Habari za Punde

Nguvu za wananchi kujiletea maendeleo ziungwe mkono - Dk.Shein

Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein, ameitaka Wizara ya Afya Zanzibar kutekeleza
maagizo yake ya kuchangia nguvu za wananchi katika miradi ya
maendeleo ya ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea maeno mbali mbali ya
Unguja na Pemba.

Dk. Shein aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi katika ziara
ya Mkoa wa Kusini baada ya kuweka mawe ya msingi ya vituo vya afya,
nyumba za madaktari na ujenzi wa kuongeza madarasa kupitia mchango wa
Wazanzibari walionje ya nchi.

Dk.Shein alisema anashangazwa na wizara hiyo ya afya kuwa bado hadi
sasa haijaweza kuweka mpango wa kuanzisha uchangiaji wa miradi ya
maendeleo ya ujenzi wa vituo vya afya ingawa tayari alishatoa agizo
hilo kwa muda sasa.

Alisema kama Serikali haiwezi kuepuka kuchangia nguvu za Wananchi na
anashangazwa kwa Wizara hiyo haina hata mpango wa aina hiyo na kuamua
kuacha kazi hiyo kufanywa moja kwa moja na wananchi.

Alisema nguvu za wananchi zinahitaji kuthaminiwa na haiwezekani
kuachwa kutoungwa mkono na serikali na ni lazima wizara ifikirie kuwa
na mpango huo ili kuutekeza hapo baadae.

Alisema kuanzia sasa serikali inataka kuona Wizara hiyo katika mipango
yake ijayo ya Bajeti inakuwa na fungu la kufanyia kazi hizo kwani
uwezekano wa kufanya hivyo inaonekana upo ndani ya wizara hiyo.

Alisema hivi sasa wizara ya elimu imekuwa ikisaidia mchango wa
wananchi kwa kuwaachia kujenga majengo katika hatua za awali na baadae
katika umaliziaji imekuwa ikifanya kazi hiyo jambo ambalo limekuwa
likiwapa moyo wananchi.

Alisema anasikitishwa kuona Wizara hiyo kwa muda mrefu ameiagiza kuwa
na mpango wa kuchangia vituo vya afya kwa kuvimaliza baada ya wananchi
kujitolea lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.

Akitoa mfano alisema katika ujenzi wa kituo cha Afya cha Kwamtipura na
Mpendae, aliagiza kumalizwa kwa majengo yake na Wizara hiyo, lakini
hadi sasa hakuna kilichofanyika.

Alisema hafahamu ni kwanini Wizara hiyo inashindwa kulitekeleza hilo
wakati serikali ikifahamu fika kuwa wapo wafadhili wanaoweza
kuisaidia Wizara hiyo kama inavyotokea katika sekta ya Elimu.

Alisema kuacha kuchangia sekta hiyo katika miradi ya wananchi hiyo ni
aibu kubwa kwa serikali kuacha kuwaunga mkono nguvu za wananchi wakati
wao wakiwa tayari wameamua kuichangia serikali yao.

“Napata tabu sana kuona Wizara ya Afya mara nyingi nilishawaambia
kuchangia miradi ya wananchi katika maendeleo ya kukuza vituo vya Afya
lakini cha kushangaza sana hakuna lililofanyika” alisema Rais.

Akiendelea alisema atachohakikisha ni kuona kwa Wizara hiyo mwakani
katika bajeti yake lazima itenge fedha kwa ajili ya kusaidia miradi
hiyo ya maendeleo ya ujenzi wa vituo vya afya.

Aidha Dk. Shein aliwapongeza wananchi kwa mchango wao mkubwa
waliojitolea kuona wanaibadili sekta ya afya kwa kuamua kuwajengea
vituo vya afya pamoja na nyumba za madaktari.

Dk. Shein aliwataka wananchi hao kuona mchango wao huo wanauendeleza
ili kuifanya sekta ya afya kuwa yenye kutoa huduma bora kwa wananchi.
Vile vile, Dk. Shein aliipongeza Idara ya Diaspora kwa jitihada
inazozifanya za kuwashajiisha wazanzibari kuchangia maendeleo ya
wananchi wa Zanzibar.

Alisema ameamua kuanzisha idara hiyo kwa lengo la kuwaunganisha
Wazanzibari katika kuchangia maendeleo ya Zanzibar na kuanza
kujitokeza kwa baadhi ya Wazanzibari kuchangia maendeleo ya Zanzibar
ni hatua nzuri.

Alisema Serikali ya Zanzibar itathamini mchango wa taasisi hiyo na
kuwatolea wito wazanzibari ambao bado hawajaitumia taasisi hiyo kuona
inatumia nafasi hiyo ili kuchangia maendeleo ya Zanzibar.

Akiendelea alisema hivi sasa serikali imefarajika kuona tayari baadhi
yao wameanza kujitokeza na kujenga skuli, vituo vya afya pamoja na
kutoa vifaa kwa ajili ya kuwapatia huduma bora wananchi.

Akizungumzia juu ya maendeleo ya ujenzi wa skuli, pia aliwapongeza
wananchi wa Unguja Ukuu kwa mchango walioutoa wa kuhakikisha
wanashirikiana na kamati za maendeleo za maeneo yao kujenga majengo
mapya.

Alisema hiyo itaongeza idadi ya watoto kuweza kupata nafasi nzuri za
kusomea masomo yao bila ya kupata usumbufu katika kupata elimu.
Akiendelea Dk. Shein aliwataka wananchi kuona wanathamini miradi
wanayopatiwa na Wawekezaji ili waweze kuwapa moyo kuendelea kuwasaidia
hapo baadae na sio kuifuja jambo ambalo linaweza likawavunja moyo.

Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya Mkoa huo ambapo ilieleza bado mkoa
huo umekuwa unakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo suala la
matukio ya ubakaji, unyanyasaji wafanyakazi katika mahoteli ya kijalii
na ajira kufanya kwa wageni,

Pia Dk. Shein katika ziara hiyo alifanya ukaguzi katika eneo jipya
lilojengwa mnara wa kurushia matangazo ya kituo cha ZBC Redio katika kituo cha Bungi ambapo aliahidiwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika baada ya miezi miwili.

Katika ziara hiyo Dk Shein, alikagua shamba la mpunga katika kijiji cha
Uzini, aliweka mawe ya msingi katika kijiji cha Unguja Ukuu, na Mwera
Kiongoni ambapo aliweka jiwe la msingi la jengo hilo pamoja na jengo
la nyumba ya daktari.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.