Na Khamis Haji. HAKUNA shaka yoyote utalii ambao unachangia zaidi ya asilimia 27 katika uchumi wetu na kuzalisha ajira kwa wananchi zaidi ya 45, 000 ni tegemo kuu la uchumi wetu.
Serikali inaelewa sana hilo na kutokana na uelewa huo wa faida ya utalii ndio maana mwelekeo wa sasa ni utalii kwa wote, kwa maana kila mwananchi aweze kunufaika na sekta hii.
Hilo linawezekana kabisa kwa kuzingatia utalii unapoimarika hata sekta nyengine kama uvuvi, kilimo na ufugaji na biashara ndogo ndogo nazo hupata msukumo wa kipekee, wale wanaojishughulisha na kazi hizo, ambapo kwa Zanzibar ni asilimia kubwa zaidihufaidika, hata kama sio moja kwa moja.
Tokea kushamiri kwa utalii wengi tunalalamikia kupanda kwa bei za bidhaa kama samaki, nyama na hata matunda, ambaz zinauzwa kwa bei nzuri kwa ajili ya hoteli za kitalii.
Lakini pamoja na mafanikio hayo kidogo, hadi sasa tuna kilio kikubwa kwamba Zanzibar inapokea watalii wa daraja la chini ambao wamebatizwa jina la 'vishuka' kwa vile kile wanachokitumia wakiwa hapa nchini ni kidogo sana.
Hivyo tunachohitaji ni kuwa na utalii wa daraja la juu ambapo watalii wanaokuja wawe ni wale wenye mapesa na wayatumie wananchi wanufaike na hapo ndipo tutapoona faida za utalii na utakuwa ni kwa wote kweli kweli.
Juhudi tafauti zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kuimarisha utalii Zanzibar, lakini bado lengo linalokusudiwa halijatimizwa kwa kiwango chenye kuleta matumaini.
Miongoni mwa hizo ni kuitangaza Zanzibar kiutalii ambapo lengo hilo litaweza kufikiwa kwa kutumia njia za kisasa za kujitangaza, njia hizo ni pamoja na kutumia vyombo vya habari vya kimataifa, kama vile CCN, BBC, Aljazeera, DW na vyenginevyo.
Vile vile kutokana na wakati tulionao hatuwezi kuepuka kutumia teknoplojia ya kisasa ya mawasiliano na habari, ambapo mitandao ya kompyuta ina nafasi ya kipekee kuwasilisha taarifa na ujumbe tunaokusudia kuusambaza.
Hadi sasa tunaambiwa kuwa fedha zinazotengwa kwa Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwa ajili ya mikakati ya kuutangaza utalii katika kiwango hicho cha kimataifa ni kidogo sana na kisichikidhi kabisa haja hiyo.
Kwa mfano vyombo vya habari vya kimataifa tulivyotangfulia kuvitaja bila shaka yoyote kuweza kupenyeza tangazo lako kunahitajika fedha nyingi sana, lakini kwa kuwa tumeshaamua kuubeba utalii, ili nasi utubebe kiuchumi, lazima tukubali gharama ili tufikie lengo letu.
Lakini mbali na vyombo hivyo, pia kuna haja tukawa na mikakati mingine maalum ya kushawishi makampuni ya Asia kutoka nchi kama India, Japan, China na nyenginezo kuitumia Zanzibar kwa kuleta wageni kwa ajili ya shughuli za utalii.
Ni kweli Zanzibar imekuwa ikishiriki katika matamasha na maonesho tafauti nje ya nchi kwa ajili ya kutangaza uzuri wa Zanzibar. Lakini hadi sasa hatujaona juhudi kubwa za kuwatumia watu mashuhuri duniani, kama wanamichezo na wasanii waliosifika Duniani
Tutumie fedha kuwaleta watu wenye majina makubwa Ulimwenguni kuandaa matangazo na kutangazwa katika vyombo vya habari vya kimataifa. Tuwalete nyota kama akina Zinadine Zudane, Thiery Henry, Drogba na masdtaa wengineo tuwapige picha wakatutangaze.
Kama tumefanikiwa kushiriki katika matamasha na maonesho tafauti ya kimataifa katika nchi za Ulaya na kwengineko, kwanini tusiongeze mtaji wa fedha tuweze kuandaa ziara ya nyota kama hao au kujitangaza kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.
Nashawishika kusema kwamba hilo linawezekana kwasababu ni hivi karibuni tu, kule Tanzania Bara, mwaka jana walitangaza mikakati kama hiyo kuinua utalii, ambapo miongoni mwa wanasii mashuhuri wa Bollywood watakuja Bongp kwa nia ya kutangaza utalii, kwanini sisi Zanzibar tusiweze.
Kwa Zanzibar ambayo imekuwa na mikakati ya siku nyingi kuinua utalii ni wakati sasa tusikie mikakati mipya na yenye manufaa zaidi kuinua sekta ya utalii.
Nadhani wakati ni sasa tujaribu kuliangalia hili, ili tuwe na utalii wenye tija kubwa zaidi, ikiwa pia ni hatua za kufanikisha utalii kwa wote.
Khamis Haji
No comments:
Post a Comment