TAARIFA
YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA
MAPINDUZI, MHESHIMIWA DKT. ALI MOHAMED SHEIN,
KWA
WAANDISHI WA HABARI, WAHARIRI NA WANANCHI KUHUSU HALI YA NCHI, TAREHE 31
MEI, 2012
Assalam Aleykum
Namshukuru Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu
wote, kwa kutupa afya njema tukaweza kuzungumzia mambo yenye mustakbal mwema wa
hali ya nchi yetu kwa jumla.
Napenda kutanguliza shukurani zangu kwa
wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza na kudumisha amani hasa tokea kupatikana kwa
maridhiano ya kisiasa baina ya vyama viwili vikuu vya siasa hapa Zanzibar,
Chama cha Mapinduzi na Chama cha CUF, yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa mnamo Novemba, 2010 kwa mujibu wa
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Maridhiano hayo yalidhihirisha silka,
ustaarabu na utamaduni wa Wazanzibari kuishi pamoja kwa kuheshimiana ,
kusikilizana na kushirikiana katika mambo yao ya kiuchumi na ya kijamii na
maendeleo yetu.
Kama tunavyoelewa kwamba Zanzibar ina watu wa makabila na dini tofauti.
Wazee wetu wa asili walisema “Zanzibar ni njema atakaye na aje”. Ustaarabu huu ulianza kutumika tangu
ulipoanza kuingia Uislamu na kuendelea hadi kufika wageni kutoka Uajemi
(washirazi), Ureno na Oman walioanzisha utawala wao katika karne mbali mbali
hadi ya 18. Uislamu uliingia Zanzibar mara tu baada ya kuwepo katika nchi ya
Saudi Arabia. Kadhalika, Ukristo uliingia
Afrika Mashariki alipofika Mvumbuzi wa Kireno, Vasco da Gama mwaka 1498 na hatimae
kuja Wamishionari wa kwanza wakiongozwa na Ludwig Krapf mwaka 1844. Mfalme wa
wakati huo wa Zanzibar aliwaruhusu kujenga Kanisa la Anglikana la Church
Missionary Society (CMS) liliopo Mkunazini. Krapf baadae aliruhusiwa kujenga mishionary
Mombasa. Madhehebu mengine ya kikristo yaliingia Zanzibar katikati ya karne ya
Kumi na Tisa na kuenea sehemu za bara kutokea hapa Zanzibar, na kanisa la pili
kubwa la Minara Miwili lilijengwa katika eneo la Shangani Mjini Zanzibar.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Naelezea haya ili nikumbushe sifa ya
Zanzibar kuwa ni pahala ambapo watu wa dini mbali mbali walifika na kuweka
makazi yao na kuendeleza shughuli zao za maisha pamoja na kidini. Anayeijua Zanzibar vizuri atakumbuka kwamba
ilikuwa taabu kumtambua Muislam au Mkristo kwa sababu wafuasi wengi wa dini
hizo walikuwa na tamaduni za mavazi ya aina
moja, wakicheza na kusoma pamoja.
Baadhi ya ndugu zetu hao leo tunaishi nao pamoja.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Hii ndio hali ya dini ya Kiislamu na Ukristo
hapa Zanzibar. Kuvumiliana na kuelewana kulikuwa ni chachu ya amani kwa muda
mrefu na kulichangia kuondoa ubaguzi. Kwa mara nyingi sherehe zao zilikuwa zinahudhuriwa na watu wa
dini zote. Aidha, wafuasi wa dini hizo walikuwa wakihudhuria shughuli za jamii
kwa pamoja na kujadili mambo ya maslahi ya nchi kwa pamoja. Katika Afrika
Mashariki ukiongelea uvumilivu wa kidini mfano mzuri ni wa hapa Zanzibar. Mnamo mwaka 1953 yalifanyika mashindano ya sanaa ya uchoraji
katika eneo la Afrika Mashariki ya kuonesha uvumilivu wa kidini. Mshindi wa
mashindano haya alitokea Zanzibar ambae mchoro wake ulionesha msikiti, kanisa
na baina yake palikuwa na temple.
Mchoro huu uliashiria mfungamano wa kidini wa watu wa Zanzibar tangu enzi .
