Na Ameir Khalid
KAMPUNI ya simu Zantel, imeamua kudhamini tamasha la tuzo za wanamuziki bora wa Zanzibar kwa shilingi milioni 32.
Tamasha la kuwatunuku wanamuziki hao limepangwa kufanyika kesho Julai 6, katika ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani kuanzia saa moja usiku, ambapo Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Habari Maelezo jana, Meneja Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo Mussa Mohammed Mussa Baucha, amesema udhamini huo unalenga kusaidia jitihada za wasanii wa muziki Zanzibar kujituma zaidi na kutengeneza kazi zenye ubora.
Baucha ameeleza matumaini yake kuwa, tuzo zitakazotolewa kwa wanamuziki watakaoshinda, zitawaongezea hamasa na kuhakikisha wanatumia zaidi maarifa, ili kuwafanya wapenzi wa muziki wazinunue kazi zao na hivyo kuwaletea tija na kuondokana na umasikini.
Aidha amesema udhamini huo, ni miongoni mwa mikakati ya kampuni yake katika kuihudumia jamii ambayo ndio wateja wake wanaoingiza faida na kuikuza biashara yake ya mawasiliano.
Ameyataja baadhi ya maeneo ambayo tayari au wanakusudia kudhamini shughuli zao, kuwa ni pamoja shindano la kusaka vipaji vya wanamuziki Tanzania 'Bongo Star Search'.
Naye Meneja wa Kitengo cha burudani wa kampuni ya Zanzibar Media inayoandaa tuzo hizo Said Khamis, amesema tuzo hizo zitahusisha wanamuziki wa maeneo mbalimbali, kama vile taarab asilia, taarab ya kisasa na muziki wa kizazi kipya.
Aidha, amefahamsha kuwa, kampuni yake imeamua kutoa tuzo za heshima kwa wanamuziki wakongwe ambao wamestaafu au kufariki, lakini walitoa mchango mkubwa katika tasnia ya muziki hapa nchini.
Alieleza kuwa wasanii watakaoibuka washindi, watanyakua tuzo maalumu pamoja na fedha taslim ambazo hata hivyo, hakuweza kuzitaja hadharani kwa maelezo kuwa hivyo ndivyo walivyokubaliana na washiriki.
Hili ni tamasha la saba tangu kuanzishwa kwake, ambapo washindi watapatkana kutkana na ujumbe wa simu unaotmwa na wapernzi wa muziki baada ya kupitishwa kwa kazi za wasanii wanaowania tuzo hizo.
No comments:
Post a Comment