Habari za Punde

Jamhuri yapumua. Hatimaye yapata mkopo kulipia faini CAF

Na Mwandishi Wetu
HATIMAYE timu ya soka ya Jamhuri imepata ahueni baada ya kwa kukopeshwa dola elfu nne ili ilipe faini iliyopigwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Itakumbukuwa kuwa, Jamhuri ilipigwa faini na CAF baada ya kuoneshwa kadi nne za njano katika mchezo mmoja mwanzoni mwa mwezi wa Machi, ilipopambana na Hwangwe FC katika Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa kanuni za CAF, kitendo cha kuoneshwa zaidi ya kadi tatu katika mechi moja ya mashindano rasmi, ni utovu wa nidhamu unaopaswa kulipiwa faini kubwa ili kuwazindua wachezaji, juu ya umuhimu wa wito wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), wafahamu kuwa soka ni mchezo.

Katibu wa Jamhuri Ahmed Omar, ameliambia gazeti hili jana kuwa, Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kimeikopesha timu yake dola 2,500, na msamaria aliyekataa kutajwa jina ametoa mkopo wa dola 1,500, huku viongozi na wanachama wa timu wakichangishana dola 1,000.

Amesema kuwa, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, na kwa kuwa Jamhuri haina njia za kujiingizia mapato, deni hilo linapaswa kulipwa kutokana na fedha itakazopata kwa ajili ya kujiandaa na ligi kuu kutoka kwa wadhamini kampuni ya TBL.

Omar amesema tayari wamezituma fedha hizo makao makuu ya CAF jijini Cairo, kupitia benki ya Barclays tangu Ijumaa iliyopita.

Aliishukuru ZFA chini ya Rais wake Amani Makungu, pamoja na wadau wengine walioisaidia timu yake kuondokana na deni hilo kwa CAF ambalo ilipewa hadi Julai 30, kulipa, vyenginevyo lingepanda mara mbili.

Aidha, amewaomba wadau wengine, wanachama na wapenzi wa Jamhuri, wajitolee kuichangia kwa kadiri ya uwezo wao, ili iweze kulipa deni hilo ndani ya mwaka huu.

“Ni jambo la kushukuru kuwa wenzetu ZFA, na wasamaria wengine wamekubali kutukopesha fedha hizi, lakini sisi ndio wenye jukumu la kulipa faini hiyo, tunawaomba wapenzi na wanachama wetu pamoja na wadau wengine, watusaidie katika hili”, alihitimisha Katibu huyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.