Zaidi ya maelezo hayo ya kihistoria,
Katiba ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 19(1) kimeelezea kuwa “kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa
mawazo, wa imani na wa uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa kubadilisha
dini au imani yake”, ambapo pia, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
nayo inazungumzia hayo hayo. Aidha, miongoni mwa masuala tunayokwenda nayo
vizuri sisi viongozi ni hili suala la
kuheshimu imani za dini mbali mbali hapa
Zanzibar.
Mfano ni tarehe 16 Septemba, 2011, mimi
nikiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi nilikutana na
viongozi wa dini mbali mbali waliokuwa wakijihusisha na juhudi za kuendeleza
amani nchini. Pia, nilihudhuria kutawazwa kwa Askofu Michael Henry Hafidh wa
kanisa la Aglikana tarehe 15 Aprili mwaka huu na nilipewa fursa ya kuhutubia
wafuasi na kuwaelezea msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya imani
za watu na kutobagua dini.
Kadhalika, mimi na viongozi wenzangu
tumekuwa tukikutana na kujadiliana na viongozi kadhaa wa dini ya Kiislamu. Kwa
mfano tarehe 25 Aprili, 2012 Kamati
maalum ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikutana na viongozi
wa Jumuiya ya Uamsho, Maimamu na Mashekhe kuzungumzia hali iliyotokea nchini
katika kufanya mihadhara ikiashiria kama kwamba kutatokea uvunjwaji wa amani
tuliyonayo. Kamati hiyo ilifanya kazi nzuri sana. Tutaendelea na utaratibu huu
wa kukutana na viongozi wa dini zote ili kujadiliana hali halisi katika jamii. Hivi
majuzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Mohamed
Aboud Mohamed, Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi pamoja na
IGP Said Mwema, wamefanya hivyo juzi na mikutano kama hiyo itaendelea kufanywa
kwa utaratibu wake.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Tunaelewa vyema kwamba mustakabali wa
nchi yetu umo katika mjadala mkubwa wa kisiasa. Msingi mkuu wa hayo ni
mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Kwa maridhiano ya
viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tulikubaliana kuwa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba
yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
katika kikao cha pamoja na viongozi wa dini zote Aprili 25, mwaka huu,
iliwasihi sana viongozi hao watumie busara na wafuate taratibu zilizowekwa
kuhusu marekebisho ya katiba. Walitakiwa kuwaomba wafuasi wao kuepuka matumizi
ya lugha na vitendo vinavyoashiria uvunjaji wa amani katika nchi yetu. Wote
walitakiwa kushiriki ipasavyo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba
utakapoanza.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Wakati huo huo, kabla ya kuanza mchakato wa mabadiliko ya katiba, Serikali
zetu mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, tangu mwaka 2006 tumekuwa tukifanya mazungumzo ya pamoja kuhusu
mambo ya Muungano kupitia Kamati ya
pamoja inayozungumzia mambo ya Muungano inayoongozwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuzungumzia kero za Muungano. Mimi nilipata nafasi ya kuingonoza Kamati hii
kuanzia mwaka 2008 hadi 2010. Hivi sasa Kamati hio inaongozwa na Mheshimiwa Dk.
Mohammed Gharib Bilal ili kujadili kero na mapungufu katika mambo mbali mbali
ya Muungano wetu.
Vikao mbali mbali vinaendelea
kufanyika. Pande zote mbili zimekuwa
zikiwasilisha mambo ambayo yanajichomoza na yanayoendelea kuchomoza kama kero
kwa Sekretarieti ambayo ina wajumbe sita, watatu kutoka kila upande wa
Muungano.
Sekretarieti hii ina jukumu la kuandaa
ajenda za mikutano ya ngazi za Wataalamu, Makatibu Wakuu, Mawaziri na hatimae
kikao cha juu kabisa kinachowajumuisha Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uwenyekiti wa
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Miongoni
mwa vikao vilivyofanyika ni:
1. Vikao
4 vya Sekretarieti vilivyofanyika kwa lengo ka kuratibu utekelezaji wa
yatokanayo katika kikao cha mambo ya Muungano.
2. Vikao
6 vya ngazi ya watendaji wa sekta mbali
mbali husika kujadili utekelezaji na taratibu za kisheria kwa mambo yote ambayo
yameainishwa katika kero za Muungano.
