Na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi kufuatia ajali ya barabarani
iliyohusisha lori aina ya Isuzu lililopinduka huku likiwa limebeba abiria.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Relya kijiji cha
Bereko, wilaya ya Kondoa Mkoani wa Dodoma Septemba
15 mwaka huu mbapo watu 15 walipoteza maisha na wengine 72 kujeruhiwa.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa na ajali hii ya lori
ambayo, katika kipindi kifupi tangu itokee ajali nyingine iliyogharimu maisha
ya watu wengi katika Mkoa wa Mara, imeondoa tena uhai wa watu wetu wengine 14
wasiokuwa na hatia,” alisema Rais Kikwete.
“Mamlaka zote zinazohusika hazina budi kuunganisha
nguvu katika kukabiliana na wimbi la ajali za barabarani za mara kwa mara
zinazokatisha uhai wa watu wengi wasiokuwa na hatia ambao kimsingi ni nguvu
kazi muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu,” alisema.
Aidha Rais Kikwete alisema anawaombea kwa Mola wote
waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea katika hali zao
za kawaida na kuungana tena na familia,
ndugu na jamaa zao.
Aliwaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na
ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza vifo vya wapendwa wao.
No comments:
Post a Comment