Na
Mwandishi maalum, Marekani
MATAJIRI
wawili wakubwa duniani wameichangia Tanzania kiasi cha shilingi bilioni
24.1 kwa ajili ya kuendeleza afya ya akinamama na kusaidia uzazi salama hasa
katika maeneo ya vijijini.
Matajiri
hao, Michael Bloomberg ambaye ni Meya wa jiji la New York, Marekani na Mama
Helen Agerup wa Sweden, wametangaza mchango wao huo mkubwa kwa Tanzania kwenye
mkutano maalum wa waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Umoja wa
Mataifa mjini New York, Marekani.
Pamoja
na matajiri hao katika mkutano huo wa waandishi wa habari walikuwepo ni Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Kati
ya fedha hizo, Meya Bloomberg alitoa kiasi cha dola za Marekani milioni nane
kupitia taasisi yake ya Bloomberg Philanthropies wakati mama Agerup alitoa
kiasi cha dola milioni 7.5 kupitia taasisi yake na mumewe ya H&B Agerup
Foundation.
Meja
Bloomberg amekuwa anasaidia afya ya akinamama na juhudi za uzazi salama katika
maeneo ya vijijini nchini Tanzania
tokea mwaka 2006 wakati hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Taasisi ya H&B kuungana
na Bloomberg Philanthropies kusaidia sekta ya afya Tanzania.
Akizungumza
kwenye shughuli hiyo, Meya Bloomberg alisema yeye na taasisi yake wameamua
kuendelea kuunga mkono jithada za Tanzania katika kuinua afya ya
akinamama na kupunguza vifo vya uzazi kwa sababu ya matokeo mazuri ambayo
yamepatikana tokea Bloomberg Philanthropies aanze kuunga mkono jitihada hizo za
serikali mwaka 2006.
Alisema
taasisi yake inajihusisha katika maeneo mawili makubwa.
Eneo
moja ni kujenga na kukarabati vituo vya afya na zahanati katika maeneo ya
vijijini na pili ni kutoa mafunzo kwa watu wasiokuwa watalaam wa afya pamoja na
wakunga kuweza kusaidia uzazi salama vijijini.
Mpaka
sasa taasisi hiyo imefundisha kiasi cha watu 106 kuweza kufanya kazi ya uzazi
salama na ukunga chini ya msaada wake kwa Tanzania.
“Tunaona
matokeo ya kuvutia sana.
Hata kama idadi ya akinamama wanaopoteza maisha haijawa ya chini –akinamama 13
kati ya 1,000- kama ile ya Marekani lakini
dhahiri kuwa idadi inapungua kwa kiasi cha kutia moyo,” alisema.
“Zaidi tunaifanya kazi hii katika Tanzania kwa
sababu tunashughulika na Rais Kikwete, kiongozi mbunifu, kiongozi mkweli na
muadilifu, kiongozi mchapakazi na anayetaka kuonyesha tofauti katika maisha ya
wananchi wake,” alisema.
Naye
mama Helen Agerup alisema alitembelea Tanzania
mwaka jana baada ya kushawishiwa na binti yake ambaye alikuwa ametembelea Tanzania mapema
na kuvutiwa na jitihada za serikali na zile za Taasisi ya Bloomberg kuhusu afya
ya akina mama.
“Nilivutiwa
sana na kazi inayofanywa na serikali ya Tanzania na taasisi ya Bloomberg kuzuia
vifo vinavyosababishwa na mambo yanayoweza kuzuilika yaani kutokwa damu kupita
kiasi na magonjwa ya kuambukiza kutokana hasa na tatizo la ukimwi,” alisema
mama huyo.
Naye
Rais Kikwete alimshukuru Meya Bloomberg na mama Agerup akisema kuwa misaada yao inaleta tofauti kubwa katika afya za akinamama katika Tanzania.
No comments:
Post a Comment