3. Vikao
4 vya ngazi ya Makatibu Wakuu kujadili maamuzi ya watendaji.
4. Vikao
vitatu vya ngazi ya Mawaziri kwa ajili ya kuandaa mapendekezo ya kikao cha juu
cha mambo ya Muungano.
5. Kikao
kimoja kati ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichoongozwa na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika Dar es Salaam
tarehe 28 Januari mwaka huu.
Wana ratiba ya kuandaa kikao chengine
hivi karibuni.
Miongoni
mwa mambo yaliyojitokeza hadi sasa na yaliyopata nafasi ya kujadiliwa ni haya
yafuatayo:
1. Utafutaji
na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
2. Ushiriki
wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
3. Uvuvi
katika Ukanda wa Bahari Kuu.
4. Ushirikiano
wa Zanzibar na Taasisi za Nje.
5. Ajira
kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
6. Uwezo
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa Ndani na Nje ya Nchi.
7. Kodi
ya Mapato.
8. Usajili
wa vyombo vya moto.
9. Ongezeko
la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO.
10.
Uharamia na utekaji nyara
wa Meli.
11.
Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.
12.
Taarifa ya utekelezaji wa masuala
ya Muungano.
Changamoto
zipo na zitafanyiwa kazi.
Nimeona
haya niyaseme ili wananchi waelewe mambo haya muhuimu yanayofanywa na Serikali
zote mbili juu ya suala hili.
Kutokana na jitihada hizi
zinazochukuliwa na Serikali zote mbili, pamoja na kuitumia vizuri fursa
tuliyopewa ya kuweza kuwasilisha maoni yetu katika marekebisho ya Katiba, matumaini
yangu ni kuwa kwa pamoja tutaweza kuondosha
kero hizi na kuandaa Katiba mpya itakayotuletea maendeleo makubwa nchi
yetu. Haya ni masuala muhimu kwa ustawi wa nchi yetu. Nawasihi wananchi
wayakabili wakiwa na subira na busara ili tuijengee mustakbali mzuri nchi yetu
katika mambo 12 niliyoyaorodhesha hapo juu mambo mengi tayari yamepatiwa
ufumbuzi na yapo baadhi ambayo yanafanyiwa kazi.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar alitangaza majina ya Tume ya
mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume hiyo inayoongozwa
na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti
Mheshimiwa Jaji Agostino Ramadhani. Naelewa
kuwa hadi sasa sio wananchi wengi wanaoijuwa sheria hiyo. Tume inafanya
utaratibu wa kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hii ili wapate kutoa maoni yao
kwa njia bora zaidi.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina
yo yote ile, wako huru kutoa maoni yao kwa njia ya amani na salama kwa Tume
hiyo itakapokuja kuanza kazi zake. Aidha, wananchi hawajawekewa vizuizi katika kutoa
maoni yao, ila tu ni kuzingatia sheria za nchi na taratibu zake. Tume nayo
imepewa uhuru wa kusikiliza maoni ya wananchi kwa kuzingatia sheria ya
Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (Toleo
la mwaka 2012).
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Ni jambo la kusikitisha sana na kutia
majonzi kuwa katika siku chache zilizopita kumezuka vitendo vya uvunjaji
sheria. Tumeshuhudia maandamano na
mikutano yenye sura ya dini lakini yenye ujumbe wa siasa, hasa kwa kuuzungumzia
Muungano wetu. Vitendo hivyo vilikuwa chachu ya machafuko yaliyojitokeza tarehe
26 Mei, 2012.
Viongozi na wafuasi wao wasiojali
sheria, ustaarabu na utamaduni wa
kihistoria wa Kizanzibari walichoma moto majengo, mali za watu wasio na
hatia na makanisa, wamevunja maduka ya
raia na kuiba mali zao na wamekuwa wakitoa matamshi ya vitisho na ubaguzi ambavyo
vimejenga khofu kwa wananchi.
Nimeshangaa sana uhusiano gani uliopo kati ya kuzungumzia muungano na
matukio hayo ambayo hatukuyatarajia kutokea. Haya ni kinyumbe na Katiba na
sheria zetu – lakini yametokea.
