Habari za Punde


Raza aupiga tafu ujenzi, maandalizi ya Ijtimai

Na Madina Issa
WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kuitumia faida wanayoipata katika biashara zao kwa kuwasaidia wananchi katika matatizo yao ikiwa ni hatua ya kuiunga mkono serikali kwenye mapambano dhidi ya kuwaondolea umaskini wananchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya kupakia na kupakua mizigo (ZAT), katika kiwanja cha Ndege cha kimataifa cha Abeid Amani Karume, Mohammed Raza kwenye hafla ya kukabidhi fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya wilaya Magharibi pamoja na fedha kwa ajili ya maandalizi ya Ijitimai.

Raza alisema endapo wafanyabiashara watajenga utamaduni wa kuchangia fedha zinazotokana na faida ya biashara yao na kuzitumia kwa maendeleo ya jamii zitasaidia kupunguza matatizo mbali mbali yanayowakabili wananchi.

Alisema hivi sasa wafanyabiashara wengi wamekuwa hawazitumii faida zinazotokana na faida za biashara zao kwa kuwasaidia wananchi ambao ndio msingi wa utajiri walionao ambao umetokana na wananchi kuwa wanunuzi na watumiaji wa bidhaa zao.

Raza ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, alisema kutokana na dharau hizo zinazofanywa na wafanyabiashara wananchi wengi wamekosa imani na wafanyabiashara jambo linaloweza kuleta mizozo iliyokua sio ya lazima.

Aidha alifahamisha kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kuwasaidia wananchi waliokuwa hawana uwezo wa kufanya jambo wakiwa peke yao.

Hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara wengine kupunguza bei za bidhaa wanazozileta ili kuweza kuwafanyia urahisi wa maisha wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao wana kipato cha chini.

Raza aliahidi kushirikiana na ofisi ya wilaya ya Magharibi kwa lengo la kuiboresha wilaya hiyo, hivyo ameiomba ofisi hiyo kuwafahamisha wananchi sheria kwa lengo la kujua haki na wajibu wao sambamba na kuelewa sheria hizo ili wasiingie katika kundi la wanaozivunja sheria za Nchi kwa makusudi.

Akitoa shukrani Mkuu wa Wilaya ya magharibi, Hassan Mussa Takrima alisema kuwa amefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Mwenyekiti wa Kampuni ya ZAT kwa kuwapokea na kuwasikiliza maombi yao na hatimae kutoa mchango mchango huo ambao utaweza kuwasaidia katika shughuli zao mbali mbali.

Hivyo aliahidi kuwa fedha walizopatiwa watazitumia kwa lengo lililokusudiwa na sio kwa lengo jengine.

Jumla ya shilingi milioni 1,900,000 zimetolewa na kampuni ya (ZAT), ambapo shilingi milioni 1,400,000 kusaidia ujenzi wa Ofisi ya wilaya ya Magharibi na shilingi 500,000 matayarisho ya Jitimai ya kimataifa inayotarajiwa kufanyika hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.