Nilibahatika
kukutana na makala kwenye facebook chini
Voice of Zanzibar zenye kuanza kuwataja wauzaji wa madawa ya kulevya katika visiwa
vya Zanzibar.
Lengo na
madhumuni ya kuwataja wahusika wa madawa ya kulevya pamoja na kuweka picha zao
ni baada ya kuona serikali pamoja na jitihada zake za kupambana na maeawa ya
kulevya imeonekana kama ni mojawapo ya sehemu ya tatizo badala ya kuwa suluhisho.
Hili
limejitokeza kwa sababu mara nyingi imeonekana wanaokamatwa na kete za unga
huwa vidagaa na si papa wakati wauza unga wote wanajulikana kwa majina na
wanapouzia.
Mara kadhaa
Polisai ambao ndio wamekabidhiwa ulinzi na usalama huonekana kwa madealers
wakipewa chao ili kusitokee chochote. Ni Polisi hawa hawa kukitokea Operesheni
kamata wauza madawa wao hutoka kinyemela na kuwatonya wauza madawa kwamba ‘kesho’
wazee wanakuja kwa hivyo walale mbele.
Ni Polisi hawahawa sasa wakionekana wao wenyewe wakishiriki katika kuuza baada ya kukamata.
Ujasiri walioonesha
Voice of Zanzibar kwa kuwataja moja kwa moja bila ya kificho na kubainisha jinsi
wanavyouza madawa haya ni wa kupigiwa mfano kwa upande mmoja. Kwani kuwaname
and shame these people kunaweza kuwaadhirisha na kama ni binadamu wenye akhlaaq, haya na
staha wanaweza kusikia aibu na asaa Mola awahidi waachane na biashara hii. La wakiwa hawana chembe ya akhlaaq, maadili au staha basi wataendelea
na shughuli yao kama kawaida.
Kwa upande mwengine kulijitokeza changamoto
nyingi katika mtandao wa facebook wakati wengi walipinga watu hawa kutajwa
hadharani kwa kuomba kuwepo ushahidi tosha wa kuwatia hatiani na si dhana na
tuhuma ambazo mwishowe ni kuhusudiana tu badala ya kusaidiana na wengine
wakidai every one should mind his/her own business.
Udogo wa kisiwa
cha Zanzibar hauhitaji rocket science kuweza kuwajua wanaouza madawa ya kulevya vidagaa
mpaka mapapa. Ni watu tunaoishi nao tunaocheza nao tunaoshirikiana nao na
wengine kufaidi matunda yao bila ya kujali upatikanaji wa mali zao kama ni
halali au haramu. Badala ya kujali madhara makubwa wanaosababisha wauza unga
sasa tumeanza kufungua vitengo vya kuwatibu waathirika wa madawa ambao ni baba
zetu, mama zetu, kaka zetu, dada zetu, watoto wetu au rafiki kama si majirani
wetu.
Hili suala la
madawa ya kulevya limefanywa kuwa gumu sana kutokana na wahusika kuifanya hii
kazi kwa usiri mkubwa. Pia kuweza kuwatia hatiani watu wa aina hii kwa Zanzibar
limekuwa ni ndoto kwa nchi inayodai inafuata utawala wa sheria na dhana utawala
bora kwani uwezo wa fedha waliokuwa nao unawaogopesha mpaka Polisi, viongozi
wa Serikali na kadhalika. Hufanya walitakalo kwa nguvu ya pesa ya haramu ya
madawa ya kulevya.
Tatizo baya
zaidi ni vipi jamii hii inayoathirika na madawa haya kuwasifu madealers kwamba
ni watu smart, wajanja na walioula. Hata jamii ikiwa na shida ndogo ndogo basi huwafuata hawa hawa madealers kwa misaada.
Niliwahi
kujaribu kuwasiliana na mtaa mmoja ulioathirika vibaya na madawa na kukutana na wazee
wa mtaa huo kujaribu kuwafahamisha kwamba suala hili sasa si la kipolisi wala
serikali maana wameshindwa, lakini sisi kama Wazazi, wanajamii tunaweza
kulivalia njuga suala hili ikiwa tutakuwa na dhamira ya kweli. Kwani waathirika
tunawajua wauza madawa tunawajua kufikia mtoto mdogo hata akili haijapevuka
lakini mtaani anajua kwamba nyumba fulani inauzwa madawa na fulani ni teja.
Nilijibiwa
kwamba kazi hii ni ngumu kwa sababu italeta fitna kubwa mtaani kwani nyumba
hizi tayari imekuwa hii ni tijara ya kuwaendeshea maisha yao. Si wao bali
wengine wa mtaani hufaidika na uwepo wa wauza unga (wenye biashara ndogo
ndogo).
Hivi ndivyo
jamii zetu zisizojiamini zilipofikia, zimekoseshwa nyenzo za kuweza kuifanyia
kazi jamii. Zimeweza kuwapa wauza unga nguvu zisizo mfano huku wakijigamba
ikiwa polisi wameshindwa mtaweza nyie?
Ukweli hali ni
mbaya sana na inakithiri kuwa mbaya kila siku zikiendelea tuombe Mungu
atusaidie na janga hili kutokana na sababu nyingi za kielimu, kimaisha na
kuiga ambazo matunda yake ni haya ambayo
tunayachuma sasa kwa kuwa na Sober Houses, Waathirika wanaokwenda na kurudi ( relapse) ,
ndoa kuharibika, nyumba kuharibika na kadhalika ni kweli maneno ya wahenga tusipoziba ufa, tutajenga ukuta.
Yaa Rabb –
Tuokoe na janga hili
No comments:
Post a Comment