Mtakumbuka kwamba hivi karibuni, tarehe
21 Machi, 2012 nilikuwa na ziara kwenye mikoa mitano ya Zanzibar. Katika
mikutano yangu ya majumuisho wakati wa ziara ya wilaya zetu zote za Unguja na
Pemba, nilikuwa nikitahadharisha sana na
kueleza kwamba hatutovumilia kwa hali yoyote uvunjaji wa sheria. Nilisema katika Mkutano wangu wa mwisho wa
majumuisho, tarehe 9 Mei, 2012 baada ya ziara ya Mkoa wa Kusini Unguja, kwamba Serikali
haitomuonea muhali mtu yeyote atayethubutu kuharibu amani yetu. Hilo lilikuwa
ni onyo kwa kila mmoja wetu. Maana ishara tuliziona kupitia mihadhara yao na
Serikali ilichukua jitihada za kukabiliana nayo kwa kuzungumza nao.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Kutokana na matokeo hayo ya siku ya
tarehe 26 Mei, 2012, Jeshi letu la
Polisi lilichukua hatua za haraka kuidhibiti hali iliyojitokeza, wengi wenu
mliiona hali ilivyokuwa. Kadhalika,
Jeshi la Polisi walihakikisha kwamba wale wote waliohusika na vitendo hivyo vya
uharibifu na aibu kwa nchi yetu na jamii ya Kizanzibari wanafikishwa kwenye
vyombo vya sheria kwa kuzingatia sheria za nchi ziliopo hapa Zanzibar. Hakuna atakaeonewa wala kudhulumiwa na kila
mmoja atahukumiwa kwa kesi inayomuhusu na kwa mujibu wa sheria ziliopo.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Nachukua fursa hii kwanza kutoa pole
kwa ndugu zetu waliotiwa hasara ya mali zao. Pia, nawapa pole wananchi wote kwa
usumbufu wote uliojitokeza. Naelewa vyema kuwa wananchi wamepata hasara kubwa
ya kiuchumi kwa baadhi ya wananchi kuvunjiwa maduka yao, kuibiwa na pia
kukatizwa shughuli zao za kujitafutia riziki na maisha yao. Kwa bahati mbaya,
wako pia waliofikwa na matatizo ambayo hawakuyategemea wala kuyazowea wakati
polisi wakifanya kazi zao. Serikali
inaendelea kufanya tathmini ya hasara zilizotokea na pia inazingatia hatua za
kuchukua katika hasara hizo.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Baada ya hayo, napenda kuwaarifu
wananchi wote kwamba hatua za Serikali zetu mbili kuidhibiti hali ya usalama
zitaendelea, ili amani idumu na usalama wa wananchi, mali na maisha yao uwepo wakati wote. Kwa wale
wanao vunja sheria na viongozi wao tunawataka watambue kwamba Serikali hatovumilia
vitendo walivyovifanya. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu ye yote
atakayevunja sheria na yule mwenye lengo la kuiharibu amani na utulivu wetu.
Amani ambayo haikuja kwa bahati tu, bali imehangaikiwa kwa muda mrefu,
tutailinda hali hiyo kwa nguvu zetu zote.
Kadhalika, nataka wananchi waelewe
kwamba Serikali haitoingilia shughuli za kweli za kidini au vitendo halali vya
viongozi na wafuasi wa dini yoyote. Kwa wale wenye maoni juu ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tungewasihi
sana wasubiri utaratibu wa kutoa maoni kama Tume ya Mabadiliko ya Katiba
itavyotangaza. Wafahamu fika kwamba kwenda
kinyume na sheria iliopo ni kosa la jinai, kwa sababu ni sheria
iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kama ilivyozoeleka, shughuli za ibada
za pamoja zifanywe katika nyumba za ibada na ikiwepo haja ya kufanya nje, iwe
kwa kufuata taratibu zilizowekwa nchini haya yanajulikana na lazima yazingatiwe.
