Na Mohammed Mhina, Zanzibar
Wakati Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa kwenye mchakato wa kutafuta fedha za  kununua meli mpya, Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), imesema iko tayari kuikopesha SMZ fedha za kununulia Meli hiyo.
Afisa Mtendaji  Mkuu wa Benki hiyo Bw. Yohane  Kaduma, amesema benki yake iko tayari  kuipitia SMZ mkopo wa kununulia Meli hiyo endapo watakubaliana na  kushirikishwa kwenye mchakato huo.
Bw. Kaduma  alikuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Zannzibar mara baada ya kukabidhi msaada wa shilingi milioni 5, kwa Makamu wa pili wa Rais wa  Zanzibat Balozi Seif Ali Iddi ili kusaiidia ghala za matibabu kwa  majeruhi na ubani kwa wafiwa wa ajali ya Meli ya Skagit.
Bw. Kaduma  amesema kuwa endapo Benk yake itaombwa kutoa mkopo huo inaweza kufanya  hivyo ili mradi tu kukaa meza moja na Serikali na kukubaliana aina ya  mkopo pamoja na mambo mengine.
Awali akipokea  msaada huo, Makam wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, amesema kuwa  pamoja na kusimamishwa kwa baadhi ya meli za watu binafsi kuchukua  abiria, SMZ pia imeagiza meli zake kufanyiwa uchunguzi kama zinafaa  kuchukua abiria.
Balozi Seif  amesema kuwa ameziagiza Mamlaka ya usafiri majini Zanzibar na Sumatra,  kuzifanyia uchunguzi meli hizo za SMZ ikiwemo MV Maendeleo ambayo  imerejea siku za karibuni ikitokea Mombasa nchini Kenya ambako ilikuwa  katika matengenezo makubwa.
Amesema Serikali haiwezi kukaa kimya huku ikiona kuwa wananchi wake wanapatwa na majanga ya mara kwa mara kutokana na kusafiri kwa meli zisizo na uhakika.
Katika hatua nyingine idadi ya maiti za MV Skagit, imeongezaka hadi kufikia 128 baada ya maiti nyinine mbili kupatikana leo karibu na Kisiwa cha Chumbe nje kidogo ya mji wa Zanzibar na nyingine sita zikipatikana mkoani Tanga.
Tofauti na  taarifa za awali kuwa maiti tano zilipatikana Bagamoyo mkoani Pwani,  ifahamike kuwa maiti hizo zilipatikana katika fukwe za bahari wilayani  Pangani na nyingine mjini Tanga.
Kwa mujibu wa  Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Tanga ACP Costantine Masawe, maiti  nne ikiwemo ya mwanamke mmoja zilipatikana huko Pangani na nyingine  mbili ikiwemo ya mwanamke mmoja zikapatikana kwenye fukwe za bahari  mjini Tanga.
Kamanda Masawe  amesema kuwa maiti zote zilichukuliwa vipimo kwa ajili ya uchunguzi wa  Vinasaba (DNA) pamoja na kupigwa picha kabla ya kuzikwa.
Hata hivyo  Kamanda huyo wa Polisi amesema kuwa maiti moja kati ya hizo,  ilitambuliwa kuwa ni ya Mohammed Saidi Salum  mkazi wa Ziwani Chakechake mkoa wa Kusini Pemba ambaye alitambuliwa baada ya simu aliyopatikana  nayo kufanyiwa uchunguzi.
Hadi sasa maiti  ambazo hazijapatikana ni 16 kutokana na kupatikana kwa watu 146 wakiwa  hai ikilinganishwa na idadi ya watu 290 waliokuwemo ndani ya meli hiyo  ya Skagit siku ya tukio.


No comments:
Post a Comment