HOTUBA YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI ZANZIBAR KATIKA
UFUNGUZI WA JENGO JIPYA LA AFISI YA MAISARA - TAREHE 13 SEPTEMBA 2012

Dk.
Ali Mohd Shein,
Mheshimiwa
Makamu wa Pili wa Rais,
Balozi
Seif Ali Iddi,
Mheshimiwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Utumishi
wa Umma na Utawala
Bora
Waheshimiwa
Mawaziri,
Viongozi
Mbali Mbali wa Serikali,
Wageni
waalikwa ,
Mabibi
na Mabwana.
ASSALAM ALAYKUM.
Kwanza
kabisa, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutupa afya njema na
kutuwezesha kufika hapa kwa mara nyengine tena kushiriki katika hafla hii ya
ufunguzi wa jengo jengine jipya la Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali Zanzibar. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa ujasiri na uwezo wa kusimamia ujenzi wa jengo letu hili
hadi kukamilika kwake.
Pili napenda
kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohd Shein, kwa kukubali mualiko wetu wa kuwa
mgeni rasmi katika shughuli hii ya ufunguzi wa jengo hili jipya la Afisi yetu, Aidha
kwa wingi wa heshima natoa shukrani zangu kwako binafsi kwa juhudi zako
unazochukua kwa kuiunga mkono Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali katika
kutekeleza majukumu yake ya kila siku kama ulivyowaahidi Wananchi wa Zanzibar
katika Mikutano na hotuba zako mbali mbali.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunafahamu
kuwa unakabiliwa na shughuli nyingi za kitaifa lakini kutokana na umuhimu na uzito wa jambo
hili umeamua kuugawa muda wako adhimu na kuja kuungana nasi katika ufunguzi wa jengo la
Ofisi yetu, ushiriki wako ni kielelezo tosha cha kuthamini mchango wa Afisi
yetu katika maendeleo ya Taifa letu.
Aidha kwa
dhati kabisa nampongeza waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, kutokana na mchango wake mkubwa na ukaribu
katika kuhakikisha kwamba Ofisi yetu inapiga hatua za kimaendeleo siku hadi
siku.
Pia nachukua
nafasi hii, kuwashukuru viongozi mbali mbali wa Serikali pamoja na waalikwa wote
kwa ujumla, kwa kuitikia wito wetu na kuweza kufika katika sherehe yetu bila
kukosa. Nasema ahsanteni na karibuni sana.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Afisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imemaliza utekelezaji wa Mpango
Mkakati wake wa miaka
mitatu ulioanza mwaka
2007 hadi 2011. Utayarishaji wa mpango mkakati huo
ulikuwa na lengo la kuweka mfumo mzuri wa kazi na kupata dira ya kutekeleza
majukumu yetu kiufanisi kwa
maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
Mpango mkakati huo ulikuwa na malengo yafuatayo:-
· Kuimarisha mazingira mazuri ya kazi
pamoja na wafanyakazi
· Kutayarisha mwongozo wa kazi za
ukaguzi (Regularity Audit manual ) na
· Kujenga Afisi za kisasa Unguja na
Pemba.
Jambo la
kujivunia ni kwamba Ofisi yetu imekamilisha na kufanikiwa kutekeleza mpango huo kwa
kiwango cha hali ya juu na kupatikana kwa ufanisi mkubwa katika kutekeleza
majukumu yake ya kikatiba.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Ofisi yetu baada ya kukamilisha utekelezaji wa
Mpango Mkakati uliyopita wa mwaka 2007-2011, tumeandaa Mpango Mkakati mwengine
wa muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2011 hadi 2014 ambao kwa sasa ndio tunaoufanyia kazi. Mpango huu ni
muendelezo wa hatua zilizofikiwa katika kuimarisha shughuli za ukaguzi wa
mahesabu ili uende sambamba na mabadiliko ya ukaguzi na teknolojia duniani kwa
kufuata viwango vya ukaguzi vilivyopo kitaifa na kimataifa.
Afisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kipindi cha miaka mitano imefanikiwa
kwa ufanisi mkubwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kama yalivyoainishwa
katika kifungu 112 (3 ) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na majukumu
mengine yaliyoainishwa katika sheria ya fedha namba 12 ya 2005 na sheria ya
namba 11 ya mwaka 2003 ya uanzishwaji Afisi
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na sheria nyenginezo.
Aidha Afisi kwa kiasi kikubwa imeweza
kutekeleza malengo iliyojipangia katika mpango mkakati wake, ikijumuisha
kuongeza uwezo wa kitaaluma kwa wafanyakazi, kuwepo kwa vitendea kazi vya
kisasa vinavyokwenda sambamba na kasi ya maendeleo na mabadiliko ya Sayansi na
Teknolojia duniani.
