Joseph Ngilisho, ARUSHA
MSIMAMIZI wa uchanguzi katika jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi amesikitishwa na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kagenzi ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru, alisema kuwa, idadi ya wapiga kura waliojitokeza ni 127,455 lakini waliojitokeza kupiga kura nia 60699 ambayo ni nusu ya idadi ya waliojiandikisha.
Alieleza kuwa idadi hiyo ndogo imetokana na watu wengi katika jimbo hilo kutokuwa na shahada za kupigia kura kwani, hali ambayo imewakosesha fursa na haki ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi wao.
Kagenzi alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanatunza na kuzilinda shahada zao ili kuepuka upotevu, kuibiwa na wengine kuondokana na tamaa ya kuuza shahada zao kwa lengo la kujipatia kipato kwani hali hiyo ni kosa kisheria.
Alisema licha ya tume ya uchaguzi kutoa elimu na hamasa ya kutosha na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi la kupiga kura, kupitia vyombo vya habari vipeperushi, na matangazo mbalimbali lakini ameshangazwa na idadi ndogo iliyojitokeza.
Akizungumzia hali ya tathmini ya zoezi zima la kampeni hadi uchaguzi alisema kuwa, alisema lilikwenda vizuri na kukiri kutawaliwa na changamoto za hapa na pale na kueleza kuwa alipokea malalamiko saba kutoka vyama mbalimbali vya siasa ambayo aliyatatua na wahusika kuridhika.
Hata hivyo alisema kuwa, moja ya malalamiko hayo ni pamoja na vijembe vya kisiasa majukwaani ambavyo vilitolewa wakati wa kuwanadi wagombea mbalimbali, lakini hata hivyo aliweza kuvipatia ufumbuzi mapema na kila upande kuridhika.
Aidha alisema kuwa, zoezi hilo lilifanikiwa kumaliza salama bila kuwa na matukio makubwa na kwamba hadi sasa hakuna malalamiko yoyote yaliyofikishwa ofisini kwake kutoka chama chochote cha siasa hivyo anaamini kuwa zoezi hilo lilienda vizuri na vyama vyote vimeridhika na matokeo.
Akizungumzia usimamizi wa uchaguzi kata ya Nkoarisambu, John Ayo ambaye alinusurika kupigo akidaiwa kubadilisha matokeo katika chumba cha majumuisho alisema kuwa, msimamizi huyo hakuwa akibadilisha matokeo ila alichokuwa akifanya ni kuweka alama ya vema kwenye jina la mgombea aliyeshinda.
Katika hatua nyingine Msimamizi wa uchaguzi huo, Triasias Kagenzi amepongezwa na watu mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Arusha kwa kutoa matokeo vizuri na kutangaza matokeo kwa wakati pamoja na kusilikiza malalamiko ya pande zote kwa kutotumia mabavu katika maamuzi hayo.
Wananchi mbalimbali wamewataka wasimamizi wengine wa uchaguzi kuiga mfano huo ili kuepuka vurugu na umwagaji damu unaosababishwa kucheleweshwa kwa matokeo kwani hali hiyo huibua minong’’ono na kuondoa uaminifu kwa msimamizi wa uchaguzi.
No comments:
Post a Comment