Kwa kutunza amani na utulivu, Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imetangaza hatua kadhaa, miongoni mwa hatua
hizo ni kupiga marufuku mikusanyiko ya aina mbali mbali, maandamano na
mihadhara ambayo haijapata kibali cha Serikali hili ni lazima kila mmoja wetu
azingatie, huu sio wakati wa kubeza, na kila mtu azingatie sheria. Mikutano ya
halali ya kijamii haitaingiliwa hata siku moja na pale pa kutaka ulinzi Jeshi
la Polisi litafanya hivyo. Napenda kuwatoa hofu waumini wa dini zote
kwamba shughuli za ibada hazitoingiliwa na waumini wa dini hizo wataendelea na ibada
zao kama Katiba ya Zanzibar ya 1984 na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya 1977.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Pamoja na kudhibiti amani na
kuwahakikishia usalama wananchi, juhudi
za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea
pia kudumisha sifa ya kuendeleza amani ambayo kama itapungua seuze kuondoka
kwake kutaathiri utalii ambao ni tegemeo la uchumi wetu, ni jukumu letu
kuendeleza amani na ni jukumu letu
kuwalinda wageni wetu wanaokuja kututembelea.
Kuathirika kwa utalii kutawaathiri wananchi ambao kwa kiasi ya asilimia 60 za
shughuli zao zinahusiana na sekta hiyo. Wananchi hawa ni pamoja na wakulima, wavuvi na
wafanyabiashara mbali mbali zikiwemo zile
biashara za usafiri, mikahawa na hoteli. Nimeshabainisha katika mikutano mbali
mbali kuwa sekta ya Utalii inachangia
zaidi ya asilimia 80 ya fedha za kigeni tunazoingiza nchini. Tutambue kwamba hao
wanaofanya fujo ni waharibifu wa uchumi
wetu na kamwe tusiwape nafasi katika kutimiza malengo yao.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Natoa wito kwa wananchi wote wanaopenda
amani washirikiane na Serikali yao katika kudumisha amani hiyo. Wafuasi wa dini wazitumie nyumba za ibada kwa
kufanyia ibada na kutumia wakati wa ibada zao kuamrishana mema na kukatazana
mabaya. Wazazi wachunguze myenendo ya
watoto wao na wachukue dhamana yao ya kuwalea watoto hao katika maadili mema na
kila wakati wawatahadharishe juu ya kutokushiriki katika vitendo vya uvunjaji
wa sheria. Viongozi wa jamii nao wanajukumu la kuisaidia jamii
katika kufikia misingi ya kuwa raia wema na kutojiingiza kwenye vitendo vya uvunjaji
wa sheria. Ni jukumu letu sote kuilinda na kuitekeleza misingi ya haki za
binadamu na utawala bora, hili ni jukumu la kila mmoja wetu si Serikali tu.
Ni jukumu letu sote tuidumishe misingi ya ustarabu na mila zetu, kwa
hakika si vizuri kutaka kuiga kila tuliloliona katika nchi za nje. Lakini tuyaige
yaliyo mazuri yenye kujenga uadilifu na utamaduni bora, lakini katu mabaya
tusiyaige hayana maana kwetu. Aidha, wakati Serikali inaendelea kudhibiti
usalama, nawataka viongozi hasa viongozi wa jamii wawache kutoa lawama
zisizokuwa na msingi katika hali hii. Viongozi wa dini, siasa na jamii wawe
waangalifu wa matamshi yao, kwani Zanzibar na Tanzania ni yetu sote. Linapoharibika ni letu sote na linapotengamaa
ni letu sote.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Kwa kumalizia, natoa tena pole kwa wananchi
wote wa Zanzibar na ndugu zetu wa kikristo walioathirika na vitendo viovu
vilivyotokea hivi karibuni. Pia, nawapa pole wale wote walioathirika kwa njia mbali
mbali.
Nawasihi sana wananchi tuendelee kuvumiliana,
tuheshimiane na tushirikiane katika shughuli hasa zile za kuiletea maendeleo
nchi yetu na kila mmoja wetu kupata manufaa.
Tuendele kupendana na tudumishe umoja wetu kama ulivyo utamaduni na
silka zetu. Jeshi letu la Polisi
litaendelea na kutimiza wajibu wao kwa faida yetu na amani ya nchi yetu. Nataka niwahakikishie wananchi wote kwamba
tutaendelea kuyalinda Mapinduzi, tutayaendeleza kwa ajili ya maslahi ya kila
mmoja wetu na Wazanzibari wote. Nataka
niwahakikishie wananchi wote kuwa Mapinduzi yetu tutayalinda kwa maslahi ya
wananchi wetu wote.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment