Habari za Punde

Mzee Small augua ghafla


MWIGIZAJI mkongwe wa vichekesho nchini, Saidi Ngamba, maarufu Mzee Small, amelazwa katika hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua ghafla.

Mzee Small anayesumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu kiasi cha kushindwa kuzungumza, aliugua ghafla juzi jioni muda mfupi baada ya kutoka Mwanza alikokwenda kwenye shughuli za kisanii.

Mwigizaji mwenzake Chausiku Salum Maele ‘Bi Chau,’ amesema kabla ya kuugua, Mzee Small alikuwa mwenye afya njema, hadi walipoachana kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wakirejea kutoka Mwanza.

Said Ngamba.( Mzee Small.)
Kwa mujibu wa Bi. Chau, wasanii hao walikwenda Mwanza Ijumaa iliyopita kwa ajili ya kusherehesha shughuli ya watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Albino,’ iliyoandaliwa na madaktari wa hospitali ya Bugando, jijini humo.

“Tuliondoka Dar es Salaam na ndege ya jioni Ijumaa tukalala Mwanza, Jumamosi tukafanya kazi iliyotupeleka. Jumapili jioni tuliondoka Mwanza kuja Dar, sasa kabla sijafika nyumbani kwangu Magomeni nikapokea simu kutoka kwa binti yake Small, akanipa taarifa za ugonjwa, nilishtuka,” aliongeza Bi Chau.

Akizungumza na gazeti la Tanzania Daima, mke wa Mzee Small, alisema bado hali ya mumewe haijatengemaa hivyo kuomba dua za Watanzania.

“Ana tatizo la presha na huwa anajikuna na kuvimba, lakini safari hii amevimba shavu moja na kadiri muda unavyokwenda hali yake inazidi kuwa mbaya,” alisema mke huyo akiwa nyumbani kwake Tabata Kimanga kabla ya kumpeleka hospitali.

Mwenza huyo wa Mzee Small, alisema juzi usiku walimpeleka mumewe hospitali ya KLM iliyoko Tabata, ambapo alipewa dawa ya kupunguza shinikizo la damu na kuruhusiwa kurudi nyumbani, lakini hali ya msanii huyo iliendelea kuwa mbaya hadi alipokimbizwa hospitalli ya Amana jana mchana.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.