yale yote mazuri yalioachwa na Marehemu. Ndio maana tunaamini kwamba kilichokufa ni kiwiliwili chake tu, lakini mawazo na fikra zake zitadumishwa. Kuna vyuo ambavyo hata miaka kumi haijafika tayari hivi sasa vinatoa digrii ya kwanza na kuhesabika kuwa ni vyuo vikuu, mfano mzuri ni ndugu zetu wa
chuo cha fedha ( Chwaka) kilichoanzishwa juzi tu, sasa kimefikia kuhesabika hivyo.

 Mwaka 1982, Rais wa awamu ya pili Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi, aliunda Taskforce (Kamati maalum) ya wajumbe 14 kwa lengo la kutathmini maendeleo ya Chuo cha Kiislamu na mafunzo ya nyanja zote mbili za kidini na kidunia.

Taskforce, hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Mhe, Aboud Talib Aboud, iliundwa na wajumbe wafuatao:
  1. Mhe. Waziri wa Elimu.
  2. Mhe. Kadhi Mkuu (Shk Habib Ali Kombo)
  3. Sh. Mussa Makungu
  4. Sh. Ameir Tajo (Mdogo)
  5. Sh. Omar Zahran.
  6. Sh. Ahmed Abdulrahim.
  7. Sh.  Ali Khatib Mranzi.
  8. Sh. Juma Abdulwadood.
  9. Sh. Hamza Ali.
  10.  Sh. Saleh Omar Kaab.
  11. Sh. Abeid Marine.
  12. Sh. Khamis Amour.
  13. Sh. Feisal S. Mbamba –  ambae alikuwa ndiye Katibu.

Mnamo 1983 taskforce hiyo ilitoa ripoti yenye mapendekezo kwamba mfumo wa Chuo cha Kiislamu ubadilishwe na  badala yake iundwe, Taasisi ya Mafunzo ya Kiislamu, itakayoundwa kisheria na kupewa uwezo kamili wa kuendesha shughuli zake.  Kwa bahati mbaya ripoti ya Taskforce haikuwahi kufanyiwa kazi na Mhe. Rais Aboud Jumbe, kutokana na mabadiliko ya hali ya kisiasa nchini, iliyopelekea Rais kujiuzulu mwaka mmoja baadae (yaani 1984).

Hata hivyo kampeni za Chuo cha Kiislamu kuelekea Chuo Kikuu ni mtazamo wa baadhi ya viongozi wa serikali, wizara, wakufunzi na wananchi  wa Zanzibar kwa ujumla, ambao wengi wao ni waislamu, ili waweze kunufaika na chuo chao, kielimu kimaadili na kimaendeleo.

Chuo kilipoanzishwa mwaka 1972, kilikuwa na majengo mawili tu.  Jengo la kwanza ni afisi ya utawala na staff ya walimu. Jengo la pili lilikuwa ni la ghorofa moja, lenye madarasa manne juu, na maabara mbili za sayansi chini. Kwa mujibu ya historia, lengo lilikuwa kujengwa majengo mengine manne ya ghorofa kwa plan ya baadae, lakini kwa masikitiko makubwa hii imebakia kama ni ndoto ya alinacha , mpaka hivi sasa hilo limeshindikana utelelezaji wake.

Mwaka 1990 jengo jipya la madarasa ya diploma lilizinduliwa na mwaka moja baadae, kozi ya diploma ilianzishwa. Mnamo mwaka 1995 jengo lenye maktaba ya chuo lilikamilika na kuzinduliwa rasmi kwa matumizi. Mpaka kufikia hii leo chuo kina majengo matatu yenye madarasa 15 staff 3 za walimu, chumba cha komputa, maktaba pamoja na maabara mbili. Majengo hayo huwa yanatumika kwa shughuli za chuo, pamoja na Sekondari ya kiislamu ya mazizini.

Chuo cha kiislamu kinatoa mafunzo ya  Ualimu ngazi ya Cheti mjumuisho,
(Inclusive education), Diploma ya Sekondari (Necta), Diploma ya sekondari ya dini na kiarabu, na Diploma ya msingi. Chuo hivi sasa kina jumla ya wanafunzi 250, 33 walimaza karibuni kwa ngazi ya cheti mjumuisho. Ama wakufunzi ni 50 na wengine 11 wako masomoni, wanaofanya idadi ya wakufunzi wote ni 61, wafanyakazi wengine ni 11 kwa jumla ya staff wote katika chuo cha kiislamu ni 72. Wakufunzi wenye kiwango cha digrii ya tatu (PhD) ni 2, digrii ya pili (Masters) ni 21, digrii ya kwanza 33 na Diploma ni 5 ambawo wanawasomesha wanafunzi wa cheti mjumuisho.

