Na Salum Vuai, Maelezo
WAANDISHI wa habari Zanzibar, wameaswa kufanya uchunguzi wa kina kabla kuandika au kutangaza taarifa wanazopewa na vyanzo mbalimbali.
Wameelezwa kuwa, si kila jambo wanaloambiwa, kusikia au kuona, kulichukulia kuwa ndiyo habari na kukimbilia kuitoa kwa umma.
Nasaha hizo zimetolewa na mwandishi wa habari mkongwe Salim Said Salim, wakati akitoa mafunzo katika warsha inayofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, juu ya namna hya kuandika habari kwa kuzingatia maadili na haki ya kujibu.
Salim alifahamisha kuwa, mara mwandishi anapoambiwa jambo, hana budi kulifanyia utafiti wa kina kabla kuliandika au kulirusha hewani, ili kuepuka migogoro.
"Taarifa mnazopata kuhusu jambo lolote, liwe kama mbegu ya kutafuta undani badala ya kukurupuka na kuandika, kwani watu wengine wanakuwa na ajenda zao, ambazo zinaweza kukutieni kwenye matatizo", alifafanua.
Alisisitiza kuwa mwandishi anapaswa kufanya maamuzi sahihi kabla kushika kalamu na kuandika taarifa anayoikusudia ili kujiepusha na kuwavunjia watu heshima.
Aidha aliwataka kupima juu ya kile wanachokiandika, na kujiepusha na habari zinazoweza kuwakashifu watu wengine mbele ya jamii kwa kuelezea mambo yao ya ndani ambayo hayana faida yoyote kwao na jamii wanayoiandikia zaidi ya kupandikza chuki na uhasama.
Akizungumzia juu ya matukio yanayopigwa picha, Salim alieleza kukerwa kwake na jinsi wapiga picha wengi wasivyojali wala kuzingatia staha ya mtu wanayempiga picha na hivyo kuijengea jina baya tasnia ya uandishi wa habari.
Alitoa mfano kwa wapiga picha katika mchezo wa netiboli, kusubiri sketi za wachezaji ziinuke, na kuona hapo ndipo pahala pa kupata picha nzuri, akisema ni lazima wanawake wastahiwe kwani ni mama na dada katika jamii inayowazunguka.
"Tusipendelee kuandika habari za kashfa hata kama ni za kweli kwani pamoja na kuishi katika zama za uwazi na ukweli, lakini kila mtu ana haki ya kuheshimiwa faragha yake", alieleza mwanahabari huyo mkongwe.
Alisisitiza kuwa mwandishi anapaswa kufanya maamuzi sahihi kabla kushika kalamu na kuandika taarifa anayoikusudia ili kujiepusha na kuwavunjia watu heshima.
No comments:
Post a Comment