Habari za Punde

Dk Shein Atuma Salamu za Rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali Said Mwema kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo Marehemu Jenerali Mstaafu Harun Mahundi.

Katika salamu hizo Dk. Shein alisema kuwa yeye mwenyewe binafsi pamoja na wananchi wa Zanzibar wamepata mshtuko na huzuni kubwa baada ya kupata taarifa ya kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Marehemu Harun Mahundi.


Taarifa hiyo alieleza kuwa wengi wana wanamkumbuka Marehemu katika utumishi wake ndani ya kipindi cha miaka kumi (1985-1995) akiwa mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania.

“Namuelewa Marehemu Mahundi kwamba alikuwa ni kiongozi mwaminifu, mwadilifu na mwenye mashirikiano makubwa kwa watu wa rika na jinsia zote, alipenda kupokea ushauri na alikuwa na uwezo wa kutoa uwamuzi wa haraka kwa masuala muhimu huku akiweka mbele maslahi ya Taifa.”, alisema Dk. Shein.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa hata baada ya kustaafu utumishi wake Serikali, Marehemu aliendelea kutoa ushirikiano wake kwa aliyowaachia dhamana, kwa viongozi na wananchi waliohitaji msaada na mawazo yake kutokana na uzoefu mkubwa aliokuwa nao katika utumishi wa umma na masuala mengine ya kijamii na hata kisiasa.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa kifo chake ni msiba kwa Tanzania na kueleza kuwa kupitia kwa Inspekta Jenerali Said Mwema, awasilishe rambirambi zake hizo na za wananchi wote wa Zanzibar kwa familia ya Marehemu Mahundi, wapiganaji wote wa Jeshi la Polisi Tanzania na Watanzania wote.

Salamu hizo, zilimuomba MwenyeziMungu awape moyo wa subira na uvumilivu wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi.Mahundi alifariki dunia Jumaatatu Aprili 2, 2012, mjini Dar-es-Salaam na anatajiwa kuzikwa Jumaamosi wiki hii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.