Tunaomba kwa kiwango hicho cha wataalamu wetu hawo, tuanzishiwe chuo kikuu kwa kuanzia na masomo ya dini na kiarabu kwani wakufunzi wake wako wengi, ambawo wanaweza kutoa digrii ya kwanza, hasa kwa kuwalenga walimu waliomo maskulini ambawo wana kiwango cha diploma tangu ilipoanzishwa katika chuo hiki kutoa ngazi hiyo 1990, na ambawo hawajaweza kujiendeleza katika ngazi ya digrii ya kwanza kwa kuchelea gharama kubwa zilizokuwemo vyuo vyengine na kuweza kupata uwezo wa kuenda nje ya nchi.

Hapo kabla, chuo na sekondari ya kiislamu ilikuwa ni kitu kimoja, lakini kwa agizo la serikali, wizara yetu imevitenganisha ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi, hata hivyo tuko pamoja katika mashirikiano kama ilivyo kwa majirani wazuri.

Uongozi uliopo sasa unachukua juhudi kubwa ya kulilinda eneo la chuo, baada ya baadhi ya maeneo kupewa baadhi ya taasisi za serikali, kama vile nyumba ya mayatima ofisi ya Mufti na taasisi nyengine. Baadhi ya taasisi mpaka hii leo bado hawajajenga lakini wamezunguushia uzio maeneo hayo. Jambo la kusikitisha kwa huzuni, baadhi ya maeneo yameshatolewa hati miliki kwa watu binafsi. Jambo ambalo lilitufanya tuchukue hatua kabambe kwa mara mbili tofauti kupigania maeneo hayo yasijengwe, na vyombo vya habari vilipaisha hewani.
Chuo sasa kina ekari 40 tu, ambazo zimepimwa na  Idara ardhi na upimaji tayari  kwa kuwekwa alama maalum (Becon), ambapo Tshs 650,000/- tumeshalipa ili chuo kipate hati miliki ya eneo lake, lakini kwa masikitiko makubwa hadi leo tunatimiza miaka (40) chuo hakijapata hati hiyo, hii ni kwa sababu baadhi ya maeneo yametolewa kwa watu binafsi ambao mpaka hivi sasa yana utata .
Chuo mpaka hivi sasa kinategemea ushahidi wa agizo la marehemu Mzee Karume, katika gazeti la serikali, ya amri ya kutangaza ekari 80 za chuo cha kiislamu, pamoja  na ushahidi wa site plan ya tangu asili inayoonesha eneo hilo. Tunaiomba serikali itusaidie na suala hili ili isitokezee kila muda kuwekwa hewani kama sisi ni wagomvi na hali tunachunga eneo hili kwa maslahi yetu na ya kizazi cha baadae.
Jambo la kufurahisha katika kudhibiti eneo la chuo, tumeshandaa michoro na eneo la ujenzi wa Hall la kimataifa na kuthibitishwa na wataalamu, lenye ghorofa 1. Chini litakuwa ni holi lenye uwezo wa kubeba watu 2000, na juu yake litakuwa na uwezo wa kubeba madarsa 7 na chumba kimoja cha komputa, lakini mpaka hivi sasa hatujapata mfadhili wa uhakika atakae simamia ujenzi wote huo.
Gharama za ujenzi huwo ni Tz/ Shs, 1,590 millioni (yaani bilioni unusu) kwa kauli ya kampuni ya Rans, ambayo ilikubaliana na PBZ kuanza alau msingi wa ujenzi huo hivi karibuni.
Tunatoa shukurani nyingi sana kwa Katibu Mtendaji PBZ ambae aliahidi katika mahafali ya mwaka jana kusaidia sehemu ya ujenzi huo, na harakati ya ujenzi huo anatujulisha kila hatua ya makubaliano na wajengaji, kwa  hivyo tunakuomba mhe, Rais pamoja na Serikali yetu mutusaidie ili kufanikisha azma hii adhim.
Katika kuhakikisha Wakufunzi wanawajibika ipasavyo kwa kutekeleza  wajibu na majukumu yao kikamilifu. Chuo kimeanzisha Idara tano za mafunzo ya Ualimu (Sayansi/Sayansi Jamii/ Lugha/ Ualimu/ Elimu Mjumuisho I.E.).

