Habari za Punde

Mfuko Zanzibar Heroes Waanza Kutuna. Zanzibar Ocean View Kuihudumia Malawi Kila Kitu

Na Salum Vuai, Maelezo
WADAU wa soka Zanzibar, wameanza kuitikia wito wa kuichangia timu ya Taifa Zanzibar Heroes, inayojiandaa kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizokuwa wanachama wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kuanzia juzi, mfuko wa timu hiyo umeanza kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali, ambapo jana, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Malindi Jeff Babu, aliwasilisha shiluingi laki tatu, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub akatoa shilingi laki moja, huku klabu ya Kikwajuni ikichangia shilingi 50,000.

Ofisa Habari wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa Munir Zakaria, amesema kabla ya michango hiyo, uongozi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View ulitoa shilingi laki tano, sawa na duka la samani la 'Royal Furniture' lililoko Kibweni, na timu ya Uhamiaji SC ikachangia shilingi 50,000.

Katika hatua ya kuhamasisha wadau, wajumbe wa Kmati Tendaji ya ZFA, ilikusanya michango ya wajumbe iliyofikia shilingi 540,000, huku mwanahabari Daudi Ismail akitoa shilingi 15,000.

ZFA imesema inahitaji shilingi milioni 40 kuiwezesha Zanzibar Heroes kusafiri na kushiriki mashindano hayo ya dunia yanayoshirikisha timu za taifa za nchi tisa, yanayotarajiwa kuanza Juni4, mwaka huu nchini Kurdistan.

Katika hatua nyengine, uongozi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyoko Kilimani mjini Zanzibar, umejoiga kifua kuihudumia timu ya Taifa ya Malawi kwa kila kitu, wakat ikiwa kisiwbnai hapa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes unaotarajiwa kufanyika Jumatatu ya Mei 28 kwenye uwanja wa Amaan wakati wa usiku.

Mkurugenzi wa hoteli hiyo Amani Ibrahim Makungu, amesema hoteli yake itawapa huduma za malazi, chakula na usafiri wa ndani kwa muda wa siku mbili wachezaji na viongozi wa timu hiyo, ambazo thamani yake inakisiwa kuwa shilingi milioni saba na laki tano.

Amesema hatua hiyo inalenga kuisaidia ZFA ili fedha zitakazopatikana kwa viingilio vya mchezo huo, ziweze kutunisha mfuko wa Zanzibar Heroes kwa ajili ya ushiriki wake kwenye michuano yake ya dunia nchini Kurdistan.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.