Na Hafsa Golo
UDHAIFU wa usimamizi na utekelezaji wa sera za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umesababisha kuporomoka kwa viwanda mbalimbali ambavyo vimekuwa vikianzishwa na serikali, na hata vilivyoanzishwa na sekta binafsi.
Mjasiriamali Ahmeid Yussouf Baalawi alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko.
Alisema licha ya serikali kutoa wito kwa wananchi wenye uwezo kuanzisha viwanda nchini,ili visiwa hivi viweze kupiga hatua ya maendeleo na kuzalisha ajira kwa vijana lakini lengo hilo halitafikiwa kwa sababu ya kuyumba kwa usimamizi na utekelezaji madhubuti wa sera za serikali.
Alisema wawekezaji wengi wazalendo wanahitaji maeneo ya uzalishaji pamoja na kuimarisha maendeleo kwenye nchi yao ,ili iondokane na wimbi kubwa la vijana wanaotegemea ajira kutoka serikalini.
“Zanzibar kuna watu wana pesa na uwezo wa kujenga viwanda mbalimbali lakini uwepo wa utekelezaji dhaifu wa sera za serikali, wanahofu ya kuwekeza kwao wanaenda kujenga kwengine,”alisema.
Baalawi alisema kutokana na hali hiyo bado suala la viwanda ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba litaendelea kuwa ndoto iwapo serikali haitowakemea baadhi ya viongozi ambao wanazifumbia macho sera na mipango iliyopo.
Sambamba na hayo alisema mazingira yaliopo nchini yanapelekea pia bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kuwa bei nafuu kuliko bidhaa zinazozalishwa ndani ya visiwa hivi.
Akifafanua alisema kuwa waingizaji bidhaa kutoka nje ya nchi wamekuwa na nafasi ya kulipa ushuru mdogo kwa kuficha kuorodhesha idadi halisi ya mali inayoingizwa na thamani yake, wakati mzalishaji wa ndani kupitia ZIPA na taasisi nyengine hufatiliwa katika taratibu zote na kwa kila ambacho kinafanyika.
Pia alisema mzalishaji wa ndani analazimika kuweka kodi ya ongezeko la thamani (VAT)katika bidhaa zake wakati waingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi wengi wao hawamo katika mfumo huo wa VAT na wale waliokuwemo wanaficha kuorodhesha thamani halisi ya mali zao.
Kwa upande wake Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko, Nassour Ahmeid Mazrui alikanusha dhana hizo,akisema viwanda vinakufa kutoka na kutokuwepo miundo mbinu nchini ikiwemo udogo wa bandari, ukosekanaji wa uhakika wa maji safi na salama,kupanda kiholela kwa bei za nishati ya umeme,barabara zisizo na kiwango.
Hata hivyo alisema kuwa uhuru na fursa zinapatikana katika uingizaji wa bidhaa kutoka nje kwani ni kuijenga ushirikiano wa karibu kati ya nchi na nchi au taifa na pia ni nafasi pekee ya kuvitangaza visiwa hivyo katika sekta ya utalii na kukuza biashara nchini.
Alisema iwapo serikali itajidhatiti kusimamia kwa kina na kuboresha miundo mbinu iliyopo nchini inaweza kupiga hatua ya kukuza hali ya uchumi hasa ikizingatiwa kuwa hivi ni visiwa vyenye vivutio mbalimbali kwa wageni wanaoingia nchini.
Naye Afisa Elimu kwa walipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania, Saleh Haji Pandu alisema hakuna uthibitisho wowote juu ya tuhuma hizo, kwani hakuna mfanyabiashara hata mmoja alieshikwa na kuhusika na tuhuma hizo.
Aidha aliwataka wafanyabiashara wawe bega kwa bega katika kuhakikisha wanawafichuwa wale wote wanaokwepa kulipa kodi.
EURO MONEY YAITANGAZA BENKI YA STANBIC KUWA BENKI BORA YA UWEKEZAJI
-
• Tuzo inadhihirisha benki ya Stanbic kuongoza katika kuchochea uwekezaji,
ajira, na ukuaji wa uchumi wa taifa.
• Tuzo hii inatambua mchango wa benki kat...
48 minutes ago
No comments:
Post a Comment