Pamoja na Idara hizo tano, Chuo pia kimeanzisha Panel za masomo  kama vile; Panel nne za Sayansi, Panel tatu za Lugha na Panel ya Sayansi Jamii.
Vile vile Chuo kimeanzisha Kamati mbali mbali za kusimamia shughuli za Chuo. Kamati hizo ni pamoja na:

1.         Kamati ya Utawala na Fedha.
2.         Kamati ya Usajili.
3.         Kamati ya Taaluma.
4.         Kamati ya Mitihani.
5.         Serikali ya Wanachuo.
6.         Kamati ya Takwimu.
7.         Kamati ya Usafi wa Mazingira pamoja na Club ya Mazingira (Mees).
8.         Kamati ya Michezo.
9.         Kamati ya Ujenzi, Ukarabati na Samani.
10.       Kamati ya Sherehe , Tafrija, harusi na Maafa.
11.       Kamati ya Matunzo ya Wakati.
12.       Kamati ya Usafiri.
13.       Kamati ya Ushauri na Nasaha.
14.       Kamati ya Vyeti.
15.       Kamati ya Chumba cha Computer na ghala.
16.       Kamati ya Da’wa.
17.       Kamati ya B.T.P. (Mazoezi ya ualimu)
18.       Kamati ya Maktaba.
19.       Kamati ya Dakhalia.

UTEKELEZAJI WA MALENGO YA CHUO:
1.                  Uongozi unafuatilia kwa karibu kuona kuwa kila alopewa dhamana anaitekeleza kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa zaidi.
2.                  Njia kuu zote za uchumi na mapato zinasimamiwa kwa karibu na Uongozi wa chuo.
3.                  Uongozi unaagiza kwa watendaji wote kutoa risiti kwa shughuli zote zinazohusu utoaji na upokeaji wa fedha, ili kusudi kukwepa upotevu wa fedha.
4.                  Chuo kimeandaa Idara mbali mbali za masomo pamoja na Wakuu wa Kozi/Panel kwa lengo la kufanikisha malengo ya Taaluma Chuoni.
5.                  Chuo kinaendelea na upandaji wa miti ya matunda katika eneo la chuo, kama moja ya njia ya kulinda mazingira.
6.                  Chuo kimelifanyia ukarabati jengo la ofisi na baadae kinakusudia kufanya hivyo hivyo kwa majengo mengine pale uwezo wa kifedha utakaporuhusu.

Aidha chuo kwa kushirikiana na wizara ya elimu kimezindua tena bodi mpya ya tatu ya chuo, ili kuleta mafanikio, wakati ambapo hapo kabla bodi ziliundwa ili kusimamia maendeleo ya chuo na faida iliwahi kupatikana kwa baadhi ya bodi hizo, lakini hatimae kutoweka.
Wajumbe wa bodi hio mpya iliozinduliwa 31/1/2012 na Mhe, Ramadhani Abdalla Shaaban, ambae karibuni tu hivi ndie aliekuwa waziri wa elimu, wajumbe hawo ni;
(1)   Dr. Issa Haji Ziddy. Mwenyekiti
(2)   Dr. Muhyiddin Ahmad (Mkuu wa Chuo) na Ndie Katibu
(3)   Mhe. Waride Jabu Mbunge wa Kiembe Samaki (Mjumbe)
(4)   Dr. Rashid Hikman (Chuo kikuu Chukwani) (Mjumbe)
(5)   Bi, Mwanate (Chuo Kikuu cha Suza) (Mjumbe).
(6)   Bw, Thani Faki Machano (Elimu Ukaguzi) (Mjumbe).
(7)   Mw. Juma Hamad (Mwl Mkuu Sekondari CCK) (Mjumbe).
(8)   Bw, Rajab Salum Rajab (Mwaakilishi Baraza La Manispaa) (Mjumbe).
(9)   Nd, Khamis Omar Khamis (Rais wa Serikali ya W'funzi (Mjumbe).
Wasaidizi wa Mkuu wa Chuo wameidhinishwa kuhudhuria vikao hivyo kwa ufanisi wa maendeleo nao ni
(10)                       Shk. Suleiman Shaaban Mussa Ms/ Mkuu wa chuo Utawala.
(11)                       Mr. Mkombe Juma Shaame Ms/Mkuu wa Chuo Taaluma.

