Habari za Punde

Kikwajuni Yakimbia Mchezo

Na Haji Nassor, Pemba

KATIKA hali isiyotarajiwa, timu ya soka ya Kikwajuni, imeondoka kisiwani Pemba jana asubuhi, na kuukwepa mchezo wake wa mwisho wa Ligi Kuu ya Zanzibar dhidi ya Jamhuri uliokuwa ufanyike leo uwanja wa Gombani

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo alilithibitishia Zanzibar Leo kuondoka kwa kikosi hicho jana na kuachia pointi zote tatu kwa wapinzani wao Jamhuri, hatua inayoipa Super Falcon ubingwa kwa asilimia 100.

Hatua hiyo inakamilisha taarifa zilizokuwa zimezagaa kisiwani hapa tangu Jumatano, kwamba ilikusudia kuikimbia Jamhuri kukwepa kufungwa magoli manane ambayo yangeiwezesha Jamhuri kuipiku Super Falcon na kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Awali, akizungumza baada ya mchezo kati ya timu yake na Chipukizi ambao Kikwajuni ilishinda kwa magoli 5-2 juzi Jumatano, Katibu Mkuu wa klabu hiyo Masoud Ali, alikanusha vikali taarifa kwamba timu yake inaondoka leo kuikimbia Jamhuri.

Aidha alikanusha taarifa zilizosambaa kisiwani hapa, kuwa Super Falcon imeifadhili timu yake kwa kila kitu, na kwamba imeitaka iondoke Pemba kabla mechi yake na Jamhuri ili kuiepusha na kipigo kizito kwa lengo la kuihakikishia Super Falcon ubingwa.

“Sisi hatuondoki Pemba mpaka tumalize mchezo wetu na Jamhuri keshokutwa (leo), na wala hatuiogopi kwani hiyo ni timu kama nyengine”, alijigamba Katibu Mkuu huyo.

Hata hivyo, habari za uhakika zilizopatikana na gazeti hili, zimethibitisha kuwa, Kikwajuni imeondoka jana asubuhi katika bandari ya Mkoani na tayari iko Unguja.

Hata kabla ya mchezo wake na Jamhuri ilioukimbia, tayari Kikwajuni imeshateremka daraja baada ya kufanya vibaya katika mechi zake za Ligi Kuu msimu huu unaofikia tamati leo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.