Habari za Punde

Maalim Seif: Filamu Zisipotoshe Azindua filamu 'Toba', Asisitiza Maadili Yalindwe



Na Hassan Hamad, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amesema serikali iko tayari kushirikiana na wasanii katika kuitangaza Zanzibar kimataifa.

Alisema wasanii hasa wa filamu wana mchango mkubwa katika kuitangaza nchi na utamaduni wake, na kuwataka kutumia sanaa hiyo kuelezea hali halisi ya nchi badala ya kupotosha na kuiga mambo yasiyokuwa na faida kwa jamii.

Maalim Seif aliyaeleza hayo juzi usiku kwenye ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani, katika hafla ya uzinduzi wa filamu ya 'Toba' iliyoandaliwa na kampuni ya CY&CL ya mjini Dar es Salaam.

Alisema filamu hiyo ambayo imeonesha mafanikio kutokana na umahiri wa waigizaji wake na maudhui ya dini ya kiislamu yaliyomo, ni mfano wa kuigwa na wasanii wengine katika kujenga picha halisi ya utamaduni wa Zanzibar.

“Sanaa yoyote ile ni kielelezo muhimu cha utamaduni wa watu na jamii maalum, kwa maana hiyo sanaa haina budi kulindwa, kuenziwa na kuendelezwa, lakini vile vile jamii inayohusika ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha sanaa hiyo ndiyo halisi, na wala haiharibiwi na kusababisha utamaduni, silka na mila zao kupotoshwa,” alifafanua.

Alifahamisha kuwa, Tanzania imejaaliwa hazina ya wasanii wazuri, na kuongeza kuwa endapo watajiendeleza wanaweza kufikia upeo wa kutengeneza filamu za kuvutia kama zilivyo za Hollywood na Bollywood za Marekani na India, hali itakayoiwezesha Tanzania nayo kuanzisha tamasha la 'Tanziwood'.

Akielezea kuhusu historia ya filamu Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais alisema nyanja ya filamu Zanzibar ni kongwe na inaelezwa kuwa nchi ya kwanza kuwa na sinema katika eneo la Afrika Mashariki mnamo miaka ya 1920.

Hata hivyo, alisema pamoja na ya sanaa hiyo kupata mafanikio, lakini inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo kuporomoka kwa mila na tamaduni za nchi mbalimbali hasa zilizo maskini, na kuwataka wasanii kuwa makini wakati wanapowasilisha sanaa zao, ili kulinda mila na silka za jamii zao.

Mapema akisoma risala kwa ajili ya uzinduzi huo, mjumbe wa kamati ya maandalizi Zanzibar Nassor Ameir Nassor, alisema wameamua kufanya uzinduzi huo Zanzibar ili kutoa fursa kwa wasanii chipukizi wa hapa kujifunza na kupata ukomavu wa sanaa hiyo.

Ameitaja sababu nyengine kuwa ni pamoja na Wazanzibari kuwa jamii ya watu waliofungamana na tabia njema kutokana na mila na silka zao za asili, pamoja na nchi ya Zanzibar kuwa kitovu cha elimu ya dini ya Kiislamu.

Uzinduzi huo uliopambwa pia na kasida za madrasa mbalimbali za Zanzibar, ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk aliyekuwa wa kwanza kununua CD ya filamu hiyo kwa shilingi laki mbili, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.