Kwa mnasaba huo, chuo kimeandaa Tamasha hili la kutimiza miaka 40 ya chuo tangu kuanzishwa kwake, na lengo kuu la sherehe hiyo ni kuzingatia yafuatayo:
  1. Kupiga harambee kwa kuomba msaada wa jengo lililotajwa hapo juu (hall la Kimataifa) na majengo mengineo.
  2. Kuboresha maendeleo ya chuo kufikia lengo la serikali la kuwa chuo kikuu.
  3. Kupatiwa fursa za masomo ya elimu kwa wakufunzi na wanafunzi.
  4. Kuendeleza huduma za maktaba na maabara.
  5. Kutatua kabisa tatizo la usafiri chuoni kwa kununua mabasi mapya na kuzifanyia matengenezo gari zilizopo.
  6. Kuhakikisha kwamba mandhari na mazingira ya chuo yanalindwa, kwa kuzunguushia uzio eneo lote la chuo lililobaki ili kuepushwa kuvamiwa tena, na maeneo yaliyotolewa kwa taasisi nyengine ambayo hayajajengwa kurejeshewa kuwa ni miliki ya chuo kama ilivyokuwa mwanzo.
  7. Kuhakikisha kwamba wakufunzi wanapata makaazi ya nyumba zilizo karibu na chuo ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi.
  8. Matengenezo ya majengo na kujenga ukumbi wa mitihani, maktaba na mikutano.
  9. Kusimamia nidhamu na maadili ya wanachuo kwa lengo la kuleta ufanisi katika tabia, silka na utamaduni wa  mzanzibari.
  10. Kuhakikisha kwamba vifaa muhimu vya ufundishaji na kujifunza vinapatikana chuoni (teaching and learning materials).
  11. Kuhakikisha kwamba komputa zinatosheleza kwa ajili ya mafunzo ya wanachuo.
  12. Kuzalisha walimu na wataalamu wa mambo ya dini watakaostahiki kufanyakazi katika maeneo mbali mbali, kama vile mahkama ya kadhi afisi ya wakfu na mali ya amana na ofisi ya mufti.
  13. Kukuza fani za kisayansi na fani nyenginezo za dini na dunia kwa ajili ya maendeleo ya kila nyanja za mwanadamu katika maisha yake.


Mwisho tunakuomba Mhe waziri uchukue hatua za makusudi kukinusuru chuo  na hali ya uvamizi na kukipangilia malengo ili tuweze kufikia nia ya kuelekea chuo kikuu, aidha tunakuomba uunde chombo katika  kusimamia ujenzi wa uzio wa chuo, ili kulinda eneo lililo salia lisivamiwe tena.  
Tunaomba msaada wako katika kulifanikisha jambo hili la kheri, kwani hakika Allah hapotezi ujira wa mwenye kufanya wema.

Mwisho tunatoa shukurani zetu za dhati  waziri wa Elimu, ambae ndie mgeni rasmi, wa tamasha hili kwa kuacha shughuli zako nyingi na kuja kuungana nasi katika kufanikisha shughuli hii, ya kukumbuka na kuendeleza msingi aliotuachia baba na muasisi wa taifa hili la Zanzibar, tunamuomba Allah amlipe kwa wema wake huo, yeye na wote wengine waliochangia na wataochangia kwenye maendeleo ya Chuo.  Amiin.

WABILAHI – TAWFIQ
WASSALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH




1 comment:

  1. Nitoe pongezi kwa CCK kufisha miaka 40, yaani kimefikia utu uzima. Si nia mbaya chuo kufikia kutowa shahada ya kwanza. Lakni ni vyema kujipanga ili kuweza kutowa shahada itakayo hitajika kwenye soko la ajira. Isije ikawa kilio huko mbele. Tunahitajia ushauri hata wa kitaalamu na kitaaluma ili kuwa na mtaala bora.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.