JUMUIYA ya Uamsho na mihadhara ya kiislamu
Zanzibar imekanusha kuhusika na vurugu zilizotokea Zanzibar, ikiwemo uchomaji
wa makanisa na uharibifu wa mali za wananchi zilizotokea Zanzibar mwishoni mwa
wiki iliyopita na mwanzoni mwa wiki hii.
Naibu Amiri na msemaji mkuu wa Jumuiya hiyo,
Sheikh Farid Had Ahmed amesema kuwa, Jumuiya yake haikupendelea vuguru hizo
ambazo zimeiondolea Zanzibar sifa kubwa ya amani na utulivu iliyokuwa nayo.
Pamoja na hayo, Sheikh Farid alifahamisha kuwa,
Jumuiya ya Uamsho itaendelea na kazi zake za mihadhara kama ilivyojiwekea na
kutarajia kufanya mhadhara mkubwa katika viwanja vya Lumumba Juni 3 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo
mbali mbali huko msikiti wa Mbuyuni wilaya ya Mjini Unguja, Sheikh Farid
alisema kwamba vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani hasa vya uchomaji moto wa
makanisa ni jambo la kulaaniwa kwa nguvu zote.
Alisema kwamba, Jumuiya ya Uamsho inafuatilia kwa
kina zaidi suala hilo na hadi hivi sasa imeshapata majina ya watu wanaowatuhumu
kuhusika na suala hilo, na endapo wakiwabaini kuhusika baada ya uchunguzi huo
kukamilika, watawafikisha katika vyombo vya sheria ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yao.
Alifahamisha kuwa, dini ya Kiisilamu haimbagui,
kumuonea wala kumuonea asiekuwa Muislamu, na kila siku inahimiza mshikamano na
maelewano kwa watu wa dini nyengine, kama alivyokuwa akifanya Mtume Muhammad
(S.A.W).
Katika kikao hicho Sheikh Farid, aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu pamoja
na wananchi kwa ujumla kudumisha amani na utulivu kama yalivyozungumzwa katika
kitabu kitukufu cha Qur'ani na hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W).
Aidha amelitaka Jeshi la Polisi kufuata taratibu
za kisheria, ili kuondosha machafuko katika nchi ambayo mengi yao yanadaiwa
kuwa Jeshi la Polisi linakuwa ni chanzo.
"Sisi
hatukatai kushitakiwa ikiwa tutaonekana
tuna makosa ikiwa tumekiuka sheria na Katiba ya nchi, ikiwa Jeshi la Polisi kwa
upande wao watafuata taratibu za kisheria hasa za ukamataji", alisema.
Hata hivyo, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kufuta mihadhara yote ya kidini hapa nchini hadi kutolewa kwa taarifa
zake, lakini Sheikh Farid alisema kuwa Jumuiya ya Uamsho itaendelea na kazi
zake kama ilivyojipangia.
Pamoja na mhadhara huo wa Juni 3, usiku wa
kuamikia leo katika Msikiti Afraa Kidongochekundu wilaya ya Mjini Unguja,
kulitarajiwa kufanyike Itikafu ya kuiombea amani nchi pamoja na kuwaombe dua
watoto walio chini ya umri wa miaka 18 waliofikishwa mahakamani kwa kuhusishwa
na machafuko hayo.
Pamoja na Itikafu hiyo, Sheikh Farid ameiomba
mahakama iwapunguzie masharti ya dhamana watoto hao, kutokana na msharti
yaliopo hivi sasa ni makubwa mno kwao kuyatekeleza pamoja na kuzitia mashaka
familia zao.
Ni vyema ikatumika busara kubwa kutafuta ufumbuzi wa mahitaji ya Wazanzibari! Nguvu za Kidola hazina faida katika sehemu inayohitaji hekima na busara kubwa. Kwa hili, linahitaji busara kubwa kutafuta waliohusika na vurugu na uchomaji wa Makanisa, kabla ya kuwashutumu UAMSHO kuhusika na kadhia hii! La pili, suala la mahitaji ya UAMSHO, yatizamwe kisheria na kielimu zaidi na ndipo itafutwe njia ya busara kutatua mahitaji husika!
ReplyDelete