Habari za Punde

JK aomboleza kifo cha Luteni Kanali Makwaia

Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Luteni Kanali (mst) Adam Hussein Mwandu Makwaia, aliyekuwa mpambe wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi.

Rais Kikwete alielezea majonzi na masikitiko yake kufua kifo cha Makwaia kilichotokea  Jumanne, ya Septemba 4, mwaka huu katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo mjini Dar es Salaam.

“Katika miaka yote ya utumishi wa Jeshi na utumishi wa umma, Luteni Kanali Makwaia alikuwa mwadilifu na mwaminifu kwa nchi yake, alikuwa na weledi wa kiwango cha juu katika taaluma yake ya kijeshi na alikuwa mtiifu kwa viongozi wake,” alisema Rais Kikwete.

Luteni Kanali (mst) Makwaia alijiunga na Jeshi Machi 24, mwaka 1974, na alilitumikia kwa miaka 23 na miezi tisa kabla ya kustaafu.
Alikuwa Msaidizi wa mpambe wa Rais kati ya mwaka 1978 na 1981 na kuwa mpambe wa Rais kwa miaka sita hadi 1987. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 62.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.