Habari za Punde

Wakulima kurejeshewa fedha zao


WAKULIMA waliokosa huduma ya kulimiwa katika mashamba yao katika msimu wa kilimo uliopita, serikali itawarejeshea fedha zao.

Waziri wa Kilimo na Maliasili Suleiman Othman Nyanga, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Wanawake, Kazija Khamis Kona, aliyetaka kujua kama serikali ina mpango wa kuwarejeshea fedha zao wakulima ambao mashamba yao yameshindwa kulimiwa kuliko sababishwa na uhaba wa matrekta katika msimu uliopita.


Akijibu hilo Waziri huyo alisema ni kweli fedha hizo zilikusanywa na zipo chini ya Wizara hiyo lakini bado kama kuna wakulima watahitaji kupatiwa fedha hizo itakuwa tayari kuwapatia.

Alisema lengo la serikali kubaki na fedha hizo ni kuona pale msimu ujao wa kilimo utapoanza wakulima hao wapewe huduma hiyo kwa kuwapa kipau mbele kwa vile tayari walishalipa na kuikosa huduma hiyo.

Akijibu suala la msingi la Mwakilishi huyo aliyetaka kujua juu ya kama ina mpango wa kuongeza matrekta, alisema ni kweli huduma ya ulimaji katika mashamba ya wakulima ilichelewa kuwafikia kutokana na uchache wa vifaa hivyo.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo Wizara hivi sasa inakusudia kununua matrekta 20 za zana za kupandia mpunga 30 ikiwa ni hatua ya kuongezeka ufanisi  katika msimu ujao wa kilimo.

Alisema pamoja na kazi hiyo pia Wizara hiyo katika msimu ujao wa kilimo tayari imeshanunua mashine za  kuvunia mpunga 14 kutoka nchini China  na zitawasili kuanzia Mwezi Julai na zitaweza kutoa huduma za kuvuna mpunga katika msimu huu wa kilimo.

Hata hivyo Waziri huyo aliwataka wakulia kuona wanabadilika kwa kupanda mbegu za muda wa kati na kati na muda mfupi badala ya kuendelea kutumia za muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.