Habari za Punde

Wazazi CCM wachaguana




Na Madina Issa
 JUMUIYA ya Wazazi Mkoa wa mjini Magharibi imemchagua  Ali Othman Said kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo baada ya kupata kura  71.

Mwengine waliochaguliwa ni wajumbe watatu wa baraza la Mkoa ambao ni Mohamed Said Dimwa, Najma Mutaza Giga na Sufiani Ramadhan Khamis.

Aliyepata nafasi ya kuwakilisha baraza kuu taifa pamoja na mkutano mkuu taifa CCM ni Saleh Said Abdallah ambae amepata kura 67.

Mjumbe mmoja anaewakilisha Halmashauri Kuu na mkutano mkuu Mkoa ni Nassibu Mohamed Haji ambae amepata kura 55, mjumbe mmoja wa baraza kuu Wilaya ya Aman ni Mwalim Haji Ameir aliyepata kura 55.


Wengine ni mjumbe wa baraza kuu Wilaya ya mjini ambao ni Maulid Suleiman Juma, mjumbe mmoja atakae wakilisha UWT Mkoa ambae ni Hakiba Khamis, pamoja na mjumbe mmoja wa kuwakilisha vijana Hassan Jecha aliepata kura 88.

Wakitoa neno la shukurani viongozi hao waliahidi kuwa watakitetea chama na kukilinda kwa maslahi ya wote na sio kwa mtu mmoja.

Akifungua mkutano huo,  Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Asha Abdallah Juma aliwataka wajumbe kuchagua viongozi bora na sio bora viongozi ili kuweza kukipa ushindi chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu 2015.


Alisema endapo wanajumuiya hao watakachagua viongozi waliokuwa makini, imara na waaminifu wataweza kukivusha chama hicho katika chaguzi mbalimbali zinazokuja.

Katibu huyo alisema CCM ndio chama pekee kilichokuwa imara na chenye demokrasia makini ya kuongoza hivyo wasisite kukipatia viongozi waliokuwa imara kwa maslahi ya wananchi wote.

"Katika nchi hii chama chenye demokrasia makini ya kuongoza ni CCM mimi sioni sababu ya kukibeza chama hichi, kwani mtu yeyote anayekibeza nahisi ameishiwa sera za kufanya," alisema Asha.

Alisema kuna baadhi ya wapinzani wanasema CCMkimepoteza muelekeo, lakini alisema wanasiasa hao wanajidanganya na wanawambia uongo wafuasi wao.

Hata hivyo aliwasihi watakaochaguliwa katika nafasi hizo wawe waadilifu na waaminifu katika utendaji wa kazi zao.

Akizungumzia mchakato wa katiba aliwasihi wanajumuiya hao kutoa maoni yao yaliyokuwa imara na sahihi yatakayoendelea kuudumisha muungano.

Nae Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Yussuf Mohamed Yussuf aliwahimiza  wanaCCM kulinda chama chao ili kuweza kukisongesha mbele katika gurudumu la siasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.