Aidha
wafanyakazi wamepata nafasi ya kufanya kazi
katika mazingira mazuri, jambo ambalo limeongeza kasi na ari za
kufanyakazi kwa ufanisi mkubwa kabisa.
Vile vile Afisi imeweza kutayarisha
stahiki na maslahi ya wafanyakazi kulingana na utaratibu uliopangwa ( scheme of
service ) kwa kuzingatia umuhimu wa shughuli
za ukaguzi pamoja na taaluma za wafanyakazi , ambapo utekelezaji wake tunategemea
utakubaliwa na kuanza muda mfupi ujao, kwani tunaamini Serikali yetu ya
Mapinduzi ya Zanzibar, inathamini mchango mkubwa na muhimu unaotolewa na Afisi yetu katika
kuimarisha utawala bora na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma, kwa maendeleo
ya wananchi na Taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Jengo hili
ulilolifungua leo rasmi, ukarabati wake umefanya na Kampuni ya kizalendo ya “Stars Construction” iliyopo Zanzibar,
na umetugharimu jumla ya Tshs. 328,460,000/- ambapo gharama hizi zote zimetolewa na Serikali yetu
tukufu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia Mia Moja (100%).
Aidha, vifaa vya
kisasa vilivyomo ndani ya jengo hili vikiwemo Samani za Ofisi, vifaa vya mawasiliano na
usalama, vifaa kwa ajili ya mafunzo na kazi mbali mbali za ukaguzi, vimegharimu
jumla ya Tshs. 27,200,000/-. Jengo hili
litatumika na wafanyakazi wapatao 64 ambapo kila mfanyakazi amepata sehemu ya
kufanyia kazi.
Vile vile
kuna ukumbi wa mkutano utakaochukuwa idadi ya wafanyakazi 85 na chumba cha
kujiongezea taaluma na maarifa Maktaba ambayo itatumika kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Ni jambo la
faraja na la kujivunia, kwani vifaa vya mawasiliano na usalama na vya
kufundishia vimewekwa na wataalamu wetu wa ndani ya Afisi wa Kitengo cha ICT,
kwa kweli wamechukua juhudi kubwa kwa kuhakikisha kuwa jengo linakuwa la kisasa
linalokwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya
kuelekea katika mfumo mpya wa e- Government.
Aidha Afisi
ina nia ya kuanza ujenzi wa Afisi mpya kwa upande wa Pemba kuanzia mwaka wa
fedha ujao wa 2013/2014 kadri hali ya uchumi wa nchi itakaporuhusu.
Kwani mazingira ya Ofisi kwa Pemba yanahitaji kurekebishwa kwa lengo la
kuimarisha mazingira mazuri na utendaji kwa wafanyakazi.
Nitakuwa
mwizi wa fadhila nisipotoa pongezi na shukrani za dhati kwa Kampuni ya Ujenzi
ya “Stars Construction” ambae ndie
Mkandarasi wa jengo hili la Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali Zanzibar. Ni ukweli uliowazi
kuwa kampuni hii ilifanya kazi
usiku na mchana ili kuharakisha na kufanikisha ujenzi wa jengo hili katika muda
uliopangwa na kwa viwango vinavyokubalika. Ahsanteni sana kwa hili.
Mheshiwa Mgeni Rasmi,
Ufunguzi huu
wa jengo unakwenda sambamba na uzinduzi
wa maktaba ya ofisi, ambayo itatumika kwa kiasi kikubwa kuongeza maarifa ya wafanyakazi wetu pamoja
na kusaidia shughuli mbali mbali zinahusiana
na kazi za ukaguzi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Baada ya
maelezo haya, sina budi kutoa shukrani maalum kwa Serikali yetu ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kutuwezesha kifedha kwa
asilimia mia moja ( 100%) kwa kulikarabati na ununuzi wa vitendea kazi na
hatimae jengo hili limesimama imara na leo hii umelifunguwa rasmi.
Aidha, ni
mategemeo yangu kuwa, Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuiunga
mkono Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Saerikali katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku
na kuimarisha utawala bora na kupunguza umasikini nchini.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Baada ya
kutoa maelezo haya, kwa mara nyengine tena kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Afisi
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali natoa shukrani za dhati kwako
Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd
Shein kwa nia yako njema ya kuitakia mema, nchi
yetu kwa kudumisha amani
na utulivu kwa maendeleo ya wananchi wake. Aidha tunamuomba Mwenyezi Mungu akujaalie kila la kheri na
mafanikio mema katika jukumu zito la kuiongoza nchi yetu ya Zanzibar, Amin.
Naomba nichukue
nafasi hii kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, ili nae aje atoe maelezo yake na baadae akukaribishe Mgeni wetu Rasmi Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi uje utupe nasaha zako.
Ahsanteni kwa
kunisikiliza
No comments:
Post a Comment