Habari za Punde

Wachimbaji wadogo 900,000 kupoteza ajira


 Na Jumbe Ismailly,Singida     

 CHAMA cha watafiti na wachimbaji wadogo wa madini (SIREMA) mkoa wa Singida kimesema endapo serikali itaendelea na msimamo wake wa kupandisha gharama za kulipia viwanja vya uchimbaji madini kuna hatari ya wachimbaji wadogo 900,000 wanaotegemea kujipatia kipato chao kupitia shughuli za madini watakuwa wamepoteza ajira zao.
   
Katibu Mkuu wa SIREMA mkoa wa Singida, alitoa kauli hiyo wakati akitoa tamko kwa waandishi wa habari kuhusu kupinga kupanda gharama za kulipia viwanja vya uchimbaji madini pamoja na shughuli zinginezo zinazohusu madini.

Katibu Mkuu huyo, alisema tamko hilo limetolewa na kikao cha kamati tendaji ya chama hicho kilichokutana kwenye ofisi zake zilizopo mjini hapa.


“Sisi wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Singida kupitia kamati ya Tendaji ya chama tumelazimika kutoa tamko letu kuhusu kupanda gharama za ulipiaji wa viwanja vya kuchimba madini na gharama zingine zihusuzo na shughuli zetu,” alisisitiza  Marando.

Aidha  Katibu huyo alifafanua kuwa serikali kupitia wizara ya nishati na madini ilipandisha gharama hizo mwaka 2010 na hatimaye kupandisha tena gharama hizo Julai,27,mwaka huu na kwamba kupanda huko kumefanyika bila kufanya utafiti wa kina kama zinalipa au la.

Aliweka bayana kwamba kupanda kwa gharama hizo kunalenga zaidi kuondoa Watanzania wazalendo wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji madini na kuwanyang’anya maeneo ya uchimbaji mdogo ili kuwapa wageni ambao wao hupewa misaada na nchi zao.

Kwa upande wake mmoja ya  wachimbaji wadogo,Mather Kayaga, alifafanua kuwa kwenye sekta ya madini wanawake ni asilimia 25 tu ya wachimbaji wote na kwamba hawachimbi kibiashara bali hufanya kazi hiyo kwa lengo la kuisaidia familia zao.

“Mimi binafsi nimepatwa na mshituko mkubwa sana baada ya kusikia ongezeko la ada hiyo na siamini kabisa kama nitaweza kulipa kiwango hicho kikubwa kiasi hicho,”alisema

Naye Julius Madembwe alisisitiza kuwa wachimbaji wadogo ndio wenye historia ya madini na wachimbaji wakubwa hupata kwa kupitia kwao.

Kwa upande wake Philip Mwembe alisema imekuwa kawaida ya serikali kutoa ahadi na kushindwa kuzitekeleza na hivyo kutumia fursa hiyo kuikumbusha ahadi iliyotolewa kwenye kikaoa cha Bunge la bajeti la 2012/2013 kwamba kuna shilingi bilioni tisa kwa ajili ya wachimbaji wadogo,nao wanufaike nazo badala ya kuendelea kuzisikia kwa wengine wanaopata upendeleo huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.