Habari za Punde

CCM yashinda Ulanga, Bangata, CHADEMA yatetea Morogoro



Joseph Ngilisho na Rose Chapewa, Morogoro

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefanikiwa kutetea kiti cha Udiwani katika uchaguzi mdogo uliofanyika kata ya Mtibwa wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro , baada ya mgombea wake Mwakambaya Lucas Edward, kushinda.

Katika uchaguzi huo mdogo ambao vyama vitatu vya siasa vilisimamisha wagombea wake, Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mvomero, Sara Linuma, alimtangaza Mwakambaya kuwa mshindi wa kiti hicho kwa kupata kura 3,096.

Wagombea wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ni Mussa Hassan Kingu wa chama cha Mapinduzi aliyepata kura 1,372 na mgombea wa chama cha Wananchi CUF, Khalid Juma Mgonja, aliyeambulia kura 67.

Uchaguzi huo mdogo wa udiwani ulifanyika Jumapili na matokeo yake kutangazwa majira ya saa nne usiku, ikiwa ni baada ya kata hiyo kuwa wazi, baada ya aliyekuwa Diwani wake, Tusekile Mwakyoma, kutoka (CHADEMA) kufariki dunia mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kuchomwa kisu na aliyedaiwa kuwa ni mpenzi wake.

Katika uchaguzi mwingine mdogo wa udiwani uliofanyika wilayani Ulanga kata ya Mahenge mjini, mgombea udiwani kupitia CCM, Mark Stephen Asenga, aliweza kuibuka kidedea kwa kuwashinda wagombea wa CHADEMA na CUF.

Akitangaza matokeo hayo, Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Godwin Kamguna, alisema Asenga alishinda kwa kupata kura 710, huku mpinzani wake wa karibu, Baltazar Kizee wa CHADEMA akipata kura 444 na Msham Mbunda wa CUF akipata kura 14.

Jumla ya watu 1,173 walipiga kura, ambapo kura halali zilikuwa 1,168 huku kura tano zikiribika.

Mjini Arusha, mwandishi wetu Joseph Ngilisho, anaripoti kuwa Chama cha Mapinduzi kimefanikiwa kutetea kiti cha udiwani katika kata ya Bangata wilayani Arumeru, ambapo mgombea wake,Olais Msere alitangazwa mshindi kwa kupata kura 1177 na kumtupa mbali hasimu wake kutoka
CHADEMA, Erick Mollel aliyeambulia kura 881 na kufuatiwa na mgombea wa TLP aliyepata kura 3.

Akitangaza matokeo hayo Msimamizi wa uchaguzi mdogo katika kata hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Halifa Hida alisema jumla ya wapiga kura katika kata hiyo walikuwa 4190 ,waliopiga kura walikuwa 2061 na kura 34 ziliharibika.

Alisema jumla ya vyama vitatu vilisimamisha wagombea katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo ambapo chama cha Chadema kilimsimamisha mtoto wa aliyekuwa Diwani wa kata hiyo ,Erick Samsoni aliyehamia Chadema baada ya baba yake,Samson Mollel (CCM) kufariki dunia.  Wakati huo huo CCM kimepata pigo baada ya kata waliokuwa wakiishikilia ya Daraja Mbili kunyakuliwa na Chadema .

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana,jumla ya vyama vitano vilisimamisha wagombea wake,ambapo CCM,ilimsimamisha,PhilpMushi,CHADEMA,Prosper Msofe,CUF,NCCR Mageuzi na TLP.

Akitangaza matokeo hayo, Afisa Mtendaji wa kata ya Daraja Mbili ,Modestus Lupogo alimtangaza ,Prosper Msofe(Chadema) kuwa mshindi kwa kupata kura 2193 dhidi ya mgombea wa CCM aliyepata kura 1324 na kufuatiwa na mgombea wa CUF kura 162,NCCR Mageuzi kura 22 na TLP kura 42.

Lupogo alisema jumla ya wapiga kura 16,295 walijiandikisha na idadi ya waliopiga kura walikuwa 3743 ,kura zilizoharibika ni 22.

Awali uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu za hapa na pale na kusababisha wafuasi 10 wa Chadema kushikiliwa na polisi na kufikishwa mahakamani,huku magari kadhaa likiwemo la aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini , Godbless Lema kushikiliwa na polisi.

Pia watu kadhaa walijeruhiwa akiwemo mfuasi wa CCM kukatwa panga mkononi huku mfuasi wa Chadema akijeruhiwa kwa kupigwa chupa kichwani
.

Wakati huo huo wafuasi wa vyama vya CCM na Chadema wamekuwa wakishutumiana kutokana na mtu ambaye hakufahamika mara moja kufyatua risasi hewani wakati zoezi la kupiga kura likiendelea hatua iliyozua hofu ya watu kukimbia ovyo kwa lengo la kujinusuru.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.