Na Mwanajuma Mmanga
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imewataka wazee wa mjini na
vijijini kukaa mkao wa kula wakati wakisubiri kukamilika sera ya hifadhi ya
jamii kwa maslahi.
Kauli hiyo ameitowa Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Mwinyihaji Makame wakati wa sherehe ya
siku ya wazee duniani zilizofanyika nyumba ya wazee Sebleni.
Dk. Mwinyihaji
alisema serikali iko katika mchakato wa kuandaa sera ya hifadhi ya jamii
ambayo itazungumzia maslahi ya makundi yote katika jamii ikiwa ni pamoja na
wazee.
Alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia
wazee kutokana na wao kuwa ni miongoni mwa watu wanaohitaji huduma na matumizi
bora.
"Hatua hii itawezesha kuwasaidia wazee kwa
kuwapunguzia umasikini, ambao faida itakuwa kwa wazee wote waliofanya kazi
katika serikali na wale waliofanya kazi zao za binafsi," alisema Dk.Mwinyi.
Alisema katika kuhakikisha serikali inaweza
kutimiza hilo
tayari imeanza kuwajengea uzio wazee hao katika nyumba wanazoishi sebleni.
Nae Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo, Vijana, Wanawake
na Watoto, Zainab Mohammed alisema Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliweka misingi
imara ya kuwatunza, kuwaenzi na kuwathamini wazee bila ubaguzi.
Hivyo alisema wazee wanahitaji matunzo na misaada
kutoka kwa watoto waliowazaa, ndugu, jamaa, mashirika na serikali.
Nae afisa kutoka shirika la kimataifa la kusaidia
wazee (Help Age),Amlesset Teworos
alisema hali ya afya bora kwa wazee ni jambo la msingi kwani ni rasilimali
muhimu kwa taifa.
Siku ya wazee duniani huadhimishwa kila ifikapo
Oktoba 1.
No comments:
Post a Comment