Habari za Punde


RC amvaa Mkurugenzi wa jiji Arusha

Joseph Ngilisho, ARUSHA
MKUU wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amemjia juu Mkurugenzi wa Manispaa ya jiji la Arusha, Estomih Chang’ah kwa kuingia mkataba uliokinyume na utaratibu wa kutengeneza taa za barabarani kwa kampuni ya Skytel.

Mulongo alisema kampuni hiyo iliyoramba mkataba wa utengenezaji wa taa hizo, ipo kinyume cha sheria kwani katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano ilipewaa zabuni ya kutengeneza taa za barabarani, ambapo haziwaki na kulifanya jiji la Arusha kuwa giza.

Kutokana na hali hiyo, Mulongo ameuagiza uongozi wa Manispaa chini ya Mkurugenzi wake Estomiah Chang’ah, kutafuta ufumbuzi wa haraka kushughulikia tatizo hilo.

“Naomba niuagize uongozi wa jiji la Arusha chini ya Mkurugenzi wake, kuhakikisha wanapata ufumbuzi wa haraka kwanini taa haziwaki, tangu nimekuja Arusha nashangaa kwanini mji unakuwa giza wakati taa zinaonekana, kwa hili nilazima tutawajibishana’’, alisema Mulongo.

Mulongo alifafanua kuwa ukosefu wa taa kwenye mitaa mbalimbali ya jiji Arusha ni kero na aibu kubwa kwa jiji linalosifika kupokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Jiji hili linapaswa kuwa kioo, kwa kuwa limekuwa likipokea wageni wa kila aina, hivyo, kukosa taa ni aibu ambayo watu wa Manispaa mnapaswa kulishughulikia mara moja”, alisema Mulongo.

Aidha alisema kuwa Manispaa hainufaiki na kitu chochote na kampuni iliyopewa kandarasi ya kuzifanyia matengenezo taa hizo, huku wakiitizama kampuni hiyo bila ya kuichukulia hatua za kumyang’anya kazi mkandarasi huyo…‘hapa kuna kitu’.

Kampuni ya Skytel ilipewa tenda mwaka 2007 na Manispaa ya Arusha kuzifanyia marekebisho taa zote za barabarani pamoja na kusimamisha nguzo mpya kwa baadhi ya barabara zilizokuwa hazina taa na kwamba ifikapo Juni 2012 mkataba wake unamalizika.

Hata hivyo, alipotafutwa Mkurugenzi wa Manispaa, Chang’a alikiri kuwepo wa dosari nyingi katika kutoa kandarasi kwa kampuni husika na kudai kuwa haikutolewa katika ushindani.

“Ni kweli tenda hiyo ilitolewa kimakosa na ilikuwa na dosari nyingi, lakini katika uchunguzi wangu wakati kandarasi ya taa tulikuwa hatuna uzoefu kwenye masuala ya tenda, hivyo walikubaliana tu na hatimaye kumpatia mkataba”, alisema.

Chang’a aliongeza Mkandarasi halipwi na Manispaa bali anajilipa kutokana na matangazo yanayobandikwa kwenye nguzo za taa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, manispaa imeunda tume kuuchunguza mkataba huo kabla ya kuchukua hatua zaidi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Skytel, Shoo Allbless Shoo, alisema viongozi waliopo hawajui mkataba ulivyokuwa kwani ni wazo lake la kuishawishi Manispaa wakakubaliana ndipo alipochukua mkopo benki wa bilioni tatu, kwa ajili kuweka taa kwenye barabara 37 za jiji hilo.

Shoo alikiri kuwepo kwa taa ambazo haziwaki kwa baadhi ya barabara katika jiji la Arusha na kudai kuwa changamoto hiyo inatokana na manispaa kwenda kinyume na makubaliano.

Shoo aliongeza kuwa changamoto inayomkabili ni pamoja na nguzo nyingi kugongwa na gari ambapo alidai hadi sasa nguzo zaidi ya 500 zimegongwa na baadhi ya wahusika kufikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.